WATOTO WANAOFUNGIWA NDANI HATARINI KUUGUA UGONJWA WA MACHO WA MYOPIA
Na Tonny Alphonce, Mwanza
Kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia, watoto wengi siku hizi wanapenda kutumia
vifaa vya kisasa na kuingia kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa macho wa Myopia ambapo
husababisha mtoto kuona vitu vya karibu, lakini hawezi kuona mbali.
Tatizo hili
limekuwa sugu kwa watoto wengi hasa wale wa miaka 2-10 maana hufurahia sana michezo hiyo
ya kwenye simu na matokeo yake ni kwamba, wanakosa mwanga wa jua, ambao ni
muhimu sana na hivyo kuwasababishia tatizo hilo la macho.
Mkuu wa
Idara ya macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Christopher Mwanansao amesema watoto
kutopata muda wa kucheza nje na badala yake kushinda ndani wakichezea simu za
wazazi wao na kutazama runinga ni hatari kwa afya ya macho yao hali ambayo
inasababisha watoto wengi wa kizazi hiki kusumbuliwa na maradhi ya macho.
Dk Mwanansao
amesema wagonjwa wengi wanaohudumiwa katika kliniki ya Bugando hukutwa na
tatizo la saratani ya mtoto wa jicho, mzio wa macho, presha ya macho, kisukari
cha macho na uoni hafifu, ambapo asilimia 60 ya watu wanaopata upofu hutokana
na tatizo la mtoto wa jicho ambalo huwakumba zaidi wazee na watoto wenye umri wa miaka 0-8.
Amesema
"kwa sehemu kubwa matatizo ya macho yanasababishwa na umri unapoenda ndipo
watu wengi wanapata matatizo hayo, hivyo unapofikisha miaka 40 walau uende
hospitali kuchunguza uwezo wako wa kuona. Pia watoto wengi wanazaliwa na mtoto
wa jicho kutokana na maambukizi ya mama, magonjwa ya kurithi na kisukari".
Ameongeza kuwa, baada ya kliniki ya Bugando upande wa macho kuboreshwa wamekuwa na
uwezo wa kuhudumia wagonjwa takribani 100 kwa siku, 500 kwa wiki na 2,400 mpaka
2,600 kwa mwezi na visababishi vikubwa vya magonjwa ya macho ni umri, mazingira
yanapelekea kupata mzio kwenye macho, kurithi upande wa watoto wadogo, kisukari
na presha.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Hospitali ya Rufaa ya Bugando Dk Fabian Masaga amewataka wazazi
kuwaruhusu watoto wadogo kushiriki michezo ya nje ili kuwapa nafasi ya kuona mbali na siyo karibu
peke yake pamoja na kuwavalisha miwani ya kukinga miale ya jua pindi jua
linapokuwa kali wakati wa matembezi ya mchana.
Dk Fabian Masaga amesema hospitali ya Bugando inafanya jitihada kuhakikisha hakuna mwananchi anayepoteza uoni kwa changamoto za macho kwa kuboresha miundombinu, kutoa huduma za kibingwa katika hospitali za wilaya na mikoa, kutoa huduma za upasuaji kwa gharama nafuu na vipimo vya bure.
Naye mmoja wa wagonjwa aliyefika hospitalini hapo Suzana Steven akiwa ameambatana na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano ili kupata huduma ya uchunguzi wa macho, amewashauri wazazi na walezi kuwa utaratibu wa kufanya uchunguzi wa macho mara kwa mara ili kubaini matatizo ya macho angali mapema.
"Nimesumbuliwa na tatizo la uoni hafifu kwa miaka mitatu sasa, baada ya kufanya kazi
ya katibu muhtasi muda mwingi nilitumia kompyuta ambapo imenipelekea kupata taitizo la uoni hafifu.Nae na mtoto wangu baada ya vipimo amegundulika kuwa na tatizo kama langu ambalo kwake limesababishwa na kuchezea simu kwa muda mrefu pamoja na kuangalia runinga kwa muda mrefu".alisema Suzana.
Dkt Masaga amehitimisha kwa kusema wazazi na walimu wanaweza kugundua kama mtoto ana ugonjwa wa macho kwa kuangalia dalili zifuatazo; mtoto kama anafinya macho akiwa anasoma, anasogeza kitabu usoni wakati wa kusoma, akiwa anaangalia runinga anaisogelea na watoto wengine hufikicha macho sana, hizo ni dalili za awali na ukiziona kama mzazi au mlezi mpeleke mtoto hospitali kwa uchunguzi mara moja.
No comments