Breaking News

WADAU WATAKIWA KUFIKISHA ELIMU YA MALEZI KWA JAMII BILA KUJALI CHANGAMOTO YA BAJETI

NA HADIJA OMARY,LINDI 

Mtaani kwetu kuna watoto kadhaa wa umri chini ya miaka 8. Nimezungumza na majirani wawili na kubaini hawajawahi kueleweshwa kiundani umuhimu wa kuwekeza kwa watoto wao kupitia mbinu za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  (MMMAM).

Wazazi walioelewa masuala ya MMMAM ni wengi ndio maana Watendaji kutoka katika idara mtambuka zinazoguswa na  utekelezaji wa Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto PJT-MMMAM wametakiwa kushirikiana kwa pamoja bila kujali changamoto za bajeti kufikisha Elimu ya malezi kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi, Consolatha Katengesya, alipokuwa anazungumza na wadau katika kikao cha uhamasishaji wa shughuli za MMMAM ngazi ya Halmashauri kilichohusisha wajumbe wa kamati ya uongozi CMT , viongozi wa asasi za kiraia pamoja na viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu .



Akizungumza katika kikao hicho amesema bila kujali ufinyu wa Bajeti katika utekelezaji wa programu hiyo, kila mdau anaeguswa  moja kwa moja, anao wajibu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kulingana na eneo lake la kufanyia kazi.

" Tuanafahamu mara zote rasilimali pesa inakuwa haitoshi na tukiendekeza uchache huo wa bajeti hatutaweza kufanya vitu vingi. Sasa kama ilivyokuwa programu jumuishi, ina maana kila mmoja anajukumu anapokwenda katika shughuli zake basi atoe hii elimu ya makuzi katika sehemu husika"

" Mfano watu wa TASAF wanapokwenda kutoa hela pale, kuna wamama na kunakuwa na wababa pia basi ni jukumu letu kuwakumbusha pale swala zima la malezi na makuzi. Hii iwe hivyo hivyo hata kwa watu wa Afya, mna kliniki pale kila siku ya akina mama, unachukua dakika chache kuzungumzia swala hili na hata idara zingine pia nazo hivyo hivyo hii itatusaidia kufikisha ujumbe huu kwa jamii kwa urahisi zaidi"

Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Lindi Charles Kigahe  amesema program hiyo jumuishi ya kitaifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto PJT-MMMAM inalenga kujibu changamoto za mahitaji kwa watoto wadogo, ukizingatia ulimwengu mzima una watoto takribani milioni 250 wenye umri  chini ya miaka mitano ambao wanapatikana kwenye nchi zenye uchumi wa chini na zile zenye uchumi wa kati ambao wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua zao za ukuwaji.

Kigahe amesema Takribani theluthi  mbili sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano  walio nchi za kusini mwa jangwa la sahara wapo katika hatari  ya kutofikia  hatua timilifu  za ukuwaji kutokana na kukosa malezi bora , umasikini, utapia mlo pamoja na matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi.

Amesema hata hivyo kumekuwa na hatua na jitihada mbali mbali za kiulimwengu katika kushughulikia maswala ya MMMAM kwa kuwepo kwa mifumo na miongozo  kadhaa ikiwa imelenga  kusaidia utekelezaji wa kina wa shughuli za  mpango huo na hatimae kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Dunia.

" Miongoni mwa mifumo iliyoandaliwa  ni mfumo wa malezi jumuishi uliozinduliwa na shirika la afya Duniani mwaka 2018 ambao una maono kuwa na Dunia ambayo mtoto anaweza kufikia hatua zake za ukuwaji timilifu na hakuna mtoto atakaeachwa nyuma " alieleza Kigahe. 

Awali mwezeshaji wa kikao hicho Nelson Choaji, mjumbe wa kamati ya uhamasishaji wa mpango wa PJT-MMMAM Mkoa wa Lindi afisa kutoka shirika la utetezi wa wanawake Lindi (LIWOPAC), amesema wadau wanapaswa kufahamu kipindi  cha uwekezaji kwa mtoto ni kipindi cha mwaka 0-8  kutokana na unyeti wake

"Katika kipindi hiki uwekezaji mkubwa upaswa kufanyika katika nyanya zote, hususan afya ya mama kuanzia mama anapokuwa mjamzito mpaka mtoto anapozaliwa, lishe , ulinzi na usalama, ujifunzaji wa awali na hata malezi yenye muitikio, haya yote yana maana kubwa sana katika makuzi ya mtoto" alisema Choaji.

Amesema katika kipindi cha mwaka 0-8 ubongo wa mtoto unakuwa umesha kua kwa asilimia 75 huku asilimia 25 zinazobaki zikiwa zinaongezeka kadri umri unavyozidi kwenda ambapo katika kipindi hiko mtoto uweza kufahamu vitu vingi na kwa haraka zaidi.

" Kwa sasa bila kutambua, wazazi walio wengi mfano kwenye maswala ya Elimu,  wanaanza kuwekeza pindi mtoto anapomaliza Darasa la saba, ndipo anapoona umuhimu wa kumtafutia masomo hata ya ziada kwa ajili ya kuanza kidato cha kwanza, wakati alitakiwa uwekezaji huo aufanye akiwa bado mtoto huku kwenye Elimu ya Awali"

Nae afisa lishe wa halmashauri ya Liwale Abas Ally alisema  idara yao imejipanga kufikisha Elimu hiyo ya malezi na makuzi kupitia shughuli mbalimbali kama vile siku ya Afya na lishe.

" Kuna kitu kwetu sisi upande wa lishe nimekiona ni muhimu sana hasa tunapokutana na jamii kwa kuwa sasa  tuna kitu kinaitwa siku ya afya na lishe ya kijiji ambapo sehemu kubwa tunatoa Elimu ya lishe , tunapima hali ya lishe kwa watoto pamoja na kufanya mfano wa vyakula mbali mbali hivyo kupitia siku hiyo tutaunganisha na utoaji wa Elimu juu ya umuhimu wa malezi na makuzi kwani ni muhimu pia katika ukuwaji wa mtoto"

Kwa upande wake Brighter Kambona, Mkurugenzi wa Brighter Foundation alisema programu hiyo jumuishi ya kitaifa ya MMMAM ni nzuri na kwamba kama itatekelezwa kama ilivyokusudiwa itawasaidia kwa kiasi kikubwa watoto wa Tanzania kukua katika utimilifu wao.

Alisema ni vizuri pia kuendelea kutoa Elimu ya uhamasishaji wa mpango huo kwa asasi za kiraia mara kwa mara kwani kwa kiasi kikubwa wanakuwa wakitekeleza majukumu yao na jamii kubwa hasa kwa maeneo ya vijijini ambako uwenda Elimu hiyo isiweze kufika kwa urahisi

" Kuhusu halmashauri kuendelea kutupatia elimu kama hizi sisi asasi za kiraia ili kusudi sisi tukawe vipeperushi kwa watu wengine pia ningeomba kutoa msisitizo kwenye hili ni muhimu kwa sababu tuliopo hapa ni wachache na hiki tulichokipata tumekipata kwa muda mfupi japo ni kizuri tunaomba mlichuku hili muone namna ya kutukutanisha wengi zaidi na kutupatia Elimu hii" alisema Kambona.

Program jumuishi ya kitaifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto  inatekelezwa kwa miaka 5 kuanzia  2021/2022 hadi 2025/2026 ikiwa imelenga kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya mwanadamu kwa kukuza malezi jumuishi yenye tija kiuchumi kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali kutoa malezi jumuishi kwa kuzingatia vipengele vitano . 

Vitu hivyo ni Afya bora kwa watoto na male, lishe ya kutosho toka ujauzito,  malezi yenye muitikio,  fulsa za ujifunzaji wa awali  pamoja na ulinzi na usalama kwa watoto.

No comments