Breaking News

TANGA YAPOKEA VIFAA TIBA KWAAJILI YA KUANZISHA WODI YA WATOTO NJITI

 Raisa Said,Tanga

Juhudi za kuokoa watoto njiti katika Jiji la Tanga zinazidi kushika kasi baada ya Hosptali mpya ya Wilaya yaTanga kupata msaada wa vifaa vya wodi ya watoto njiti vyenye thamani ya Sh milioni 35.


Vifaa hivyo ambavyo vimatolewa na Mfuko wa Dr Doris Mollel vitaiwezesha hospitali hiyo kuanzisha kitengo maalum cha watoto wanaozaliwa kabla ya wakati. Vilikabidhiwa kwa Waziri wa Afya UMMY Mwalimu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Doris Mollel na Msanii Elias Barnaba ambaye ndiye Champion wa kampeni ya kuokoa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Waziiri huyo, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tanga, alisema msaada wa Dk Mollel ni muhimu sana katika kupunguza vifo vya watoto njiti katika Jiji la Tanga na kupunguza mzigo wa kazi unaoikabili Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga iliyopo Bombo jijini hapa. Vifaa hivyo vilitolewa na Assemble Insurance ambayo ilitoa 5Million na mfadhili mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe 30Million.

Hivi sasa hospitali ya mkoa inapokea watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao kutoka takriban wilaya zote za Mkoa wa Tanga, jambo linalofanya Jiji la Tanga kuonekana kuwa na vifo vingi vya watoto njiti.

Waziri Ummy akitoa shukrani kwa Taasisi hiyo, ambayo imefanya kazi katika kampeni ya kuokoa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa miaka minane, alisema kuwa mchango huo unaenda sambamba na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuokoa vifo vya wajawazito na watoto wakiwemo watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.


 “Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa kuna wodi ya watoto njiti katika hospitali zote za wilaya. Tumefanya hivi kwa hospitali zote za mikoa,” alisema Waziri Ummy

Ummy alisema kuwa kupitia juhudi za Rais Dk Samia, nchi imepokea msaada wa  ya Sh Bilion 625 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha afya ya mama na mtoto nchini Tanzania.

“Juhudi za kuokoa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati zinaonyesha dalili za mafanikio. Kitaifa, vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati vimepungua kutoka 67 kwa kila watoto 1,000  mwaka 2015 hadi 45 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa mwaka 2022.

Kwa watoto wenye umri wa mwaka mmoja kiwango cha vifo kimepungua kutoka 43 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi 33 lakini alibainisha kuwa walio kati ya umri wa siku moja hadi 28 bado kuna tatizo la  kupunguza vifo  walipungua kutoka 25 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hadi 24 pekee.

Akizungumzia hali hiyo kwa Mkoa wa Tanga, Ummy alisema vifo vya watoto njiti vimepungua kutoka 263 kwa kila watoto 1000 hadi kufikia 165. “ Kuna programu ya Wataalamu Bingwa wa Mama Samia  ambapo madaktari bingwa hufanya programu ya wiki mbili ya mafunzo kwa vitendo katika vituo vya afya ili kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya jinsi ya kuhudumia watoto njiti,” alisema.

Akizungumzia msaada huo, Dk Doris Mollel alisema taasisi hiyo imetoa msaada kwa vituo vya afya zaidi ya 70 na hospitali tano tangu walipoanza kampeni miaka minane iliyopita.

Msanii Barnabas alisema amefurahishwa na kuwa sehemu ya kampeni ya kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na kutoa wito kwa wasanii wengine na vyombo vya habari kuungana katika mapambano hayo ili kuokoa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Naye Mganga Mkuu wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Dk Mohamed Salim alisema watoto wanaozaliwa njiti wanahitaji uangalizi mkubwa wa wataalamu mara baada ya kuzaliwa kwa sababu wanakabiliwa na matatizo kama vile kupungua kwa sukari mwilini na kushindwa kupumua.

Dk Salim alisema kuwa kuanzishwa kwa kitengo hicho katika Hospitali ya Wilaya ya Tanga kutasaidia kupunguza mzigo wa kazi unaoikabili Bombo.

Uwekezaji katika sekta unaenda sambamba na program Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  yenye lengo la kumaliza changamoto za afya kwa watoto ili waweze kukua katika utimilifu wao kuanzia mwaka 0-8.


No comments