WANANCHI BUKOMBE WATAKA ELIMU YA MMMAM IFIKE HADI VIJIJINI
Salum Maige,Geita
Baadhi ya wananchi wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameomba serikali na wadau kuhakikisha wanafikisha elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya vijiji.
Wamesema hatua hiyo itasaidia wananchi wengi kuzingatia malezi bora kwa watoto na kuepukana na vitendo vya kikatili vinavyoathiri ukuaji wa watoto.
Pendo Pius mkazi wa Kijiji cha Namonge wilaya ya Bukombe anasema wananchi walio wengi wamekuwa kikwazo kwa ukuaji timilifu kwa watoto kutokana na kufanyia ukatili na kuwatumikisha kazi zilizo nje ya uwezo wao.
“Wazazi wengi hatujui hayo,tunaweza kusingizia watoto wetu ni wajinga kumbe tumewadumaza sisi wenyewe kwa kushindwa kufuata misingi mizuri ya malezi tangu mimba inapotungwa,hii elimu ikimfikia mmoja naamini kabisa taifa litakuwa na wasomi wengi”anasema Pendo.
Katika mahojiano na Masanja Makendi ambaye ni mkazi wa Ushirombo wilayani humo anashauri serikali na wadau wasikomee maeneo ya mjini pekee ilihali baadhi ya watoto walioko maeneo ya vijijini na kumbana na mikasa ya ukatili.
“Watotot wanafanyishwa kazi nje ya uwezo wao,wanachunga mifugo,wanalea watoto wenzao,wazazi wanaachia nyumba,toka asubuhi hadi mchana,hawana muda wa kupumzika,hivyo elimu hii ni muhimu sana maeneo ya vijijini”anasema Makendi.
Aidha,kwa mujibu wa Programu jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) ni kwamba nchini Tanzania asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na viashiria mbalimbali vya hatari.
Viashiria hivyo ni pamoja na utapiamlo,umasikini,kukosekana kwa uhakika wa chakula,msongo wa mawazo ya kifamilia,miundombinu duni,uhaba wa rasilimali pamoja na kutelekezwa na unyanyasaji wa watoto.
Ili kushughulikia changamoto hizo baadhi ya wadau yakiwemo mashirika binafsi,waandishi wa habari kwa kushirikiana na serikali wameanza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kutoa elimu kwa watumishi wa serikali wakiwemo maafisa lishe,ustawi wa jamii,wamiliki wa vituo vya malezi ya watoto,na viongozi wa dini.
Mkoani Geita tayari serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la NELICO linalotekeleza mradi wa Mtoto kwanza mkoani hapa ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha watoto wa mwaka 0 – 8 wanafikia ukuaji timilifu imeanza kutoa elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa halmashauri zote sita.
Akizindua program hiyo mkuu wa wilaya ya Bukombe Said Nkumba,aliyewakilishwa na katibu tawala wa wilaya hiyo Onesmo Kisoka amesema kuanza kwa mpango huo wa serikali wilayani kwake ni jambo muhimu sana katika jamii ya Tanzania ukiwemo uchumi wa nchi.
“Katika umri wa 0-8 ni wakati mzuri sana katika kusimamia malezi ya mtoto,tunataka watoto wasome lakini hawawezi kusoma vizuri endapo hawana makuzi na malezi mazuri,hakutakuwa na maana ya serikali kujenga vyumba vya madarasa ili watoto wasome katika hatutawekeza kwene malezi na makuzi”anasema Kisoka.
Anasema,katika kutekeleza mpango huo wa Rais ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bukombe itahakikisha inatekeleza kwa kusimamia vizuri program hiyo ili kufikia lengo la Mh.Rais la kujali mazingira mazuri ya makuzi ya watoto.
Naye mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe,Dkt Kaji Mahona ,halmashauri hiyo iko tayari kuhakikisha mpango huo wa serikali inafika kwa jamii ili kuwa taifa lenye watu bora.
“Sisi kama halmshauri tutatenga bajeti kwa ya kuhakikisha elimu hii inafikia jamii nzima kwa kushirikiana na watumishi wa Afya,ustawi wa jamii,maendeleo ya jamii,lishe na dawati la jinsia ili tu kuhakikisha mtoto anafikia ukuaji timilifu”anasema Dkt.Mahona.
Awali akitambulisha program hiyo,Afisa ustawi wa Jamii mkoa wa Geita ,Frank Moshi amesema serikali imekuja na mpango huo baada ya kuona kuna changamoto zinazowakabili watoto kufikia hatua ya ukuaji timilifu.
Akizungumzia katika suala la elimu ya awali kwa mtoto,Moshi amesema ,inatakiwa kuwekeza katika madarasa yanayoongea kwa ajili ya ujifunzaji wa awali wa mtoto ili kumjenga mtoto katika ufahamu wa ndani ya ubongo wake.
Anafafanua kuwa,madarasa hayo yanapaswa kuwa na zana kujifunzia zikiwemo picha mbalimbali za wanyama,na vitu vingine vinavyopatikana kwenye mazingira yetu .
“Mtoto wa miaka mitatu na minne hatikiwa kuandika chochote isipokuwa anapaswa kujifunza kwa kutambua vitu kwa picha na sanaa zitazokuwa darasani kabla ya kuanza darasa la awali anapofikisha miaka mitano”anasema Moshi.
Kadhalika,aliwataka washirikia hao wanapoenda katika maeneo yao ya kazi wakatoe elimu kwa jamii kwamba ijitahidi kujizuia kutamka maneno yasiyofaa mbele ya watoto wadogo ambao umri huo wa 0-8 ubongo wao unashika vitu vingi.
Aidha,amewataka viongozi hao wa halmashauri pamoja na wadau kutambua kwamba mpango huo wa taifa unajumuisha utambuzi wa mapema watoto wenye ulemavu.
Hatua hiyo ambayo amesema, itahusisha wazazi,walezi,walimu na watalaamu wa afya ili kusaidia kupunguza makali ya ulemavi,kuwezesha kupata takwimu sahihi kwa ajili ya mipango ya utoaji huduma.
Kwa upande wake,mratibu wa mradi wa Mtoto Kwanza mkoani kutoka shirika la NELICO Sophia Njete mradi huo unakusudia kuwafikia wadau wa mtoto wakiwemo watumishi wa serikali,wamiliki wa vituo vya kulea watoto,viongozi dini,wanasiasa ili kuwapa elimu ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Njete amesema kipindi cha miaka 0-8 ni kipindi ambacho mtoto anatengeneza ubongo wake kwa kujifunza vitu mbalimbali kwa kutaja,kutamka,na kujifunza kila kitu kinachomzunguka.
Ameongeza kuwa ubongo wa mtoto hukua kwa asilimia 90 akiwa katika umri wa miaka sita ,ambapo mzazi au mlezi akishindwa kumlea moto akiwa katika umri huo wa miaka 0-8 hapo ndiyo madhara hutokea.
Amewataka wadau wa mtoto,viongozi wa serikali,wazazi na walezi kuhakikisha wanajikida kuondoa vihatarishiri vinavyosababisha mtoto kutofikia ukuaji timilifu vikiwemo lishe duni,umasikini,ukatili,msongo wa mawazo,utapiamlo na kukosa malezi yenye mwitikio.
“Baadhi ya wazazi wanapenda sana mtoto anapoanza tu darasa la awali baada ya siku chache ajue kusoma na kuandika,wapeni elimu wazazi kwamba umri wa miaka 2 hadi mine mtoto hatakiwi kujua kuandika mtoto anauwezo wa kujifunza kwa kuona,kushika na ukajikuta anajua hata kuhesabu 1-10 lakini hajui kuziandika”anasema Njete.
Takribani theluthi mbili sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano walio nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na kukosa malezi bora,umasikini,utapiamlo,
No comments