Breaking News

NSSF YAWATAKA WATANZANIA KUJIWEKEA AKIBA

 




*Yasema imenzisha skimu maalumu kwa ajili waliojiajiri wenyewe pamoja na walioajiriwa lakini wanapenda kujiwekea akiba 

Na MWANDISHI WETU,
Dodoma. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia NSSF ili waweze kujikinga na majanga kama vile uzee na ukosefu wa kipato kwa kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko.

Aidha, NSSF imesema imenzisha skimu maalumu kwa ajili ya kuwafikia wananchi waliojiajiri wenyewe wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine ili waweze kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema.

Hayo yalisemwa na Meneja wa NSSF wa sekta isiyo rasmi, Bi. Rehema Chuma, tarehe 20 Novemba 2024 jijini Dodoma kwenye mkutano wa Chama Cha Wahasibu Wanawake Tanzania. 

Amesema NSSF umeanzisha mpango wa kitaifa kwa sekta isiyo rasmi kwa lengo la kuwafikia watanzania wote waliojiajiri wenyewe ambapo wanaweza kujiwekea akiba kwa kima cha chini cha shilingi 30,000 ambapo atanufaika na mafao pamoja na huduma ya matibabu kwa mtu mmoja na atakeyejiwekea akiba ya 52,200 atanufaika na mafao pamoja na huduma za matibabu yeye mwenyewe na familia yake na kuwa mtu anaweza kuchangia hata shilingi 1000 kwa siku.

Amesema utaratibu wa kujichangia ni rafiki na rahisi sana ambapo unaweza kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo na kuwasilisha michango popote ulipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za Mfuko au kutumia wakala.

"Kujiunga na skimu hii ni rahisi sana unaweza kutumia simu ya kiganjani kwa kupiga *152*00# kisha unaenda namba 3, kisha unaenda namba 6 unachagua NSSF, kisha namba Moja ambapo utaingiza namba ya NIDA na hapo hapo utakuwa umesajiliwa ambapo pia unaweza kutumia mfumo huo kujilipia michango yako na kuangalia taarifa nyingine," amesema Bi. Rehema.

Kuhusu skimu ya uchangiaji wa ziada, Bi. Rehema asema ni kwa ajili ya Watanzania walioajiriwa lakini wanapenda kujiwekea akiba kwa hiari ili kuongeza kipato wakati wa kustaafu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahasibu Tanzania, Tumaini Lawrence, ametoa wito kwa wahasibu ba wataalamu wa kada nyingine kuchangamkia fursa ya kujiunga na kuchangia NSSF kupitia mpango wa ziada (Supplementary Scheme) na wa sekta isiyo rasmi ili waweze kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema.

"Katika mkutano huu tupo na ndugu zetu wa NSSF ambao wapo hapa kwa ajili ya kutupa elimu hasa kupitia skimu ya uchangiaji wa ziada pamoja na ile ya sekta isiyo rasmi ambapo unaweza kujiwekea akiba hata kama ni mwajiriwa wa Serikali NSSF wanakuruhusu kujichangia kwa ajili ya kesho iliyokuwa njema," amesema Bi. Tumaini.

Kwa upande wake, Bw. John Masatu, Afisa Matekelezo kutoka sekta isiyo rasmi amesema mwanachama anaweza anaweza kujisajili popote alipo kwa kutumia simu ya kiganjani na kuwa wataendelea kuwafikia wananchi wengi wengi zaidi kuwapa elimu ya hifadhi ya jamii na kuwahamasisha kujiunga.




 

No comments