WAZAZI, WALIMU NA WANAFUNZI WAPEWA ELIMU YA KUTENGENEZA ZANA ZA KUJIFUNZIA WATOTO WA MADARASA YA AWALI
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Zana za
kujifunzia na kufundishia huwakilisha vifaa vyote ambavyo mwalimu hutayarisha
na kutumia wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ili zimrahisishie
ufundishaji wake na kuwafanya wanafunzi waelewe somo kirahisi zaidi.
Pamoja na
faida hizo kumekuwa na tatizo la wazazi kushiriki katika kutengeneza zana hizo za kujifunzia watoto
ambapo baadhi ya wazazi hukwepa wakidhani ni gharama kubwa kuandaa zana hizi
ambazo kiuhalisia hutengenezwa na malighafi zilizopo katika mazingira yao
yanayowazunguka.
Kwa kuliona
hilo Shirika la Tanzania Eary Childhood Education and Care -TECEC kwa kushirikiana
na walimu wa madarasa ya awali katika shule ya msingi ya Luchelele pamoja na wazazi wameunda zana na vifaa vya kujifunzia na kuchezea kwa
watoto wa darasa la awali kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira ya
shule.
Mkurugenzi wa
TECEC Joel Elphas anasema wao kama shirika wanajua umuhimu watoto kujifunza na kucheza na kupitia zana mbalimbali
za kujifunzia kutaweza kukuza ujuzi wao wa kijamii, kiakili, kimwili na
kihisia.
Joel amesema
kupitia vifaa hivyo vya ubunifu vinatoa uhakika kwa watoto kupata fursa ya
kujifunza kwa njia ya vitendo na kujifurahisha, wakati pia wakichunguza
mazingira yao ya karibu.
“Mwanzoni ilikuwa
ngumu kuwapata wazazi ili nao washiriki katika utengenezaji wa zana hizi lakini
baada ya kuwaelimisha tumepata ushirikiano mkubwa na tumefikia lengo kama
taasisi kutengeneza zana nyingi ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwa vijana”.alisema
Joel
Amesema wanajivunia
kuwa sehemu ya juhudi hizo za kipekee kwa kuwa zimewezesha upatikanaji wa elimu
bora na fursa za kujifunza kwa watoto na
amewashukuru walimu wa madarasa ya
awali, wazazi na walezi kwa mchango wao mkubwa na ushirikiano wao katika
kufanikisha mradi huo wa kutengeneza zana za kujifunzia.
Joel amewataka
wazazi kujenga utamaduni wa kutengeneza zana za kujifunzia wao pamoja watoto
wao kwa kuwa malighafi zote zinapatikana katika mazingira waliyopo na kama
watahitaji msaada wa kiufundi wanaweza kuwasiliana na shirika la TECEC kwa
msaada zaidi.
Ester
Macha ambaye ni mtaalamu wa elimu ya
awali kutoka TECEC amesema kuwa katika kutekeleza zoezi hilo wazazi na wanafunzi walishirikishwa ili kutoa mawazo
yao na michango yao ya ubunifu na kwa pamoja wakafanikiwa kutengeneza zana za
kujifunza ambazo zilikuwa rahisi kwa watoto kuelewa na kufurahia ujifunzaji shuleni.
“Tulibaini
kwamba vifaa kama vile chupa za plastiki, maboksi,Sponji na vitu vingine vya
kawaida vinaweza kutumiwa kutengeneza zana hizi za kuchezea na kujifunza zikiwa
zinahitaji ubunifu bila gharama kubwa kwa kuwa
rasilimali zote zipo kinachohitajika ni kutengeneza tu vifaa hivyo”.alisema
Ester
Mwalimu
Zawadi Kokutangilila amelishukuru shirika la TECEC kwa kuwapa ujuzi wa namna ya
kutengeneza zana za kufundishia kwa watoto wa madarasa ya awali na kuwaomba
wazazi ambao wamepewa ujuzi kuwa mabalozi wazuri kwa wazazi wengine ili nao
wapate ujuzi huo.
Nae mzazi Joel
Mafuru na Agness Masanja walioshiriki katika
zoezi hilo wamesema mwanzoni hakuwakujua
kama zana hizo ni muhimu katika ujifunzaji wa mtoto lakini wameshuhudia jinsi
watoto walivyochangamka na kupata furaha wanapojifunza kupitia zana hizo.
“Kwa sasa
ninao uwezo wa kutengeneza zana hizi na kuanzia leo takuwa namtengenezea
mwanangu ili ziweze kumsaidia katika safari yake hii ya masomo ya darasa la
awali”.alisema Mafuru
Kanuni za
vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na watoto wachanga ya mwaka 2012 inahusisha
mchakato wa uandaaji wa kiongozi cha
utengenezaji wa vifaa vya michezo na kujifunzia watoto chini ya miaka 5.
Vilevile,
uelewa juu ya umuhimu wa ujifunzaji kupitia michezo haukupewa kipaumbele katika
ngazi zote za maamuzi, udhibiti ubora, watoa huduma, waelimishaji na jamii kwa ujumla
ikiwemo wazazi.
Ukosefu wa
vifaa vya kuchezea watoto, vitabu, uelewa na ujuzi kuhusu malezi na wazazi kutokuchangamana
na watoto mara kwa mara nayo imeripotiwa kama changamoto.
No comments