Breaking News

MRADI “BARRICK-TWIGA FUTURE FORWARD EDUCATION PROGRAM” WALETA MAPINDUZI SEKONDARI ZA SERIKALI NCHINI

    

Wanafunzi wa shule ya sekondari Mtwara wakisoma katika miundo mbinu iliyojengwa kupitia programu hii.
Muonekano wa baadhi ya madarasa na mabweni ya kisasa yaliyojengwa kupitia mradi hii

#Awamu ya kwanza imefanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kisasa 374,mabweni 89 na mashimo ya vyoo 569 nchini kote
**
Mradi mkubwa wa aina yake wa kusongesha mustakabali wa elimu nchini unaotekelezwa kwa ubia kati ya kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania unaojulikana kama ‘Barrick-Twiga Future Forward Education Program’ umeanza kupata mafanikio makubwa katika awamu yake ya kwanza baada ya kukamilika kwa miundombinu ya madarasa ya kisasa, mabweni na vyoo katika shule za sekondari za Serikali katika mikoa mbalimbali nchini.

Programu ya Barrick-Twiga ya kusongesha Mbele Mustakabali wa Elimu (‘Barrick-Twiga Future Forward Education Program’) imelenga kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule za sekondari za serikali za elimu ya juu (Advance level) ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa ambao walikuwa wanakosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na uhaba wa miundombinu sambamba na kuhakikisha wanapata elimu katika mazingira rafiki.
Muonekano wa baadhi ya madarasa na mabweni ya kisasa yaliyojengwa kupitia mradi hii

Wakati wa kutangazwa utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa aina yake fedha mwezi Machi mwaka jana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Dk.Samia suluhu, ilibainishwa kuwa utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 70.5 za fedha za Tanzania ukilenga kujenga madarasa 1,090 ,majengo ya maliwato na vyoo 1,640 na mabweni 270 katika shule 161 nchini kote.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa awamu ya kwanza ya mradi tayari umefanikisha kujengwa vyumba vya madarasa ya kisasa 374,mabweni ya kisasa 89 na matundu ya vyoo 569 na walengwa wameanza kufurahia matunda ya mradi wakati mchakato wa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi ukiendelea.

Akiongea wakati wa kutangaza kutoa fedha za mradi huu katika mkutano wake na Rais Samia, Ikulu Dodoma mwaka jana, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dhahabu ya Barrick, Mark Bristow alisema kuwa Barrick inaamini elimu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na ndio sababu mbali na fedha za mradi huu, migodi yake nchini ya Bulyanhulu na North Mara imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa na kuboresha miundombinu ya elimu ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ufundi katika maeneo yanayoizunguka migodi hiyo, jambo ambalo limefanikisha baadhi ya shule hizo kuwa miongoni mwa shule zinazoongoza mara kwa mara katika mikoa ilipo migodi hiyo.
Muonekano wa madarasa kwa ndani
Wanafunzi wanaonufaika na mradi, na wadau mbalimbali wameulelezea mradi huu kuwa ni wa aina yake nchini kwa kuwa umeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu nchini na utafanikisha kuinua ufaulu sambamba na kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu.

Wanafunzi wanazungumziaje Barrick-Twiga Future Forward Education Program’

“Mradi huu umesaidia kuondoa msongano katika mabweni ,madarasa, na kwenye vyoo,kwa sasa tunasoma katika mazingira mazuri, kwa jinsi mazingira yalivyo sasa naamini ndoto yangu ya muda mrefu ya kuwa Daktari bingwa wa upasuaji itatimia”, alisema Prisca Mawaga anayesoma kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Lucas Malia iliyopo wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Wanafunzi wa shule ya sekondari wakisoma katika miundo mbinu iliyojengwa kupitia programu hii.

Rushda Idd, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mamire iliyopo wilayani Babati, mkoani Manyara, alisema mradi huu ni wa aina yake kwa kuwa umefanikisha kujengwa mabweni,Vyoo na madarasa ya kisasa “Tunasoma katika mazingira rafiki kwakulinganisha na miundombinu iliyokuwepo awali hususani kwetu wasichana ambao tulikuwa tunaugua magonjwa ya kuambukizana kutokana na kutumia vyoo visivyo rafiki na kulala kwa msongamano katika mabweni na kulala wanafunzi zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja”alisema Rushda kwa furaha.

“Mradi huu umewezesha mazingira mazuri na rafiki ya kusoma na kusababisha kuipenda shule na mimi na wenzangu tunaotumia miundombinu hii tunayo furaha na tunaishukuru Barrick na Serikali kwa kutukumbuka na wengi wetu tunasoma kwa bidii kuhakikisha tunaingia vyuo vikuu na ndoto zetu za maisha kutimia”,alisema Gilbert Chiyumbe mwanafunzi wa sekondari ya Ibwaga iliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Simon Bujiku, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Sumve iliyopo mkoani Mwanza alisema kuwa mradi huu utasaidia kuongeza ufaulu na umeongeza thamani ya shule za Serikali “Miundombinu yetu ya mabweni,madarasa na vyoo kupitia mradi huu ni mizuri kiasi kwamba najivunia kusoma shule ya serikali,mbali na viwango pia umejingatia mahitaji wa wanafunzi walemavu ambao wamejengewa miundombinu rafiki ya kuingia madarasani, na vyoo maalumu kwa ajili yao”alisema Bujiku kwa furaha.

Mwajuma Omar mwanafunzi wa sekondari ya wasichana ya Ifunda alisema “Kupitia mradi huu mazingira ya kusoma yamekuwa rafiki maana tuna madarasa,mabweni na vyoo vya kisasa ambavyo ni rahisi kutunza usafi,kwetu wasichana tumekuwa pia na mazingira rafiki ya kujistiri wakati wa vipindi vya hedhi tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali”, alisema Mwajuma kwa furaha.

Wakuu wa shule wanasemaje kuhusu mradi?

Mkuu wa shule ya Wasichana ya Ifunda, Blandina Nkondola anasema “Mradi huu umewezesha wanafunzi na walimu kuwa katika mazingira rafiki ya elimu bora naamini utafanikisha kuleta matokeo makubwa kuanzia sasa mpaka siku za mbele utakapokamilika”
Muonekano wa baadhi ya madarasa na mabweni ya kisasa yaliyojengwa kupitia mradi hii

Maria Kitakala, Kaimu Mkuu wa sekondari ya Sumve alisema “Mradi huu umekuja kwa wakati mwafaka ambao tulikuwa na uhaba wa miundombinu ya madarasa, mabweni vya vyoo, kwa idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa shule hii imeongezeka na tunaweza kuwahudumia vizuri.Nashukuru Barrick kwa kutekeleza mradi huu wa aina yake”.

Eva Mwansililo, Mkuu wa sekondari ya Ibwaga wilayani Kongwa anasema “Mradi huu ni mzuri na umefanikisha watoto kusoma katika mazingira mazuri,umepunguza utoro,mbali na kunufaisha wanafunzi wa vidato vya juu (A-level) pia umenufaisha wanafunzi wa madarasa ya chini wanaotoka kwenye maeneo ya mbali na shule ambao walikuwa wanapitia changamoto mbalimbali wakati wa kuja na kutoka shuleni”.

Fitelly Akyoo ,Mkuu wa sekondari ya Mamire wilayani Babati anasema “Mradi huu umefanikisha wanafunzi wa kike kusoma katika mazingira rafiki zaidi,walimu kufanya kazi kwenye mazingira mazuri pia utaongeza kiwango cha ufaulu kwa kuwa walimu na wanafunzi wote wamefurahi kutokana na miundombinu ya kisasa iliyojengwa hapa shuleni”

Hilda James Paul.Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari ya Lucas Malia iliyopo Ruangwa mkoani Lindi anasema Barrick-Twiga Future Forward Education Program’ italeta matokeo makubwa kwa sasa na miaka ijayo,naipongeza Barrick na Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa elimu nchini.


Wazazi sehemu mbalimbali wanauzungumziaje mradi?

Issa Nkunga mkazi wa kijiji cha Mamire wilayani Babati mkoani Manyara anasema, “Mradi huu umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya upungufu wa mabweni,mashimo ya vyoo na madarasa,sasa watoto wanaosoma katika mazingira mazuri na kwa vyovyote ufaulu utaongezeka vilevile umesaidia kupunguza vitendo vya utoro,watoto wakike kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia pia kuna wanafunzi wa madarasa ya chini ambao walikuwa kutoka vijiji vya mbali ambao walikuwa wanakabiliwa na hatari wa kudhuriwa na wanyama wakali wakati wa kwenda na kutoka shuleni ,sasa wamepatiwa hifadhi katika mabweni mapya yaliyojengwa na mradi”.
Wanafunzi wa shule ya sekondari mkoani wakisoma katika miundo mbinu iliyojengwa kupitia programu hii.

Moses Mpwapwa mkazi wa kijiji cha Mbekenyela wilayani Ruangwa anasema "Mradi huu ni mzuri na umekuwa shirikishi,tangu ulivyoanza katika shule yetu ya Lucas Maliya,wazazi wote tuliambiwa na sasa tunafurahi kuona watoto wetu wanasomea kwenye madarasa na wanaishi kwenye mabweni bora.Tunategemea watoto wetu watafanikisha ndoto zao".

Samwel Luhunga ,mkazi wa kijiji cha Ibwaga wilayani Kongwa alisema,"Barrick imefanya kitu kikubwa kuwekeza katika elimu nchini,uwekezaji huu utanufaisha vizazi na vizazi,pamoja na kuboreshewa miundombinu bado zipo changamoto nyingine,naomba taasisi nyingine pia zijitose katika uwekezaji katika sekta ya elimu".

Oddo Asanterabi, mkazi wa Geita anasema “Uboreshaji wa miundombinu kupitia mradi huu wa Barrick tunaamini utawezesha watoto wetu kufanikisha ndoto zao pia umeondoka changamoto za mara kwa mara tulizokuwa tunapata wazazi hususani watoto kuugua mara kwa mara kutokana na kutumia miundo mbinu isiyoendana na idadi yao ,sasa tunafurahi watoto wanasoma katika mazingira rafiki na wana furaha”.

Viongozi wa elimu na wadau katika maeneo ya mradi

Ashura Mpambije, Kaimu Afisa Elimu Sekondari wilayani Ruangwa mkoani Lindi anasema “Mradi umekuja kwa wakati mwafaka ambapo idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kusoma vidato cha juu imeongezeka,umesaidia kuboresha mazingira ya kusomea na naamini wanafunzi wengi watafaulu na kuendelea vyuo vikuu kutokana na kusomea katika mazingira rafiki”.

Dk. Jamaa Mhina, Mkurugenzi wa Manispaa ya wilaya ya Muheza anasema “Naipongeza na kuishukuru Barrick na Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi huu mkubwa wa kuboresha elimu nchini kote maana wengine huku hakuna migodi yao lakini mradi mzuri kama huu umetufikia na utaleta manufaa kwa watoto wanaosoma katika shule ambayo mradi utekelezwa”

Aliche Mwalo, Afisa Elimu Sekondari wilayani Babati anasema, Mradi huu umefanya mazingira ya shule kuwa rafiki kwa wanafunzi na walimu,naamini utaongeza ufaulu wa wanafunzi na sisi wasimamizi wa elimu umetusaidia katika usimamizi na kufanikisha mipango ya ukuzaji taaluma”

Serapion Bashange, Afisa elimu Sekondari wilaya ya Muheza , alisema,Mradi umekuja kwa wakati mwafaka na utasaidia kupunguza changamoto za wanafunzi kusomea katika mazingira yasiyo rafiki,umeleta motisha kwa wanafunzi kusoma na walimu kufundisha katika shule ambazo umetekelezwa”.

Mkuu wa wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba alisema ,"Mradi huu ambao umetekelezwa katika wilaya hii umesaidia kuongeza idadi ya wanafnzi wanaopata fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari ya juu pia umepunguza changamoto ya uhaba wa madarasa,mabweni na matundu ya vyoo.Nawapongeza Barrick kwa kushirikiana na Serikali kwa kusambaza mradi huu nchi nzima",

Elizabeth Renjima, Diwani wa kata ya Ugogoni wilayani Kongwa anasema “Mradi umeleta mwamko mkubwa wa watoto wetu kusoma na kuacha utoro kutokana na miundombinu yake kuwa na viwango vya kimataifa”.
Muonekano wa baadhi ya madarasa na mabweni ya kisasa yaliyojengwa kupitia mradi hii

Utekelezaji za Malengo ya milenia SDG 4/SDG 17

Kwa utekelezaji wa mradi huu, Barrick imefanikisha malengo ya milenia SDG 4 lengo linalohusiana na kufanikisha upatikanji wa elimu bora (Quality Education) na lengo SDG 17 linalohusu ushirikiano wenye kufanikisha mafanikio (Partnership for Goals).

Takwimu za TAMISEMI Ongezeko la Wanafunzi shule za sekondari za juu

Akitangaza idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya kati mwaka huu wa 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mh.Mohamed Mchengerwa alisema idadi ya wanafunzi 188,787 na kati yao wanafunzi 123,948 wamepangiwa katika shule za sekondari za bweni za kitaifa za kidato cha tano.

Mchengerwa, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh.Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuhakikisha miundombinu ya Elimu inapatikana ambayo imewezesha w wanafunzi wote waliokuwa na sifa kuchaguliwa kidato cha tano na vyuo.

No comments