SABABU ZA WAZAZI KUKWEPA KUWAPELEKA WATOTO KLINIKI ZABAINIKA
Na Tonny Alphonce,
Mwanza
Imebainika
kuwa wazazi wengi wenye watoto wenye
umri wa miaka 2 – 3 huacha kuendelea kuwapeleka watoto wao Kliniki na
kuwasababishia magonjwa mbalimbali yanayoweza kuathiri ukuaji wao.
Baadhi ya
wazazi wametaja sababu hizo kuwa ni kukosekana kwa huduma za afya katika maeneo
wanayoishi,kutopata elimu juu ya umuhimu wa kumpeleka mtoto Kliniki pamoja na
wazazi kutumia muda mwingi katika shughuli za kiuchumi.
Mariam Tandu
mkazi wa kata ya Luchelele mtaa wa Ngaza mkoani Mwanza anasema sababu kubwa
iliyomfanya kuacha kumpeleka mtoto wake Kliniki tangu alipokuwa na umri wa
miaka 2 ni kutokana na umbali uliopo kutoka eneo analoishi hadi kwenye Zahanati
ya Shadi.
“Kusema kweli
mimi niacha kumpeleka Kliniki kwa sababu ni mbali ni kama kilometa 6 sasa
nilimwangalia mtoto nikaona anaendelea vizuri haumwi nikaacha hadi leo ndio
kaanza kupata huduma ya chanjo baada ya wataalamu hawa wa afya kuja kwenye
kituo chetu hiki cha kulelea watoto,tunalishukuru sana hili shirika la Dunia
Rafiki wanawasaidia sana watoto wetu hapa Ngaza”.alisema Mariam.
Nae Joseph
Elisha mkazi wa mtaa wa Ngaza amesema kuwepo kwa kituo hicho cha malezi katika
mtaa wao ni neema kubwa kwa kuwa watoto wanalelewa katika mazingira salama
lakini wanapata nafasi nzuri ya kupata huduma za afya pamoja na ufatiliwaji wa
ukuaji mtoto.
Mkurugenzi
wa Kituo hicho cha Kijamii Cha Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Sophia Asenga amesema wameamua
kushirikiana na Zahanati ya Shadi kutoa huduma ya dawa za Minyoo,Matone ya
Vitamin A na Upimaji uzito kwa watoto baada ya kugundua watoto wengi waliopo
mtaa wa Ngaza hawapati huduma ya Kliniki.
Sophia amesema
wameendesha huduma hiyo ya upimaji kwa watoto zaidi ya 30 waliopo katika kituo
hicho na wengine wan je ya kituo hicho kwasababu ni muhimu katika ukuaji wao lakini inasaidia kujua pia maendeleo ya
ukuaji wa mtoto na endapo atapata tatizo lolote ni wazi kuwa wahuduma wa afya
watagundua mapema na kumaptia matibabu sahihi.
“Mtaalamu wetu
wa afya kupitia zoezi hili la leo ameona
afya za watoto wetu hapa mtaani Ngaza
na wengine amegundua baadhi ya watoto wanachangamoto ya ugonjwa wa ngozi
na tayari tumewapa taarifa wazazi ili wawapeleke hospitali kupatiwa tiba”.alisema
Sophia.
Akizungumzia
shughuli zinazofanywa na kituo hicho Sophia amesema mbali na huduma hizo za
afya,kituo hicho kinatoa huduma za uchangamshi,elimu ya awali,malezi yenye
mwitikio kwa kuwashirikisha wazazi pamoja na lishe kwa watoto wenye umri wa miaka
3-4.
Nae muuguzi
wa Zahanati ya Shadi Maria Geoffrey amewataka wazazi kuendelea kuwapeleka Kliniki watoto hadi
wanapofikisha umri wa miaka mitano kwani ni kipindi ambacho wataalam
wanaendelea kufuatilia afya ya mtoto ili kumwezesha kufikia ukuaji timilifu.
Maria
amesema wazazi wengi wanafanya makosa kuacha kuwapeleka watoto Kliniki hasa
watoto wenye umri wa miaka 2-3 kwasababu bado wanatakiwa kupatiwa chanjo hizi
za Matone, Vitamin A na Dawa za Minyoo ambazo huwasaidia kujikinga na minyoo na
Vitamin A humkinga mtoto na maambukizi ya magonjwa ya macho.
Maria ameyataja
magonjwa mengine yanayoweza kumpata mtoto asiyepata chanjo kuwa ni pamoja na
kifua Kikuu,ugonjwa Polio, Ugonjwa wa
kuharisha,Homa ya uti wa mgongo, Pepo punda, kifaduro, Surua,Homa ya
ini, Vichomi lakini pia mtoto anaweza kupoteza maisha.
Mpango wa taifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali unaonyesha kundi la umri wa miaka 3-5 linatakiwa kuendelea kupata huduma nyingine za lishe kama vile ufuatiliaji wa ukuaji, nyongeza ya vitamini A, vidonge vya minyoo na usimamizi jumuishi wa magonjwa ya watoto.
Hata hivyo inaonyesha pia changamoto iliyobaki ni wazazi kuacha kupeleka watoto wao kwenye kliniki za RCH mara kwa mara baada ya kumaliza chanjo wafikapo miaka 2.
No comments