Breaking News

KAMATI YA BUNGE YAMSHUKURU RAIS SAMIA KURUHUSU MIRADI YA UWEKEZAJI,


Na MWANDISHI WETU
Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imeishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa kibali cha kuendelezwa kwa mradi wa kitega uchumi wa Mzizima unaomilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Fatma Hassan Taufiq tarehe 14 Novemba, 2023 wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya ziara ya kutembelea mradi huo uliopo jijini Dar es Salaam.

Lengo la ziara hiyo ni kuona maendeleo ya mradi huo ambao ulisimama kipindi cha nyuma, lakini kwa maelekezo na busara za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliagiza miradi yote iliyosimama kwa sababu moja au nyingine ifanyiwe tathimini ili iweze kuendelezwa.

“Kamati inaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona uwekezaji huu uendelee kuwepo ili uweze kuleta tija kwa Watanzania, kuongeza ajira, kukuza thamani ya Mfuko, kukuza uchumi kwa kupata kodi ambazo zitasaidia kuleta maendeleo mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu na maji,” alisema.

Aidha, wameupongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuendelea kusimamia na kufanya uwekezaji wenye tija kwenye miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Mfuko maeneo mbalimbali.

Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na kazi kubwa inayoendelea kufanywa na NSSF katika utekelezaji wa mradi huo huku wakiipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa kibali cha kuendelea kukamilisha mradi huo ambao ulikuwa umesimama kwa muda.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye dhamira yake ni kukuza uwekezaji nchini.

Alisema mradi wa jengo la Mzizima lina minara miwili yenye urefu wa sakafu 35 na zina jumuisha sehemu ya biashara na makazi, hivyo litakapokamilika litafungua fursa mbalimbali za kiuchumi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, alisema maoni yote yaliyotolewa na wajumbe wa kamati wameyapokea na wataenda kuyafanyia kazi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea mradi huo ambao unafikia hatua za mwisho kukamilika.

Mshomba alisema ushauri waliopewa na wajumbe wa kamati hiyo wataufanyia kazi, huku akibainisha kuwa mradi utakapokamilika unatarajia kulipa ndani ya kipindi cha miaka 15 ambacho ni cha kawaida kwa miradi mikubwa kama hiyo.

“Mfuko unaendelea kukua na umefikia thamani ya trilioni 7 ukuaji huu ni mkubwa ukizingatia kwamba wakati Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani thamani ya NSSF ilikuwa ni shilingi trilioni 4.8,” alisema Mshomba.


No comments