WANANCHI SHIBULA WATAANZA KUONA MABADILIKO WIKI HII
Na Mwandishi wetu, Mwanza.
Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza(MWAUWASA) inaendelea na maboresho katika maeneo ya Kata ya Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza hivyo wananchi wanaopata huduma ya maji kutoka chanzo cha maji Igombe wataanza kuona mabadiliko ndani ya wiki hii.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Neli Msuya wakati alipoongozana na wataalam wa mamlaka hiyo ambayo ilikutana na viongozi wa mitaa 14 wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Shibula Swila Dede ili kujadili namna ya kuboresha hali ya upatikanaji maji katika kata hiyo.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ya Kata ya Shibula, MWAUWASA imeainisha mipango iliyopo katika kutatua changamoto zinazoikabili mitaa hiyo pamoja na kujibu hoja zilizoibuliwa na viongozi hao.
Msuya amesema MWAUWASA inaendelea na maboresho katika eneo hilo hivyo wananchi wenye mtandao wa maji kutoka chanzo cha maji Igombe wataanza kuona mabadiliko ndani ya wiki hii
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo ina timu ya wataalam ambao wanafanya kazi kuhakikisha hali ya maji katika eneo la kihuduma la MWAUWASA inaimarika na kuwanufaisha wananchi
"Timu hii itafika hapa na kusaidiana na wenyeviti wa mitaa husika kufanya tahthmini pamoja na kupata suluhisho, niombe ushirikiano pindi timu hii ya wataalam itakapokuwa katika mitaa yenu," ameeleza
Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Robert Lupoja amesema mipango inayoendelea ni kuboresha chanzo cha maji Igombe pamoja na kuongeza ukubwa wa bomba la usambazaji kutoka inchi 6 hadi inchi 10.
"Mradi huu unaotekelezwa kwa sasa, utahusisha ujenzi wa magati 10 katika mitaa inayopatikana Kata ya Shibula, tunajadili kuongeza idadi ya magati,tunaboresha miundombinu ya maji ili kupokea ongezeko la maji pindi mradi wa maji Butimba utakavyoanza kufanya kazi moja kwa moja,".
Amesema kuwa MWAUWASA iko kwenye mpango wa kuweka mtandao na mfumo wa maji ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa maeneo ya pembezoni na tayari shughuli za ulazaji wa mabomba zinaendelea.
Diwani wa kata ya Shibula Swila Dede ameishukuru MWAUWASA kwa kufika na kuzungumza na viongozi wa mitaa ndani ya kata ya Shibula na kuiomba kuharakisha utekelezaji wa miradi ndani ya muda uliopangwa ili kuleta tija kwa wananchi.
No comments