IMF YAITAJA TANZANIA MIONGONI MWA MATAIFA 10 YENYE MADENI MADOGO ZAIDI BARANI AFRIKA
# IMF yaitaja Tanzania miongoni mwa mataifa 10 yenye madeni madogo zaidi barani Afrika
Januari 18, 2024
Na Mwandishi Wetu Zanzibar
Hatua ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuitaja Tanzania miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika yenye deni dogo la taifa imedhihirisha mafanikio ya mageuzi ya kiuchumi yanayoendelea nchini tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani karibu miaka mitatu iliyopita.
Chini ya utawala wake, Rais Samia ameongeza maradufu uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu na huduma za jamii, ikiwemo sekta za elimu, maji, afya, umeme na kilimo.
Uwekezaji wa serikali, hususan kwenye ujenzi wa miundombinu, umechochea ukuaji wa uchumi nchini.
Kupitia mkakati wa Royal Tour, Rais Samia pia ameongeza kwa kiasi kikubwa sana idadi ya watalii wanaokuja nchini.
Ongezeko la watalii limeleta pesa za kigeni nchini na kuongeza ajira.
Vilevile, Serikali yake imeongeza bajeti kwenye sekta ya kilimo kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana tangu nchi ipate uhuru na hivyo kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Sera rafiki za Serikali ya Samia kwa sekta binafsi zimesaidia kuongeza kasi na ukubwa wa uwekezaji wa makampuni ya nje na ya ndani.
Rais Samia pia ameweza kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia wa Tanzania na taasisi za kimataifa na nchi za nje ambazo zimeongeza utoaji wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa Tanzania.
Mikopo nafuu yenye riba ndogo na muda mrefu wa marejesho imepunguza mzigo wa deni la taifa.
Pamoja na kwamba Tanzania imeendelea kukopa nje ili kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, ukopaji makini wa Serikali ya Rais Samia wa kutumia mikopo nafuu badala ya mikopo yenye masharti ya kibiashara na ukuaji wa kasi kubwa wa Pato la Taifa (GDP), vimepunguza mzigo wa deni la taifa.
Uwiano wa Deni la Taifa kulinganisha na GDP ambao hutumiwa na IMF na wachumi wengine duniani kupima uhimilivu wa deni la taifa, uko chini Tanzania kulinganisha na wastani wa dunia.
Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa jumla ya deni duniani sasa hivi ni Dola za Marekani trilioni 307, ambayo ni sawa na asilimia 336 ya GDP ya dunia.
Zifuatazo ni nchi 10 za Afrika zenye uwiano wa Deni la Taifa mdogo kabisa kwenye bara hilo kuilinganisha na pato la taifa (GDP), kwa mujibu wa IMF:
🇨🇩 DRC 11.1%
🇧🇼 Botswana 18.1%
🇪🇹 Ethiopia 31.2%
🇬🇼 Guinea Bissau 31.5%
🇬🇶 Equatorial Guinea 33.7%
🇰🇲 Comoros 36.9%
🇹🇩 Chad 38.7%
🇨🇲 Cameroon 39.6%
🇳🇬 Nigeria 41.3%
🇹🇿 Tanzania 41.8%
Nchi 10 duniani zenye kiwango kikubwa cha deni (uwiano wa Deni la Taifa kulinganisha na GDP) hizi hapa:
Japan🇯🇵 264%
Singapore 🇸🇬 160%
Italia 🇮🇹 145%
Marekani 🇺🇸 129%
Hispania 🇪🇸 113%
Canada 🇨🇦 113%
Ufaransa 🇫🇷 112%
Uingereza 🇬🇧 101%
India 🇮🇳 89%
Argentina 🇦🇷 85%
No comments