Breaking News

WAFANYABIASHARA ACHENI KUSHINDA NA WATOTO SOKONI-SERIKALI

Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

Desemba 2021 Serikali ilizindua Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) Desemba 2021 ikiwa na lengo la kutekeleza afua tano za malezi ambayo ni pamoja na lishe, afya, elimu, malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama.

Programu hiyo inalenga watoto wenye umri kuanzia umri wa miaka sifuri hadi minane, Fatuma Issa ni mfanyabiashara wa soko la Tandika lililopo Manispaa ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam ambaye analazimika kwenda na mtoto wake sokoni Khamis Suleiman (2.9) kutokana na kukosa mtu wa kulea mwanae wakati yeye akisaka mkate wa kila siku.

Akizungumza hivi karibuni anasema kuwa, mtoto wake ni mdogo na mazingira siyo rafiki, nakwamba analazimika kuondoka naye asubuhi na kurudi naye jioni kila siku ili aweze kumuweka katika mazingira salama zaidi kuliko kumuacha nyumbani ambako hakuna usalama wa kutosha kwa mtoto.

“Nina watoto sita akiwamo huyu Khamis, nalazimika kuondoka na mwanangu kila siku kwenda sokoni kufanya biashara na kurudi naye jioni kwa sababu hakuna mtu wa kubaki nae nyumbani, dada na kaka zake wote ni wanafunzi.

“Naishi nyumba ya kupanga na kama unavyojua kuwa maisha ni magumu, lazima nitoke ili watoto wale, wasome na nilipe fedha ya pango,” anasema Fatuma.

Anaongea kuwa, Khamis sio wa kwanza kwenda nae kufanya biashara, hata baadhi ya watoto wake wakubwa alikuwa akiondoka nao kwenye maneno ya biashara na sasa hivi wanasoma shule ya msingi na kufanya vizuri darasani kama ilivyo watoto wengine wanaotoka kwenye familia zenye uwezo.

“Ningekuwa na uwezo, ningetafuta mtu wa kulea mwanangu, lakini sina na maisha ni magumu, nina watoto sita, watano wanasoma kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, wanarudi jioni na wanafanya vizuri darasani kama ilivyo watoto wengine wanaotoka kwenye familia zenye uwezo, mwanangu anashindwa kupata mtu wa kucheza nae mpaka kipindi cha likizo ambacho ndugu zake wapo nyumbani, namuacha nyumbani na mimi napata nafuu,” anasema.

Kitaalam ikoje

Mtaalam wa Elimu, Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Children In Crossfire (CIC), Davis Gisuka anasema kuwa, kitendo cha mzazi kwenda na mtoto kwenye maeneo ya masoko kufanya naye biashara kunaweza kusababisha mtoto kujifunza vitu visivyo na maadili, kwa sababu lugha zinazotumika kwenye maeneo hayo kwa baadhi yao siyo rafiki kwa mtoto.

Amesema kuwa, ubongo wa mtoto unakua kwa kasi, anaweza kushika mambo mabaya na mazuri, jambo ambalo linahitaji umakini wakati wa makuzi yake.

Amesema kuwa, lakini pia, maeneo hayo kuna baadhi ya mambo yanayofanyika yanaweza kusababisha mtoto kufanyiwa vitendo vya ukatili wa aina moja au nyingine.

“Baadhi ya wafanyabiashara wanatumia lugha zisizo rafiki kwa mtoto, hivyo basi ni rahisi kujifunza mambo yasiyofaa akiwa mdogo.

“Ubongo wa mtoto unakua kwa kasi sana, akifika umri wa miaka 3-4 ubongo wake unakua kwa asilimia 75 hadi 80, na anapofikisha umri wa miaka mitano ubongo wake unakua kwa asilimia 90, hivyo basi ni rahisi kujifunza mambo mazuri na mabaya inategemea na mazingira husika,” anasema Gisuka.

Ameongeza kuwa, ndiyo sababu wanashauri serikali kujenga vituo vya kulea watoto mchana (DCC) kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya kibiashara ikiwamo masoko ili mtoto aweze kukaa kwenye maeneo salama wakati mzazi anaendelea na majukumu yake.

“Ikiwa mtoto atapelekwa kwenye kituo hicho, ataweza kujifunza mambo mbalimbali ya kukuza ubongo wake kimwili na kiakili,” anasema.

Ustawi wa Jamii

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha amesema kuwa, serikali itaendelea kutoa elimu kwa wazazi ili waweze kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kulea mchana kuliko kwenda naye sokoni ambako hakuna maadili mazuri ya kujifunza.

Anafafanua zaidi kuwa, mtoto anapopelekwa kituoni anakuwa salama zaidi kuliko anapoenda nae kwenye shughuli za kijamii ambazo zinaweza kumfanya kujifunza vitu visivyo na maadili.

“Kwenye maeneo ya biashara kuna baadhi ya watu wanaweza kuongea lugha zisizo na maadili, ikiwa utaenda na mtoto utamfanya ajifunze vitu visivyofaa, hivyo basi wanapaswa kuwapeleka kwenye vituo ili waweze kujifunza na kujichanganya na watoto wenzake,” anasema Nyamara.

Mtaalamu wa Lishe

Kwa upande wake, mtaalam wa lishe, Khadija Lyeluu anesema kuwa, mzazi anapoenda na mwanae sokoni kufanya biashara, uwezekano wa kumpa vyakula vyenye virutubisho ni mdogo, kwa sababu atakuwa ‘busy’ na biashara na mtoto kulishwa chakula chochote kitakachoonekana ilimradi ashibe.

Amesema kuwa, mtoto anahitaji lishe bora ili aweze kukua katika hali ya utimilifu, anatakiwa kunyonya ziwa la mama hadi anapotimiza miezi sita na kuanza kula vyakula mchanganyiko vikiwamo maji na matunda.

“Ikiwa mama yupo ‘busy’ na biashara, maanayake hata muda wa kunyonyesha hana, mtoto atapewa chakula chochote atakachokumbana nacho kwenye mazingira yake, jambo ambalo linaweza kusababisha kupata udumavu,” amesema Lyeluu.

Amesema kuwa, baadhi yao hawafanyi hivyo kwa kisingizio cha kutafuta fedha, jambo ambalo linasababisha udumavu, hivyo basi wataendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuona umuhimu wa mtoto kula vyakula vyenye virutubisho ambavyo vitaweza kumjenga kimwili na kiakili.

Serikali

Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na watoto iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ikiwepo haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na haki ya kutobaguliwa.

Sambamba na hilo, serikali iliweza kuratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ambayo kila mwananchi anapaswa kuitekeleza.


No comments