MASHIRIKA 6 YANAYOJIHUSISHA NA MAZINGIRA MWANZA YAUNGANA ILI KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Katika kuunga mkono mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi wa mwaka 2021 – 2026 mashirika 6 yanayojihusisha na utunzaji wa mazingira na tabia nchi ya jijini Mwanza yameanza kampeni ya kubadilisha tabia za wananchi katika utunzaji wa mazingira kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari mwanaharakati wa mazingira na mjumbe wa mtandao wa kijinsia na mabadiliko ya tabia nchi Tanzania Sophia Donald amesema suala la mabadiliko ya Tabia Nchi linagusa watu wa jinsia zote hivyo mpango walionao ni kuhakikisha wanawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa mazingira.
Sophia amesema
hatua ambayo wameichukua kwa hivi sasa ni kuwakutanisha wadau wa mazingira
pamoja na maafisa kutoka serikalini kwa lengo la kujadiliana na kupata azimio
moja ambalo litafanyiwa kazi mashirika yote 6 yaliyoungana.
“Kwa hivi
sasa katika kuhakikisha uhamasishaji
unayafikia makundi yote tunatumia mikutano ya hadhara ili kufanya uhamasishaji
kwa jamii, kushirikiana na vyombo vya habari
na sekta za Kiserikali zinasimamia masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi”.alisema Sophia
Kwa upande
wake Franklin Kamalamo kutoka Taasisi ya Mazingira Bora amesema Katika kuhakikisha kampeni hii ya kupambana na
changamoto za tabia nchi inaleta matokeo chanya watatoa elimu kwa pamoja wadau
wote wa mazingira na hii itasaidia elimu kufika kwa urahisi.
“Safari hii
tunaamini elimu itafika kwa urahisi kwa kuwa jamii tayari inaona mabadiliko
mfano kuongezeka kwa joto, maeneo ya joto kupata baridi kali hivyo nirahisi
wananchi kuelewa tunachokisema lakini pia tutatumia wasanii kufikisha ujumbe
kwa wananchi”.alisema Franklin
Nae Mkurugenzi
mtendaji wa shirika la Mikono Yetu Organization Maimuna Kanyamala amesema
katika kampeni hii wataelekeza nguvu kubwa pia kwenye shule za msingi ambao ni
watumiaji wakubwa wa miti ili wajue umuhimu wa kupandamiti kunakoendana na
matumizi yao ya kila mwaka.
“Katika kujenga
tabia lazima tuwaguse na hawa wenzetu wa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi
wanapanda miti na ikiwezekana lazima kila mwanafunzi awe na mti wake hii
itasaidia utunzaji wa mazingira”.alisema Maimuna
Naye Afisa
mazingira wa halmashauri ya Magu Ngusa Buyamba amesema katika kuhakikisha
mapambano hayo ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi ni lazima wahakikishe
wanapata taarifa sahihi kutoka katika malamaka sahihi za serikali.
"Kwa mfano mpango wa serikali kwa sasa ni kuwa kila halmashauri inatakiwa kuhakikisha inapanda miti milioni moja na laki tano, sasa ukiangalia halmashauri hazina uwezo kupanda miti hiyo na hapa ndio wadau wa mazingira wanatakiwa kuingia".alisema Buyamba
Mtandao wa
kijinsia na mabadiliko ya tabia nchi
Tanzania umejidhatiti kuhakikisha unatoa elimu ya mabadiliko ya tabia nchi na
kwa sasa mtandao unaendelea na kampeni ya kuielimisha jamii kwa njia mikutano
ya hadhara,kutumia vyombo vya habari
pamoja na mitandao ya kijamii.
No comments