MAKTABA YA WATOTO HOSPITALI YA MKOA WA MWANZA NI KIVUTIO KWA WAKUBWA NA WATOTO
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Maktaba Ya Watoto
ni chumba maalumu cha watoto kucheza kikiwa kimepambwa na vifaa mbalimbali vya
kuchezea watoto huku kuta zake zikiwa zimepambwa na michoro ya herufi
mbalimbali.
Maktaba hii
ipo mkoani Mwanza katika Hospitali ya Mkoa ya Mwanza (Sekou Toure)na inaelezwa
kuwa kwa Tanzania Maktaba za watoto zipo mbili tu nchi nzima.
Afisa Ustawi
wa jamii mkoa wa Mwanza Faithmary Lukindo anasema vyumba hivi ni muhimu kwa kuwa
vinasaidia watoto kupata nafuu ya magonjwa haraka lakini pia watoto kupata
uchangamshi na kuweza kuwasiliana na wenzao kupitia michezo inayofundishwa
katika Maktaba hizo.
Faithmary amesema
waliamua kuanzisha maktaba hii hospitalini ili kuwasaidia watoto ambao wamelazwa
waweze kupata nafasi ya kujifunza kupitia Maktaba ya Watoto ambayo kiuhalisia
inawasaidia pia kupunguza maumivu ya ugonjwa wanaopitia kwa kipindi hicho.
“Mtoto anapoendelea
kukua magonjwa ni sehemu katika ukuaji wake lakini hata anapokuwa ameugua ukuaji
hausimami hatua za ukuaji zinaendelea kama kawaida na ubongo unaendelea kukua
kama kawaida kwa hiyo maktaba hii inamsaidia mtoto kupata fursa ya kujifunza
pale anapopata nafuu kidogo wakati akiendelea na matibabu”.alisema Faithmary
Kwa upande
wake Teddy John afisa ustawi katika hospitali ya Sekou toure kitengo cha ustawi wa jamii amesema maktaba
hii wa watoto inawasaidia sana watoto wanaolazwa kwa muda mrefu kupata nafasi
ya kujifunza huku wakiendelea na matibabu.
“Kabla hatujaanzisha
maktaba hii ya watoto ilikuwa mtoto anashinda wodini muda wote na ilikuwa
ikisababisha watoto kukosa amani na kulia muda wote lakini baada ya kuanzisha
maktaba hii ya watoto tumeona tofauti maana mtoto akiisha ingia kwenye chumba
hiki anabadilika anachangamka anaanza kucheza kwa kuwa kuna vitu vingi vya
michezo tumewawekea”.alisema Teddy
Amesema katika
maktaba hiyo wapo watoto wanaojifunza kusoma na kuandika na wapo watoto ambao
wao hucheza kupitia michezo mbalimbali iliyopo katika chumba hicho.
“Kwa kweli
watoto hufurahia sana wanapokuwa hapa maana kuna midori kuna magari wanaendesha
kiasi kwamba watoto wengine wakiishaingia
maktaba kucheza huwa hawataki kuondoka kutokana na michezo iliyopo
kuwavutia”.alisema Pendo
Mmoja wa
wazazi ambae amelazwa hospitalini hapo kwa zaidi ya mwezi mmoja amesema mara ya
kwanza msimamizi wa Maktaba ya Watoto alipoenda kumchukua mtoto wake alikuwa na
wasiwasi kuwa mtoto wake ataenda kusumbua lakini ilikuwa tofauti kabisa na
alivyofikiria.
“Matroni alipokuja
kumchukua mtoto mara baada ya kutibiwa na daktari nilitaka kumkatalia lakini
nikashangaa nusu saa nzima kimya mtoto hajarudishwa maana namjua mtoto wangu
huwa mara nyingi anapenda kuwa na mimi tu sasa nikaamua kwenda kumuona
nilipoingia kwenye Maktaba hiyo ya Watoto nilishangaa ilivyo nzuri na
nilishangaa kumuona mtoto wangu amechangamka anacheza utadhani haumwi”.alisema
mzazi huyo
Bila shaka
katika tafiti zilizopangwa kufanyika ili kusaidia mchakato wa kutengeneza
taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Malelezi, Makuzi na Maendeleo ya
Awali ya Mtoto (MMMAM) kwa kutambua ubunifu,
mbinu zilizoleta matokeo chanya, vizuizi na viwezeshi utaigusa hospitali hii ya
mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) kwa ubunifu huu wa kuwa na Maktaba Ya Watoto
kwaajili ya watoto wanaotibiwa katika hospitali hiyo.
No comments