Breaking News

SARATANI KWA WATOTO INATIBIKA ENDAPO ITAWAHIWA

 Na Tonny Alphonce, Mwanza

Yunis Mutayoba, mama wa mtoto mmoja wa kiume, mkazi wa Nyamadoke mkoani Mwanza, alishuhudia jinsi madaktari walivyogundua mapema saratani ya jicho kwa mtoto wake na kuyakomboa wa maisha ya mtoto wake.

Yunis anaeleza kuwa ilimchukua miaka minne kugundua kuwa mtoto wake mwenye umri wa miaka minne alikuwa na saratani ya jicho.

"Nilikuwa sijui kama mwanangu ana tatizo kubwa, mpaka siku moja rafiki yangu, ambaye ni muuguzi, aliniambia jicho la mtoto wangu halipo sawa na akanishauri nionane na daktari," anasema Yunis.

Baada ya kufika hospitali ya Bugando, vipimo vilifanywa kwa kutumia tochi maalumu kwa ajili ya macho, na ndipo walipogundua kuwa mtoto wake alikuwa na saratani ya jicho.

Yunis anasema aliogopa sana na alihisi kama ameanza kumpoteza mwanaye,lakini daktari alimhakikishia kuwa ugonjwa huo ulikuwa bado katika hatua za awali na kwamba mtoto wake anaweza kutibiwa na kupona.

Dkt. Kashindye Mayolwa, kutoka kitengo cha saratani, anasema kuwa watoto wengi wenye umri kati ya miaka 1 hadi 8 wameshambuliwa na saratani bila wazazi kugundua mapema.

Hii inasababisha watoto wengi kufika hospitali wakiwa na saratani katika hatua za mwisho, ambapo matibabu huwa magumu na mara nyingi hufariki dunia.

Dkt. Mayolwa anaeleza zaidi kuwa uchunguzi uliofanywa Bugando mwaka 2023 ulionyesha kuwa idadi kubwa ya watoto walikuwa na saratani ya macho, lakini pia waligundua watoto wengi wakiugua saratani ya misuli, saratani ya figo, saratani ya damu, saratani ya mifupa, saratani ya ubongo, na saratani ya figo.

“Kwa sasa, Bugando imeanzisha utaratibu wa kuwapima watoto macho mara tu wanapozaliwa ili kugundua mapema kama wana saratani ya macho, na tumefanikiwa kuwaokoa watoto wengi kupitia matibabu ya mapema,” anasema Dkt. Mayolwa.

Amewashauri wazazi na walezi kuwa makini na kuwapeleka watoto hospitali mara tu wanapoona dalili zisizo za kawaida. "Saratani inatibika endapo itagundulika mapema," anasisitiza.

Profesa Suleiman Mwenda, mkurugenzi wa utafiti na maendeleo wa shirika la Revoobit, anawahimiza wazazi kufuatilia afya za watoto wao mara kwa mara.

Amesema shirika la Revoobit limefanikiwa kutengeneza dawa zinazosaidia kuzalisha seli mpya mwilini, ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wa saratani, hasa wale ambao seli zao zimeathiriwa na ugonjwa huo.

Kwa upande mwingine, Isack Sindano mwenyekiti wa shirika la African Child Comforters Organization, anasema shirika lao limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kuhusu saratani na kusaidia watoto wenye saratani kupata matibabu.

Ameongeza kuwa wanaowasaidia watoto wenye umri wa kwenda shule kwa kuwapatia elimu pia shirika hilo pia linashirikiana na taasisi nyingine ili kuhakikisha wazazi wanapata elimu ya kutosha kuhusu saratani na umuhimu wa uchunguzi wa afya kwa watoto.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Tanzania, kila mwaka, watoto wapya 1,300 sawa sana watoti 108 kwa mwezi na  ama watoto wanne kwa siku  hugundulika na saratani.

No comments