RAIS SAMIA : SERIKALI IMERUHUSU WANANCHI WALIOAJIRIWA NA WALIOJIAJIRI KUJIWEKEA AKIBA KATIKA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
*Amesema Tanzania mambo ni moto moto
*Mhe. Makonda aishukuru NSSF kuwafikia wananchi waliojiajiri mkoani Arusha
*Kupitia kampeni ya Staa wa Mchezo wa NSSF wengi wahamasika kujiunga
Na MWANDISHI WETU,
Arusha. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanyika ni kuiruhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa nafasi kwa sekta binafsi na sekta ya Waliojiajiri kupata fursa ya kujiwekea akiba katika Mifuko hiyo.
Mhe. Rais Dkt. Samia amesema hayo tarehe 8 Machi, 2025 katika sherehe za Siku ya Wanawake Duniani 2025 ambayo kitaifa imefanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
"Lakini jengine katika hifadhi ya jamii ni pale tuliporuhusu Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii itoe madirisha ambayo sekta binafsi na sekta isiyo rasmi na yenyewe itapata ridhaa ya kujiwekea hifadhi katika Mifuko yetu," amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Mhe. Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa jambo hilo linafanywa vema na kwa hiyo Tanzania mambo ni moto moto.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kwa kazi kubwa uliyofanya katika Mkoa huo ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na kuandikisha wanachama waliojiajiri.
"Lakini pia niwashukuru sana NSSF wamefanya kazi ya tofauti sana, wananchi wa Mkoa wa Arusha wamejiunga sasa wana uhakika wa kuwa na pensheni hata wale ambao sio wafanyakazi wa Serikali. Mfumo huu ulioufanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni bora sana, ambao unamtengenezea mazingira mwananchi wa kawaida kuwa na akiba lakini pia kupata matibabu katika mazingira mazuri," amesema Mhe. Makonda.
Elimu hiyo kwa wananchi waliojiajiri imefanyika jijini Arusha, kupitia kampeni ya ‘NSSF Staa wa Mchezo’ ambayo ilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam na Mhe. Ridhiwani Kikwete, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, katika viwanja vya Zakhem Mbagala, ambapo inaendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Katika kampeni hiyo ya ‘NSSF Staa wa Mchezo’ inafikisha elimu kwa wananchi waliojiajiri kujiunga na ‘Hifadhi Scheme’ kwa kuchangia kidogo kidogo kwani unabofya *152*00# ambapo mwanachana anaweza kuchangia shilingi 30,000 au zaidi kwa kutoa kidogo kidogo kwa siku bukubuku, kwa wiki, kwa mwezi au kwa msimu kulingana na kipato chake. Kupitia michango yake atanufaika na mafao ya matibabu na mafao ya uzeeni. Pia Mwanachama atachangia Shilingi 52,200 kwa ajili yake na wategemezi wake watano yaani mke au mume na watoto wanne, ambao watanufaika na mafao ya matibabu.
Katika Jiji la Arusha, utoaji huo wa elimu uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba katika soko la Kilombero ambapo mamia ya Wananchi waliojiajiri walifanikiwa kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha bora ya sasa na ya baadaye.
Staa wa Mchezo ni wananchi ambao wamejiajiri kupitia Sekta ya Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Madini (wachimbaji wadogo wadogo), Usafirishaji (Boda boda na Bajaji), Sekta ya Biashara Ndogo-Ndogo (Machinga, Mama/Baba Lishe, Ususi, Muuza mkaa, muuza nyanya na Staa wengine wote). Ujio wa 'Hifadhi Scheme' unatoa nafasi kwa NSSF kushika usukani na kuwa ‘Staa wa Mchezo’ katika maisha ya uzeeni au pindi majanga yanapotokea kwa wananchi waliojiajiri ambapo NSSF inakuhakikishia inalinda leo na kesho yako kwa kutoa huduma na mafao mbalimbali kwa mujibu wa Sheria.
NSSF STAA WA MCHEZO, HIFADHI SCHEME- HIFADHI YA JAMII KWA WOTE
No comments