Breaking News

TAKUKURU MWANZA YAWEZESHA KUKUSANYWA KWA ZAIDI YA MILIONI 290

 Na Tonny Alphonce, Mwanza

Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mwanza imewezesha kukusanywa kwa zaidi ya Shilingi Milioni 290 kutoka katika halmashauri za Mkoa wa Mwanza kupitia mfumo wa ukataji na uwasilishwaji wa kodi ya zuio.

Kukusanywa kwa fedha hizo kumetokana na maazimio yaliyowekwa kati aya TAKUKURU,Halmashauri za Mkoa wa Mwanza na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza James Ruge amesema baada ya kudhibiti mapungufu mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa kodi na utoaji risiti za EFD Shs.290,744,721.65 zimeweza kukusanywa na kuwasilishwa TRA ikiwa ni makusanyo ya kodi ya zuio.

Akizungumzia uchunguzi na mashitaka yaliyofanywa na TAKUKURU,Ruge amesema malalamiko 64 yamepokelewa  na kati ya hayo malalamiko 43 yalihusu rushwa huku malalamiko 21 yakiwa hayahusiana na Rushwa.

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza James Ruge akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita mbele ya waandishi wa habari wa mkoa wa Mwanza

Amesema katika kipindi hiki cha miezi mitatu ya utendaji  vibali 26 vimetolewa na ofisi ya taifa ya mashitaka ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.

Akizungumzia mikakati iliyojiwekea TAKUKURU katika  robo ya kwanza kwa mwaka huu wa 2024/2025 ,Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza James Ruge amesema kipaumbele cha kwanza ni kuzui vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali.

'Ili tupate matokeo ya haraka tutafatilia vitendo vyote vya rushwa kabla ya uchaguzi,wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi na wahusika endapo watabainika watachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.'amesema Ruge

Aidha Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza James Ruge amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU katika kuzui vitendo vya rushwa kwenye maeneo yote ya huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na katika kuelekea uchaguzi wa Serikali Za Mitaa.

No comments