Breaking News

KUELEKEA CHAGUZI ZIJAZO TAKUKURU MWANZA YAKUTANA NA ASASI ZA KIRAIA

 Na Tonny Alphonce,Mwanza



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mwanza imefanya kikao maalum na asasi za kiraia katika jitihada za kuelimisha umma kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza, James Ruge, alisema rushwa imekuwa kikwazo kikubwa katika kuleta maendeleo nchini. 

Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa makundi yote katika jamii kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya rushwa, hasa kipindi hiki cha uchaguzi.

Ruge alieleza kuwa, kwa mujibu wa Mkakati wa Kitaifa wa TAKUKURU (PCCA), taasisi hiyo ina jukumu la kushirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kupambana na rushwa. Kwa mantiki hiyo, TAKUKURU imeanzisha mpango maalum wa kukutana na makundi tofauti ya jamii, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, viongozi wa dini, na asasi za kiraia.

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza, James Ruge akisisitiza jambo kwa  washiriki wa kikao cha viongozi wa asasi za kiraia kilichofanyika katika ofisi za TAKUKURU Mwanza
Lengo ni kuimarisha uelewa wa namna ya kuzuia rushwa, kuwakumbusha wananchi kuhusu maadili mema, na kuwahamasisha kuripoti vitendo vya rushwa hasa wakati wa uchaguzi.

"Idadi ya watu mkoani Mwanza imefikia milioni 3.2, na hivyo TAKUKURU peke yake haiwezi kuwafikia wote. Hii ndiyo sababu tumeanzisha utaratibu wa kukutana na makundi maalum ili kuhakikisha elimu ya kuzuia rushwa inawafikia watu wengi zaidi," alisema Ruge.

Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Lilian Macha, aliwataka wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa za uongozi bora na wanaojihusisha na shughuli halali za kujipatia kipato.

Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Lilian Macha akiongea na ashiriki wa kikao cha viongozi wa asasi za kiraia kilichofanyika katika ofisi za TAKUKURU Mwanza
Alisisitiza umuhimu wa kuwa makini katika kuchagua viongozi watakaowakilisha vyema jamii kwenye ngazi ya mtaa na ngazi nyinginezo za uongozi.

Pia alihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi kwa kuwa ni haki yao ya kikatiba kuchagua na kuchaguliwa.

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi, Eli Makala, alisisitiza jukumu muhimu la asasi za kiraia katika kuelimisha jamii kuachana na dhana potofu ya kutumia uchaguzi kama msimu wa mavuno.

Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi, Eli Makala akiwasilisha mada ya nafasi ya asasi za kiraia katika kupambana na rushwa

Aliwaonya wananchi dhidi ya kujihusisha na vitendo vya rushwa, akisema kufanya hivyo kutawezesha kuchaguliwa kwa viongozi wasiofaa na kukiuka sheria za uchaguzi.

Makala aliwahimiza viongozi wa asasi za kiraia kushirikiana na taasisi za umma kama TAKUKURU katika kutoa elimu ya uraia, elimu ya kupiga kura, na mapambano dhidi ya rushwa.

Pia alihimiza umuhimu wa kufanya utafiti na kutoa mafunzo kuhusu masuala ya utawala bora na maadili ya uchaguzi ili kuboresha mchakato mzima wa uchaguzi.

Baadhi ya washiriki kutoka taasisi mbalimbali wakifatilia wa kikao maalum kati ya TAKUKURU Mwanza na Asasi za kiraia 

Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uadilifu na uwazi katika mchakato wa uchaguzi, ambapo wananchi na makundi mbalimbali wanaendelea kushirikishwa. Rushwa ina madhara makubwa kwa maendeleo ya nchi, hivyo ushirikiano kati ya taasisi za umma na asasi za kiraia ni muhimu katika kufanikisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, hasa kuelekea uchaguzi.

No comments