EMEDO NA TMA WAZINDUA MFUMO MPYA WA UTOAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA WAVUVI
Na Tonny Alphonce,Goziba
Katika
juhudi za kuhakikisha usalama wa Wavuvi na Wadau wa uvuvi katika Ziwa Victoria, Shirika la
Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Utabiri wa Hali ya Hewa (TMA) Kanda ya Ziwa, wamezindua mfumo mpya wa utoaji wa
taarifa za hali ya hewa kwa jamii ya wavuvi wa Kisiwa cha Goziba.
Mfumo huu wa
utoaji wa taarifa za hali ya hewa unategemea mabango maalumu yatakayotumika
kuonesha hali ya hewa kwa urahisi, ili wavuvi na wadau wa shughuli za uvuvi
waweze kupata taarifa kwa wakati na kuelewa hali ya hewa kabla ya kuingia
ziwani.
Hatua hii
inakuja baada ya utafiti uliofanywa na EMEDO mwaka 2021, ambao ulibaini kuwa
moja ya sababu za ajali za mara kwa mara za kuzama kwa wavuvi ni upungufu wa
taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa wakati sahihi na uelewa wa taarifa hizo.
Utafiti wa
EMEDO ulionyesha kuwa wavuvi wengi wamekuwa wakikosa taarifa sahihi za hali ya
hewa, hali inayosababisha ajali za kuzama na kupoteza maisha kwa baadhi yao.
Ili kutatua changamoto hiyo, EMEDO kwa kushirikiana na TMA wameanzisha mfumo
huu wa mabango.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mabango hayo, Meneja wa TMA Kanda ya Ziwa, Augustino Nduganda, alielezea umuhimu wa mfumo huo kwa wavuvi na wadau wote wa uvuvi.
"Tumefikia hatua hii kutokana na utafiti uliofanywa na wenzetu wa EMEDO. Tulikaa chini tukajiuliza mfumo gani ungekuwa rahisi na bora kwa wavuvi, na tukapata jawabu la mabango haya. Kwa picha tu, mnaweza kujua hali ya hewa ikoje kwa siku hiyo," alisema Nduganda.
Nduganda
aliongeza kuwa taarifa za hali ya hewa zitakuwa zinatolewa mara mbili kwa siku.
Saa sita mchana kwa ajili ya wafanyabiashara wa samaki, na saa tisa alasiri kwa
wavuvi wanaoelekea ziwani usiku.
Arthur
Mgema, Meneja wa Mradi wa Kuzuia Ajali za Kuzama kwa Wavuvi kutoka EMEDO,
alitoa wito kwa wavuvi wa Kisiwa cha Goziba kutumia mabango haya kabla ya
kuingia ziwani.
Alisema kuwa mfumo huo umekuwa ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za kutatua changamoto zinazosababisha ajali kwa wavuvi.
"Kupitia
mradi huu wa kuzuia kuzama maji, tumekuwa tukitatua changamoto moja baada ya
nyingine tukiongozwa na utafiti wetu wa mwaka 2021.
Taarifa
sahihi za hali ya hewa ni jambo ambalo wavuvi walikuwa wanahitaji sana, na sasa
limefanyiwa kazi," alisema Mgema.
Utafiti uliofanywa na Shirika la EMEDO mwaka 2021 ulibaini sababu mbalimbali zinazopelekea Wavuvi kuzama maji na wengine kupoteza maisha na sababu moja wapo ilibainika kuwa ni changamoto ya upatikana wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa wakati na uelewa kuhusu taarifa zenyewe na ili kutatua changamoto hiyo EMEDO na TMA wamefanikiwa kuja na mabango yatakayotoa taarifa za hali ya hewa kwa jamii ya wavuvi na kwa kuanza wameanza na kisiwa cha Goziba.
No comments