Breaking News

WAZAZI CHANJO CHA UGONJWA SELIMUNDU UNAOPOTEZA MAISHA YA WATOTO

                                                       Na Tonny Alphonce, Mwanza

Nilipo mzaa mtoto wangu miezi michache baadae alianza kuumwa mara kwa mara na ukuaji wake ulikuwa wa taratibu sana, nilijitahidi kumpatie lishe lakini sikuona mabadiliko.

Niliamua kuwauliza watu wazima wanaonizidi umri ili wanisaidie kujua nini kinamsumbua mtoto wangu, mama wa kwanza aliniambia mtoto wangu atakuwa amerogwa na mama wa pili alinishambulia kwa matusi akidai kuwa nimefanya umalaya nikiwa bado nanyonyesha hivyo nimemsababishia matatizo mtoto wangu halafu najifanya sijui tatizo la mwanangu.

Hayo ni maneno ya Nyanzala Magulu mkazi wa Kisesa mkoani Mwanza ambae alimpoteza mtoto wake akiwa na miaka mitatu baada ya kufariki kwa ugonjwa wa Selimundu ugonjwa ambao umekuwa ukisababisha vifo vya watoto kwa asilimia 70 hadi 90 ambapo watoto wanaozaliwa na ugonjwa  huo hupoteza maisha  ndani ya kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya maisha yao.

Nyanzala anasema hakujua kama mtoto wake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Selimundu hali iliyopelekea kifo chake baada ya kuchelewa kumpeleka hospitali kwaajili ya matibabu na kuitaka serikali na wadau wengine  kutoa elimu kwa jamii ili iwe na ufahamu wa kutosha kuhusu ugonjwa huu.

“Mtoto wangu aliteseka sana na ugonjwa huu, alipungukiwa damu mara kwa mara na kunawakati kila kiungo kilimuuma nikawa nashindwa hata nimbebe vipi maana ukimshika mkono analia ukimshika miguu analia aliteseka”.alisema Nyanzala

Mwenyekiti wa taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania Priscilla Chassama amesema kabla ya kuianzisha taasisi hiyo mwaka 2018 walifanya utafiti na kugundua kuwa jamii haina elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huu na ndio sababu Selimundu bado ni tatizo katika jamii.

Mwenyekiti wa taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania Priscilla Chassama akielezea namna seli zinavyofanyakazi.

Chassama amesema ni rahisi kupambana na ugonjwa wa Selimundu kwa kuwa ni ugonjwa wa kurithi ambapo baba na mama wanachangia kumzaa mtoto mwenye ugonjwa huo.

“Ile damu ya baba na mama badala ya kuwa na umbo la duara  ina kuwa na umbo kama la nusu mwezi ndio maana tunaita Selimundu ugonjwa huu yani seli iliyojikunja”alisema Chassama

Chassama amesema kutokana na seli kujikunja inaleta madhara ikiwemo kusababisha upungufu wa damu kwasababu inavunjwa sana kitu ambacho siyo sawa katika mwili.

Amesema ugonjwa huu pia husababisha maumivu makali ya viungo na sehemu mbalimbali za mwili wa mtoto kutokana seli hizi kujikunja husababisha kukwama kwenye mishipa ya damu.

“Seli hizi sio kama hizi za kawaida ambazo zinaweza kujiminya ndio maana huwa zinasababisha maumivu ya miguu, mikono na maeneo mengine ya mwili wa mtoto na hiyo seli ikikwama kwenye mishipa ya kichwani husababisha ugonjwa wa kupooza”.alisema Chassama

Amesema pia seli hiyo ikikwama kwenye mapafu mtoto anaweza kupata lemonia ya sikoseli lakini pia husababisha ukuaji duni kwa mtoto kwa sababu seli hii haibebi oksijeni ya kutosha kupeleka sehemu mbalimbali za mwili ili kufanya mtoto aweze kukua vizuri.

Chassama amewataka wazazi na walezi kuwapeleka mapema watoto hospitali mara tu wanapohisi mtoto kuwa na dalili za ugonjwa wa Selimundu ikiwemo kupungukiwa damu mara kwa mara,ukuaji wa taratibu pamoja na mtoto kulalamika maumivu ya mwili.

Amesema mtoto akipelekwa hospitali atapimwa na kupewa  vidonge vya folic acid kila siku na vitamin D kwaajili ya kusaidia  vitu mbalimbali kwenye mifupa, dawa ya hydroxyurea ambayo ni nzuri kwa watoto wa chini ya miaka mitano pamoja na penicillin v kwaajili ya kutuliza maumivu ya kifua.

Chassama pia amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima vinasaba kabla kuoa au kuolewa ili kujua vinasaba vikoje kabla ya kupata mtoto kwa kufanya hivyo jamii itapunguza au kumaliza tatizo la sikoseli.

Nae daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Bugando Emmanuela Ambrose amesema tatizo hilo ni kubwa nchini ambapo Tanzania ni nchi ya 5 ikiwa na watoto zaidi ya 14000 wanaozaliwa na ugonjwa huo wengi wao wakitokea Kanda ya Ziwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka Bugando Emmanuela Ambrose akielezea ukubwa wa tatizo la Selimundu kwa watoto.

Amesema kwa Bugando peke yake ina zaidi ya watoto 1000 ambao wanahudhuria kliniki kila mwaka kwaajili ya matibabu ambapo kila siku jumatatu huwatibu watoto 30 hadi 50 huku ijumaa watoto 50 hadi 80.

Dkt Emmanuela amesema kuwa bado utafiti mkubwa unahitajika ili kuelezea bayana ukubwa wa tatizo hilo kwani bado watoto wengi wanazaliwa wakiwa na shida hiyo.

Amesema ukubwa wa tatizo hilo unasababishwa na watu kutoelewa kama wamebeba chembechembe za ugonjwa huo na mara nyingi wanatambua mara baada ya kupata mtoto.

“Ni vyema wakapima kabla ya kuingia kwenye ndoa lakini pia mtoto anapozaliwa apimwe na akikutwa na tatizo hilo la Sikoseli aanzishiwe kiliniki na matibabu mapema ambayo yatamsaidia kutibu matatizo  yote yatokanayo ugonjwa huo hivyo kumfanya kuishi muda mrefu”.alisema Dkt Emmanuela

Akizungumzia matibabu ya Selimundu amesema ni gharama kubwa na inamlazimu mzazi awe na fedha hasa wenye watoto walio na umri wa juu ya miaka mitano ambao serikali haiwaghramii.

Tanzania imekuwa ikitekeleza Program Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto yenye lengo la kumaliza changamoto za afya kwa watoto na changamoto nyingine dhidi ya watoto hususani walio chini ya umri wa miaka nane.

Wenza kupima afya zao na kujua hali zao kabla kuamua kuzaa kutasaidia watoto watakaozaliwa kuwa na afya njema kuanzia akiwa tumboni kwa mama mpaka hatua za awali ya makuzi yake.


No comments