Breaking News

JITIHADA ZA HALMASHAURI YA ILEMELA KUMALIZA UTAPIAMLO ZAANZA KUZAA MATUNDA

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Halmashauri ya Ilemela, mkoani Mwanza, imeanza kuona matokeo chanya kutokana na juhudi zake za kupambana na tatizo la utapiamlo, ambapo zaidi ya watoto 100 wamepatiwa matibabu. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ilemela, Ummy Wayau, alisema kuwa mafanikio haya yanatokana na jitihada za halmashauri kutoa huduma muhimu kwa watoto ambapo mwaka jana halmashauri ya Wilaya ya Ilemela ilianzisha mpango wa kutoa huduma za lishe shuleni, ambapo jumla ya shule 52 kati ya 76 za serikali zilianza kutoa lishe kwa wanafunzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Ilemela  Ummy Wayau 

Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Msingi na Awali, Mwamu Busungu, alieleza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa hadi Mei 2024 shule zote zitakuwa zinatoa lishe bora kwa wanafunzi wa madarasa ya awali hadi darasa la saba.

Takwimu zinaoenyesha hadi sasa  watoto 66,711 wamepatiwa matone ya vitamini A, huku watoto 128 waliokuwa na Utapiamlo wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Buzuruga.Watoto hao sasa wamepona, jambo ambalo linathibitisha mafanikio ya jitihada hizo.

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa kwa watoto 30,385, watoto 30,098 walikuwa na hali nzuri ya lishe, huku asilimia 0.9 walibainika kuwa na dalili za utapiamlo. Watoto watatu tu walikuwa na utapiamlo mkali, idadi ambayo halmashauri imepania kuipunguza hadi ifikie sifuri.

Takwimu za mkoa wa Mwanza kupitia taarifa ya Lishe ya Watoto Mkoa  (2018) zinaonyesha kuwa hali ya udumavu bado ni changamoto kubwa, ambapo takribani asilimia 34 ya watoto wa mkoa huo wanakabiliwa na udumavu, na asilimia 4.7 ya watoto wakiwa na uzito pungufu. 

Asilimia 63 ya watoto wa Mwanza wanapata nyongeza ya matone ya vitamini A, kiwango ambacho kinahitaji kuongezeka zaidi ili kuhakikisha afya bora kwa watoto wote.

Afisa Lishe wa Manispaa ya Ilemela, Bi Pili Kasimu, amesisitiza kuwa pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto za elimu duni kuhusu lishe bora kwa watoto.

 Alibainisha kuwa baadhi ya wazazi hawawapeleki watoto vituoni kupatiwa matone ya vitamini A, na pia hawana uelewa wa mpangilio mzuri wa chakula kwa watoto. Hii inasababisha watoto wengi kupewa aina moja ya chakula, jambo linalopelekea utapiamlo.

"Muhimu sana kwa wazazi kuendelea kujifunza jinsi ya kuchanganya vyakula vilivyopo nyumbani ili watoto wapate virutubisho sahihi kwa ukuaji bora," alisema Bi Pili.

Sophia Asenga, mwakilishi wa Shirika la Dunia Rafiki, aliongeza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wazazi ili kuwahamasisha juu ya umuhimu wa lishe bora na matone ya vitamini A.

Asenga alisema kuwa imani potofu kuhusu chanjo za matone imekuwa kikwazo kikubwa, huku baadhi ya wazazi wakiwaficha watoto wao wakati wa kampeni za chanjo.

Masalu Masanja, mkazi wa Luchelele, Mwanza, ni mmoja wa wazazi waliopata elimu kupitia kampeni hizi.

Awali, watoto wake walikutwa na dalili za utapiamlo licha ya kula chakula cha kawaida kama ugali na wali lakini baada ya kupata elimu, aligundua kuwa chakula alichokuwa anawapa watoto wake kilikuwa hakitoshelezi mahitaji ya virutubisho.

 "Nilianza kuwapa vyakula vya ziada vilivyo na virutubisho na kuona mabadiliko makubwa sana," alisema Masanja.

Mafanikio haya yanatokana pia na ongezeko la vituo vya afya katika halmashauri ya Ilemela, ambavyo sasa vimefikia 65 kati ya hivyo, vituo 24 ni vya serikali, 4 vya mashirika ya umma, 2 vya dini, na 35 vya watu binafsi.

Halmashauri imekuwa ikitekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), ambayo inalenga kuimarisha afya na ukuaji wa watoto.

Kwa juhudi hizi, halmashauri ya Ilemela ina matumaini ya kufikia asilimia 100 ya watoto wenye lishe bora katika miaka michache ijayo.

Hii inaenda sambamba na jitihada za kitaifa kupitia Mpango wa Taifa wa Lishe (2016-2021) wa kupunguza kiwango cha udumavu kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 hadi asilimia 28 ifikapo mwaka 2025.

Serikali pia inalenga kupunguza utapiamlo mkali hadi chini ya asilimia 1 kupitia Mpango huu wa Taifa wa Lishe.


No comments