Breaking News

HALMASHAURI YA NYANG'HWALE MKOANI GEITA YAKWAMA KUFIKIA LENGO LA UANDIKISHAJI AWALI LA KWANZA 2024

 Salum Maige, Geita.

Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita bado imekwama kufikia lengo lake la kuandikisha wanafunzi 15,838 wa darasa la awali na la kwanza katika uandikishaji ulioanza tangu disemba mwaka jana.


Malengo ya halmashauri hiyo ilikuwa ni kaundikisha wanafunzi wa darasa la awali 8,213 na wale wa darasa la kwanza halmashauri hiyo ilitarajia kuandikisha wanafunzi 7,625.

Kwa mujibu wa afisa elimu ya awali na msingi wilaya ya Nyang’hwale Nassoro Hamis hadi kufikia januari 30,mwaka huu wanafunzi waliokuwa wameandikishwa ni 13,555 wakiwa ni wanafunzi wa awali na msingi.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita akizungumza kwenye kikao kazi kilichoenda sambamba na uzinduzi wa Programu jumuishi ya taifa ya malezi na makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) wilayani humo.

Amefafanua kuwa,matarajio ni kuandikisha wanafunzi 8,213 wa darasa la awali lakini hadi kufikia January 30,wanafunzi waliokuwa wameandikishwa ni 6,681 sawa na asilimia 81.35.

Kwa upande wa darasa la kwanza matarajio ya idara hiyo yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 7,625 lakini wanafunzi waliokuwa wameandikishwa katika kipindi hicho ni wanafunzi 6,874 sawa na asilimia 90.2.

“Lakini uandikishaji unaenda hadi machi mwaka huu,hivyo niwasihi sana wazazi na walezi waendelee kuleta watoto ,wasiwatumikishe kulea,kuna watoto wadogo wanaaachiwa wadogo zao wazazi wanaenda shamba ,hii haikubaliki tunaomba sana wazazi wajitokeze kuwapa watoto fursa ya kujifunza”anasema Hamis.

Katikati ni mkuu wilaya ya Nyang'hwale Grace Kingalame akiwa katika picha ya pamoja na timu PJT-MMMAM mkoa wa Geita mara baada ya kuzindua programu hiyo wilayani kwake.

Aidha,akizungumzia kuhusu suala la ujifunzaji wa awali amebainisha kuwa tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi 575,000 kwa halmashauri hiyo kununua zana za kujifunzia watoto wanaosoma elimu ya awali ikiwa ni hatua zinazochukuliwa za kuboresha fursa za ujifunzaji kwa watoto wadogo.

Amesema fedha hizo zinaenda kutumika katika kuboresha madarasa ya awali kwa shule 11 kati ya shule 74 za wilaya hiyo.

“Hata hivyo kupitia mradi wa busta unaotekelezwa na serikali huu,madarasa ya awali matatu ya mfano yamejengwa ambayo yanayoengea yakiwa na kila kitu,michoro,bebea na walimu wenye uzoefu wa kufundisha watoto wa awali”alisema Hamis.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kharumwa wilayani humo wanasema kwa kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea inawezekana matarajio hayo ya serikali yakafikiwa.

Husein Ally mkazi wa kijiji hicho anasema, kwa kuwa zoezi linaendelea yawezekana baadhi ya wazazi wakawa wamechelewa kuandikisha kwa sababu mbalimbali.

Anazitaja sababu hizo kuwa ni pamoja hali ngumu ya maisha kwa baadhi ya wazazi kushindwa kununua mahitaji ya shule kama vile madaftari,sare na umbali mrefu wa watoto kwenda shule.

“Wapo wazazi lakini si wengi wanaoshindwa kuandikisha watoto wao kwenda shule kwa sababu uhamasishaji ni mkubwa sana kupitia mikutano ya hadhara,wananchi wanatangaziwa na viongozi wanafuatilia”anasema Salome Cherehani na kuongeza.

“Labda mzazi anayeshindwa kuandikisha mtoto wake atakuwa na matatizo yake binafsi labda hali ngumu ya maisha,kwanza mtoto unaacha kumpeleka shule ili iweje,mtoto mdogo hata akibaki nyumbani atakusaidia nini wewe mzazi?’’

Hatua hiyo inakuja wakati serikali kwa kushirikiana na wadau wa watoto wakiwa wanatekeleza program jumuishi ya taifa ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) iliyozinduliwa disemba ,2021.

Aidha hivi karibuni wakati akizindua program jumuishi ya taifa ya maelezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM)mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Grace Kigalame amewataka wadau wa watoto wakiwemo wenye vituo vya malezi kuhakikisha vituo hivyo vinakuwa na madarasa yanayoongea.

“Tunaposema madarasa yanayoongea ,ni madarasa ya vitendea kazi,vifaa vyote vya kujifunzia kwa mtoto wa awali,vivyo hivyo kwa shule za msingi za serikali na binafsi kuwepo na ubunifu wa vifaa na vitendea kazi wezeshi kwa watoto”anasema Kingalame.

Aliongeza kuwa, vifaa hivyo vitamsaidia mtoto kujifunza na kumchangamsha kimwili na kiakili ili kufikia malengo ya program hiyo ya kuondoa viashiria hatari vinavyoweza kusababisha mtoto kutofikia ukuaji timilifu.

Mratibu wa mradi wa mtoto kwanza mkoa wa Geita kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la NELICO linalotekeleza program ya MMMAM kwa kushirikiana na serikali Bi.Sophia Njete amesema zana kujifunza humsaidia mtoto kuchangamsha akili yake ipasavyo.

Anasema zipo changamoto pia kwa wazazi wanaopeleka watoto wao kwenye vituo kule kwamba wanataka mtoto ajue kusoma na kuandika baada ya siku chache bila kuangalia umri wake na hatua za kuanza kujifunza.

“Tunapokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa vituo kwamba wazazi wanataka watoto mtoto aandike,Hapana mtoto huanza kujifunza kuhesabu kwa kuimba kwa picha lakini pia umri,mtoto ana miaka mitatu au mine mzazi anataka ajue kuandika,tunaharibu watoto”anasema Njete.

Kwa mujibu wa taarifa ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,halmashauri ya Nyan’ghwale inakadiriwa kuwa na jumla ya watu 241,034 kati ya hao watu 55,101 sawa na asilimia 23 ni watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.


No comments