TACEC YAJA NA KAMPENI YA MALEZI, MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO MIAKA 2-3
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Shirika la
Tanzania Early Childhood Education and Care (TACEC) limeanzisha kampeni ya
dakika 30 za kucheza na kujifunza na mtoto nyumbani kila siku ikiwa na lengo la
mzazi kushiriki kumuandaa mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 2-3 kwa ajili ya elimu ya awali na kuendelea.
Kampeni hiyo
ya TACEC inahusisha mpango jumuishi wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya
mtoto mwenye umri kati ya miaka 0-8 unaolenga kuhakikisha mtoto anakingwa na
hatari zote zinazoweza kuathiri maisha na ustawi wake wa baadae.
Kwa mujibu
wa Bi Ester Macha ambaye ni mtaalamu wa
elimu ya awali kutoka TACEC anasema kampeni hiyo ya dakika 30 za kucheza na
kujifunza na mtoto nyumbani,kampeni ambayo itamsaidia mzazi kujua uwezo wa
mtoto wake katika kutoa maamuzi,kufanya jambo,kutatua tatizo kupitia michezo
zaidi ya 30 ambayo wameiandaa kupitia kitabu ambacho kinatoa maelekezo ya
michezo hiyo.
Ester
amesema kupitia kampeni hiyo wamekuwa wakiwatembelea wazazi majumbani kwa lengo
la kutoa elimu namna gani wanaweza kucheza na watoto michezo ambayo itamjenga
mtoto kiakili ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya elimu yake ya awali.
“Sisi
tuliona kuna pengo hilo la huyu mtoto kutopata maandalizi yoyote ya kumuandaa
na elimu ya awali lakini pia katika umri huu wa miaka 2-3 ndio umri ambao mzazi
anaweza kugundua kipaji cha mtoto wake kwa kuchezanae lakini pia mzazi anaweza
kuelewa uwezo wa mtoto wake katika kujifunza au kufanya vitu na hii itasaidia
hata kujua kama mtoto wake anaelewa haraka au taratibu”.alisema Ester
“Mtoto
ukiona anachukua unga au nchele anajaribu kupika usimchape mkataze kwa maneno
ukijaribu kumuelekeza kwamba akitaka kupika achukue mchanga ndio apike asitumie
unga au mchele kwasababu atahitaji kula baadae mtoto atakuelewa”.alisema Ester
Nae
mkurugenzi wa shirika la Uzao Wetu Yusuph Mtobela amewataka wazazi wenye watoto
wa umri wa miaka 2-3 kujua lugha ya mtoto ambayo ni michezo ili kugundua kipaji
alichonacho mtoto kupitia michezo anayocheza.
“Binadamu kiasili anavipaji vinane na kuendelea kiasili hivyo mzazi anaweza kugundua na kuendeleza kipaji cha wake wakati anapochezanae cha msingi michezo hiyo lazima inazingatie usalama wa mtoto na iwe uhusiano na namna ya kumuendeleza kielimu”.alisema Mtobela
Amesema ili
kuhakikisha kuwa kundi hili la watoto linasaidiwa na walezi shirika la Uzao Wetu limeanzisha mafunzo ya
malezi na makuzi ya mtoto mahali pa kazi ambapo wamewalenga wazazi na walezi
ambao wanapewa mafunzo ya kujenga mahusiano baina yao na mtoto kwa lengo la
kumuandaa na elimu ya awali.
Magembe
amesema suala hili la watoto hao wa miaka 2,3 kusahaulika linaweza kufanyiwa kazi
na serikali endapo wadau watatoa hoja za msingi na kuzipeleka kwa watunga sera
kwaajili ya kufanyiwa kazi.
Amesema kuanzisha
Vituo vya Malezi na Makuzi ya awali kwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili,
mitatu na minne nchi nzima ni moja ya mikakati ya kumjenga na kumlinda mtoto.
“Ukitaka
kujua serikali ni sikivu angalia kuhusu vituo hivi vya kulelea watoto,baada ya
kuonekana vinahitajika takwimu zinaonyesha kuwa Mwaka 2020, Serikali ilisajili
vituo 134 vya kulelea watoto wadogo mchana ikilinganishwa na vituo 373 mwaka
2019 na kufanya jumla ya vituo vilivyosajiliwa kufikia 1,677”.alisema Magembe.
Neema Thodas
mama mwenye mtoto wa mwaka mmoja na nusu mkazi wa kata ya Luchelele anasema
kabla ya kupewa mafunzo hayo ya namna ya kucheza na mtoto wa umri wa miaka 2-3
kwaajili ya kumuandaa na elimu kumekuwa na mabadiliko makubwa katika malezi
yake kwa kuwa hivi sasa amekuwa akicheza na mtoto wake michezo ambayo
inamuandaa kuanza kuandika, kuhesabu pamoja na kujua vitu mbalimbali na matumizi
yake.
Raheli
Sengesa mkazi mtaa wa Kasamiko kata ya Luchelele ambae anaishi na wajukuu wake
anasema hakujua kama watoto hawa wenye umri wa miaka2-3 wanaweza kundaliwa
kwaajili ya elimu ya awali kwasababu alijua hiyo ni kazi ya walimu pale mtoto
anapoanza shule.
Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu Msingi (MMEM) 2012- 2016, vimebainisha kuwa elimu ya awali ni moja kati ya vipaumbele vya serikali.
Kwa Tanzania watoto wenye umri wa miaka 4-5 huanza elimu ya awali na umri wa miaka 5-6 mtoto huanza darasa la kwanza huku watoto wenye umri wa miaka 2-3 hawaguswi na Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi.
No comments