Breaking News

WAJAWAZITO ,WATOTO WATAABIKA KWA KUKOSA HUDUMA YA AFYA KARIBU

 Salum Maige,Geita

Wakazi wa mtaa wa Mwilima kata ya Kanyala halmashauri ya mji wa Geita wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa zahanati unaoendelea.

Picha kwa hisani ya BMG

Mtaa wa huo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 una wakazi 1,734 kati yao watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni 271 wakiume 116 na wa kike 155.

Kukosekana kwa huduma ya Afya karibu kwa wananchi hao inaweka kwenye wakati mgumu  hasa akina mama wajawazito wanapohitaji huduma ya kujifungua na wakati wa kupeleka watoto wao kliniki.

Wanasema kukosekana kwa huduma ya Afya katika mtaa huo hulazimika kwenda kupata huduma hiyo mbali na makazi yao katika kituo cha afya cha Kasamwa umbali wa kilomita zaidi ya tano.


                  Zahanati ya Mwilima ambayo bado ujenzi wake unaendelea.

Sekelwa Faustine mkazi wa mtaa huo anasema ili kufikia huduma ya afya kwenye kituo cha afya Kasamwa hutumia usafiri wa baiskeli na pikipiki na wakati mwingine hutembea kwa mguu.

“Tunashukuru sana serikali kwa mradi huu lakini bado haujakamilika,kwa sasa tunapata shida kwani nyakati za usiku inapotokea mgonjwa ana hali mbaya au mama mjamzito na mtoto wanahitaji tiba tunahabgaika sana”anasema Anna Joseph.

Naye Mpiga Lushosha mkazi wa mtaa huo anasema huduma ya afya kuwa karibu husaidia sana watoto na akina mama wanapopata changamoto ya afya hasa usiku.

“Tunahangaika hasa usiku tunapopata mgonjwa ,na hasa wajawazito kwenda Kasamwa kuna umbali sana,kakini mimi niipongeze serikali kwa kutuletea huu mradi ,sasa ukikamilika utakuwa umetukomboa sehemu kubwa sana”anasema Kushosha.

Kwa mujibu wa afisa mtendaji wa mtaa wa Mwilima Salome Debwe ni kwamba ujenzi wa mradi huo ulianza machi mwaka jana baada ya kupokea fedha za awamu ya kwanza kiasi cha shilingi milioni 50 kutoka serikali kuu.

Anasema mradi huo ukikamilika utagharimu shilingi milioni 140 fedha kutoka serikali kuu,halmashauri ya mji wa Geita na na nguvu za wananchi.

Zahanati ya Mwilima ambayo bado ujenzi wake unaendelea.

Hata hivyo pamoja juhudi hizo za wananchi na serikali, mtendaji anasema licha mradi huo kuelekea hatua
  ya ukamilika bado kunachangsmoto ya choo, kichomea taka,shimo la majivu pamoja na nyumba ya watumishi.

Diwani wa kata ya Kanyala Enock Mapande anasema mradi huo unatarajia kukamilika ndani ya mwezi huu na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ambao kwa sasa wanahangaika kwenda kituo cha afya Kasamwa ambako ni mbali.

Anasema tayari halmashauri ya mji wa Geita imetenga kiasi cha shilingi milioni 20 kwa ajili wa ujenzi wa choo na kicheo taka na ujenzi wa maeneo hayo utaanza februari mwaka huu ili zile huduma ndogo za kliniki kwa akina mama wajawazito na watoto zianze kutolewa.

Kaimu mratibu wa huduma ya mama na mtoto halmashauri ya mji wa Geita Rehema Kitonga anasema mama mjamzito anatakiwa kuonana na mtoa huduma mara nane katika kipindi cha ujauzito tofauti na zamani ambapo ilikuwa ni mara tatu.

Hivyo,anasema umbali mrefu wa kufika kwenye huduma ya Afya inaweza kusababisha mama mjamzito kushindwa kutimiza masharti ya watalaalamu wa afa kuonana na mhudumu wa afya mara nane katika kipindi cha ujauzito.

“Umbali mrefu wa kufika kwenye vituo vya afya ni moja ya changamoto zinazowasababisha wajawazito kuanza kliniki kwa kuchelewa,hali hii husababisha pia vifo vya watoto wachanga,na wajawazito kwa kukosa huduma mapema”anasema Kitonga.

Moja ya vikwazo vinasababisha watoto kutofikia hatua za ukuaji timilifu ni kukosa huduma bora ya afya tangu mimba inapotungwa hadi kuzaliwa hasa kwenye kipindi cha kuanzia mwaka 0 hadi 8 umri ambao mtoto anahitaji huduma bora ya afya.

No comments