TAMASHA LA 7 LA JINSIA NGAZI YA WILAYA 2024 KUFANYIKA KONDOA AGOSTI 27-29
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Zaidi ya Wanaharakati na Wadau 300 wanaotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini kutoka pande mbalimbali za nchi wanatarajia kushiriki katika Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 katika Viwanja vya Sabasaba, Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma kuanzia Agosti 27-29 , 2024 kwa ajili ya kusherehekea mafanikio na kutathmini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo.
Akitoa Tamko leo Jumatatu Agosti 26,2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi amesema Tamasha hilo la siku tatu litakaloongozwa na mada kuu ‘Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange’ linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule.
Amesema Tamasha la 7 la Jinsia ngazi ya Wilaya limeandaliwa na TGNP kwa kushirikiana na mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa jinsia nchini wakiwemo WFT, CAMFED, WAJIBU, Chuo cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa, Policy Forum, PELUM Tanzania, na Msichana Initiative, Vituo vya Taarifa na Maarifa kutoka Mtwara Vijijini, Lindi, Same, Mwanga, Babati, Morogoro Vijijini, Gairo, Kinondoni, Ilala, Ubungo, Kondoa Vijijini na Kishapu.
Liundi ameeleza kuwa, wameandaa tamasha hilo kwa ufadhili wa wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Uswidi, CrossRoads International UN Women, Coady international, Ubalozi wa Ireland, Global Affairs Canada kupitia Seedchange na Aga Khan Foundation.
“Tamasha hili litahusisha mbinu mbalimbali za uwasilishaji maudhui zitakazochagiza, kuhamasisha na kutoa nafasi kwa washiriki kuwa pamoja katika kubadilishana ujuzi, uzoefu na kujengeana uwezo. Miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na Mawasilisho na Majadiliano ya pamoja sanaa/burudani zinazofunza, warsha, visa mkasa na maonesho ya kazi na bidhaa mbalimbali zitokanazo na harakati za ukombozi wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia katika jamii na taifa kwa ujumla”,ameeleza.
“Mijadala ya pamoja itajenga dhana halisi kuhusu mada ndogo katika siku husika. Siku ya mwisho itahusisha kufunga kwa kuyaweka pamoja masuala yaliyoibuka katika mijadala mbalimbali siku zote tatu za Tamasha. Kwa kuzingatia masuala yaliyoibuliwa, washiriki watatengeneza mipango mkakati kwa ajili ya utekelezaji”, ameongeza Liundi.
Hali kadhalika kutafanyika Maonesho katika siku zote za Tamasha kutoa nafasi kwa mashirika na mitandao inayoshiriki kuonesha kazi zao kupitia njia mbalimbali kama vile video, mabango, picha ambapo Wachapishaji, AZAKI na wanawake binafsi pia wanakaribishwa kuonesha na kuuza bidhaa zao na kwamba sehemu maalumu zitatolewa kwa vikundi maalum kutengeneza vitovu vya mtandao, kupeana taarifa na kupanga mikakati ya pamoja.
Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024 litaongozwa na mada kuu isemayo ‘Dira Jumuishi ya 2050: Miaka 30 Baada ya Beijing Tujipange’ huku mada ndogo ndogo zikiwa ni pamoja na Miaka 30 baada ya Beijing: Viongozi wanawake wako wapi? Mada hii itajikita kuangazia namna yakuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi hasa kwenye nafazi za viongozi wa serikali za mitaa kuelekea uchaguzi wa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025 wa Madiwani, Wabunge na Rais. Tafakuri hii itaenda sambamba na uwasilishaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake ngazi ya kata.
"Tunatambua kuwa kwa sasa nchi yetu ina Rais Mwanamke kwa mara ya kwanza kabisa; kwa upande wa wabunge wanawake ni asilimia 37 tu ambao 9.5% ni wabunge wa kuchaguliwa na 29% ni wa vitimaalumu. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ni miongozi mwa wanawake wakuu mikoa wachache nchini na pia, mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Fatma Nyangasa ni miongoni mwa wakuu wa wilaya wanawake wachache nchini", amesema Liundi.
"Aidha, kati ya nafasi 11,915 za wenyeviti wa vijiji, wanawake walipata nafasi 246 pekee, ambayo ni asilimia 2.1 ya wenyeviti wote, huku wanaume wakipata asilimia 97.9. Kati ya nafasi 4,171 za wenyeviti wa kata, wanawake walishinda nafasi 528, ambayo ni asilimia 12.6 ya wenyeviti wote, huku wanaume wakipata 87.4%. Pia, nafasi za uenyekiti wa vitongoji 62,612, wanawake walishinda nafasi 4,171, ambayo ni asilimia 6.7 ya wenyeviti wote wa vitongoji, kwa mujibu wa Ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 2019. Bado idadi ya uwakilishi wa wanawake katika ngazi za maamuzi ni ndogo, hivyo, jitihada zinatakiwa kuendelea kufanyika ili kuongeza uwakilishi huu na kufikia 50/50",amefafanua.
Ameitaja mada nyingine kuwa ni, Harakati za Kijamii na ushiriki wa makundi rika. Mada hii itaangazia na kuchakata ushiriki wa makundi rika katika harakati za kushiriki maendeleo na namna gani makundi haya yanarithishana mbinu, nyenzo na mikakati bora katika kutengeneza Tanzania yenye maendeleo ya watu na vitu sawa sawa na azma ya Dira ya 2025 na inayoandaliwa ya 2050.
Pia kuna mada ya Teknolojia na Mabadiliko ya Tabianchi ambapo Mada hii itaangazia na kujadili kwa namna gani mabadiliko ya tabia ya nchi yameathiri maendeleo na mipango, mikakati gani imewekwa kuendana na mabadiliko ya Teknolojia ikishirikisha watu kwa pamoja na kusaidia kupiga hatua katika jamii pamoja sambamba na kuweka mikakati juu ya matumizi ya nishati safi na kuhamasisha Serikali kuweka bei elekezi ili kuwawezesha wananchi walipo vijijini na wengi kutumia nishati zafi. Mada hii pia itaangazia umuhimu wa Teknolojia katika kufikia usawa wa kijinsia kulingana na mabadiliko na ukuaji wa Teknolojia duniani. Takwimu zinaonesha kuwa wanawake viongozi katika teknolojia ni asilimia 27.
Aidha mada nyingine ni Ziko wapi kazi zenye ujira na staha kwa wanawake na vijana?. Mada hii itajikita kuangalia changamoto kubwa zinazoletwa na mzigo wa kazi za huduma zisizo za staha na ujira kwa wanawake na vijana. Mwisho mada hii itaangazia kuunda njia mahususi kuepukana na aza hizo kuanzia ngazi ya familia mpaka ya jamii nzima. Kutokana sera ya Jinsia ya 2023, wanawake wanaofanya katika sekta zisizo rasmi ni asilimia 51. Kulingana na takwimu za UN Women, wanawake wanatumia masaa 4.4 kwa siku kwenye kazi zisizo na ujira na kazi za nyumbani ukilinganisha na lisaa 1.4 kwa wanaume.
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Elizabeth Shoo akizungumza wakati Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Lilian Liundi akitoa tamko kuhusu Tamasha la 7 la Jinsia Ngazi ya Wilaya 2024
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Elizabeth Shoo ameipongeza TGNP na wadau mbalimbali wanaoshirikiana na serikali kuongeza uchechemuzi katika kupigania usawa wa kijinsia huku akibainisha kuwa Tamasha hilo litakuwa chachu kubwa ya maendeleo hivyo kuwaomba wanaharakati, wadau na wananchi kushiriki katika tamasha hilo.
KUHUSU TAMASHA LA JINSIA
Tamasha la Jinsia ni moja ya majukwaa ya TGNP katika ujenzi wa nguvu za Pamoja. Jukwaa hili ni la wazi kwa ajili ya wanawake na wadau wa haki za binadamu ambao hukutana pamoja kila baada ya mwaka mmoja kubadilishana uzoefu, kusherehekea, kutathmini na kupanga mipango ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
TGNP iliratibu tamasha la kwanza kabisa mwaka 1996 na hadi sasa takribani matamasha 15 yamekwishafanyika ambapo yameweza kuleta pamoja zaidi ya washiriki 27,000 (70% wanawake na 30% wanaume) katika viwanja vya TGNP.
Kutokana na mafanikio ya Tamasha kubwa la Jinsia, mwaka 2010, TGNP na washirika wake walizindua Tamasha la Kwanza la Jinsia Ngazi ya Wilaya lilizinduliwa mwaka 2010 na tangu wakati huo MaTamasha ya Jinsia yaliyoandaliwa wilayani yamefikia matano na Tamasha moja lilifanyika ngazi ya Kanda na kuleta pamoja zaidi ya washiriki zaidi ya 60,000 tangu kuanzishwa kwake.
Tamasha la kwanza la Jinsia kiwilaya lilifanyika Kisarawe (2010) na kufuatiwa na la kata ya Mkambarani-Morogoro mwaka 2011 na 2016. Wilaya ya Tarime kata ya Nyamaranda (2014), Mkoa wa Shinyanga Wilaya ya Kishapu kata ya Maganzo (2018), na Mkoa wa Mbeya kata ya Ijombe (2020). Na Tamasha la kwanza la Jinsia la Kanda lilifanyika Same - Kilimanjaro mwaka 2022.
Ikiwa ni sehemu ya kupanua vuguvugu la mabadiliko ya wanawake nchini na kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki, kumekuwa na haja ya kuandaa Tamasha la Jinsia la Ngazi ya Wilaya litakalokutanisha wadau mbalimbali kutoka kanda mbalimbali nchini.
TGNP ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 1993, TGNP inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza mashirikiano ya asasi za kiraia kwa kujenga uwezo wa kuchanganua na kuibua mijadala ya umma na hivyo kuleta mapinduzi ya kijinsia na hatua za pamoja kwenye masuala muhimu ya maendeleo kijamii, kitamaduni, kisiasa na kiuchumi.
No comments