SERIKALI YATAKIWA KUSOGEZA HUDUMA YA MAMA NA MTOTO KISHIRI MWANZA
Na Tonny Alphonce,Mwanza
Wakazi wa kata ya Kishiri wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wamekuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa zaidi ya sita ili kupata huduma ya kujifungua kwa mama wajawazito.
Emmaculata
Masanja mkazi wa Kishiri anasema serikali iliwahi kutangaza kumaliza tatizo
hilo kwa kujenga jengo la Mama na Mtoto
kupitia mfuko wa kusaidia Kaya Masikini (TASAF) lakini hadi sasa ujenzi
huo bado haujakamilika.
“Kwa hivi
sasa mama akikaribia kujifungua lazima uhakikishe unapesa ya usafiri wa
kumpeleka hospitali vinginevyo mjamzito anaweza kujifungua mkiwa njiani na
tukifika hospitali mama ameishajifungua wahudumu wa afya wanakuwa wakali
kwanini tumemchelewesha mama”. alisema Emmaculata
Makilagi
amesema malengo ya kujenga jengo la mama na mtoto katika kata ya Kishiri ni
kuwapunguzia adha akina mama wa ukanda wa huo waliokuwa wakifuata huduma umbali
mrefu hadi Igoma na kusababisha kujifungulia njiani na watoto pamoja na mzazi kupata
matatizo mbalimbali ya kiafya.
"Mratibu
wa TASAF hakikisheni jengo hili linakamilika kwa wakati na kuanza kutumika
maana linavyozidi kuchelewa ni wazi linakwamisha juhudi za wananchi
waliojitolea nguvu kazi kuhakisha mradi haukwami ili umalizike kwa wakati na wananchi wapate huduma wanayohitaji," amesema Makilagi.
Akizungumzia madhara ya mama mjamzito kucheleweshwa hospitali Getrude John Ndalifashe mkunga na mtaalamu wa
masuala ya mama,uzazi na mtoto kutoka shirika la Uzao Wetu amesema mama
na mtoto wote wanaweza kupata
madhara ukiwemo ugonjwa wa Fistula,kupoteza damu nyingi na mtoto anaweza kupata
tatizo la mtindio wa ubongo endapo ubongo wake utatikisika wakati wa kuzaliwa.
Getrude
amesema ni muhimu mama kuhakikisha anajifungulia hospitali kwa kuwa wakati mama
anapojifungua anaweza kupata changamoto zitakazohitaji kutatuliwa na wataalamu
wa afya wakiwemo madaktari bingwa.
"Mama
anapojifungua huwa tunangalia mambo mengi lakini pia huwa tunaangalia kama mtoto amepata maambukizi kwenye kitovu
wakati wa kuzaliwa kwasababu tofauti
yoyote inaweza kusababisha utofauti katika ukuaji wa mtoto".alisema Getrude
Malengo 17
ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yanatarajiwa kufikiwa mnamo
mwaka 2030, yaani kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi hadi kufikia uwiano wa 70 kwa vizazi hai 100,000.
Ripoti ya jamii na afya ya ofisi ya
Taifa ya Takwimu, 2015-16 TDHS-MIS yaonyesha kuwa kuna vifo 556 kwa kila vizazi
hai 100,000.
Pamoja na kuwa baadhi ya kata za mkoa wa Mwanza bado hazina huduma za Mama na Mtoto takwimu zinaonyesha kuwa Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitano
ambayo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaojifungua kwenye vituo
vya matibabu hii ni kwa utafiti uliofanywa mwaka 2018.
Mikoa mingine ni mkoa wa Dar es Salaam
unaongoza kwa kuwa na wanawake 128,853 wanaojifungua kwenye vituo vya matibabu
(asilimia 10.8). Mwanza, wanawake 79,077 (7%); Mbeya, wanawake 78,732 ( 7 %);
Dodoma, wanawake 63,208 ( 5 %); na Tabora, wanawake 61,457 (5%).
Tanzania imekuwa ikitekeleza Program Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto yenye lengo la kumaliza changamoto ya lishe duni na changamoto nyingine dhidi ya watoto hususani walio chini ya umri wa miaka nane.
Kukamilika kwa ujenzi huo wa jengo la mama na mtoto utasaidia ulinzi wa mtoto kuanzia akiwa tumboni kwa mama mpaka hatua ya awali ya makuzi yake.
No comments