Breaking News

SERIKALI YAOMBWA KUINGIZA KWENYE KATIBA HAKI YA KILA MTOTO KUPEWA BIMA YA AFYA

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Serikali imeombwa kuingiza kwenye katiba haki ya kila mtoto anayezaliwa hapa nchini kupewa bima ya afya kwa ustawi wa mtoto na taifa kwa ujumla.

Wadau kutoka mashirika mbalimbali yanayotekeleza afua za wanawake na watoto wameyasema hayo kwa nyakati tofauti mara baada ya kugundua kuwa huduma za afya kwa watoto zimeporomoka tangu kutondolewa kwa bima afya ya toto kadi.

Sophia Donald mkurugenzi wa shirika la Sauti Ya Mwanamke Ukerewe ameyaomba mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuungana kwa pamoja ili kutatua changamoto ya bima ya afya kwa watoto na walemavu.

Sophia Donald mkurugenzi wa shirika la Sauti Ya Mwanamke Ukerewe akitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa watoto hoja iliyoibuka katika Uzinduzi wa Mradi wa Uraia Wetu unaotekelezwa na Shirika la NELICO.

“Kuondolewa kwa toto bima kadi  kiukweli imekuwa kikwazo na ina athiri afya ya watoto kwasababu tayari tumekiuka upatikanaji wa huduma bora na rafiki kwa watoto”.alisema Sophia.

Kwa kuliona tatizo hilo Doreen Mayani mratibu mradi kutoka Child Support Tanzania amesema wao wanatoa huduma kwa watoto wenye ulemavu ambao wanachangamoto nyingi upande wa matibabu kama vile kuugua kila siku,kuhitaji matibabu ya viungo ambapo wengi wao inakuwa  sio rahisi kumudu gharama za matibabu.

Doreen Mayani mratibu mradi kutoka Child Support Tanzania akitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa watoto hoja iliyoibuka katika Uzinduzi wa Mradi wa Uraia Wetu unaotekelezwa na Shirika la NELICO.

Sisi kama taasisi tumesaidia watoto kupata bima ya afya mwaka jana tulitoa bima 130 kwa watoto na mwaka huu pia tumetoa bima 130 kwa watoto ambazo matokeo yake ni makubwa kwa watoto wenye ulemavu.

Doreen amesema Ili kuhakikisha watoto wanapata bima za afya wamekuwa wakiwahamasisha wazazi na walezi kukata bima kupitia kwenye taasisi au vikundi ili waweze kupata bima za afya kwaajili ya watoto.

Kwa upande wake meneja Uhasiano wa shirika la New Light Children Centre Organization (NALICO) Kwaresma Mgige  amesema jambo ambalo linaweza kufanywa na Azaki  zote ni  kusimamia suala la bima ya afya kwa mtoto liwe ni lazima kwa kila mtoto anayezaliwa kupatiwa bima ya afya.


Meneja Uhasiano wa shirika la New Light Children Centre Organization (NALICO) Kwaresma Mgige akitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa watoto hoja iliyoibuka katika Uzinduzi wa Mradi wa Uraia Wetu 

“Tukiweza kulichagiza hili na likaingia kwenye katiba au likatambuliwa kisheria  tutakuwa tumewasaidia watoto na tukiweza kulisimamia na likafanikiwa hili basi tutakuwa tumewaokoa watoto wote  wa Tanzania hasa wale wanatoka katika familia masikini”.alisema Qurezima.

Nae Atanasi Evaristi kutoka Azaki ya Fadhili Teens Tanzania ameitaka serikali kuondoa masharti iliyoweka kwa taasisi zenye nia ya kuwakatia bima watoto kwakuwa mashariti hayo yamekuwa yakiwasababisha washindwe kuwakatia bima watoto hao licha ya bajeti kuwepo.

Atanasi Evaristi kutoka Azaki ya Fadhili Teens Tanzania kitoa mchango wake kuhusu umuhimu wa bima ya afya kwa watoto hoja iliyoibuka katika Uzinduzi wa Mradi wa Uraia Wetu 

Kupitia waziri wa afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu alisema alipokuwa bungeni kuwa bima ya afya ndio roho yahuduma za afya hapa nchini ambapo asilimia 70 ya fedha za hospitali za serikali na binafsi zinategemea bima ya afya.


Serikali imesema baada ya kufanya uchambuzi waligundua kuwa baadhi ya vifurushi vinahatarisha uhai na uendelevu wa mfuko wa taifa wa bima ya afya ikiwemo toto afya kadi ambapo matumizi yao yamekuwa makubwa kuliko michango yao hivyo kuleta hasara kwenye mfuko bima ya taifa.

“Watoto wanachangia shilingi 54000,katika kila shilingi 100 watatumia shilingi 667 lakini la pili kwa mwaka 2020- 2021 watoto waliosajiliwa toto afya kadi walikuwa  157920 wakachangia bilioni 5.9 na kutumia bilioni 40.5 hii ni hasara”.alisema Ummy

Ummy alihitimisha kwa kuagiza watoto wasajiliwe shuleni au watoto wasajiliwe pamoja na wazazi wao ili kuwepo kwa uendelevu wa bima akitolea mfano watoto watakaposajiliwa shuleni itakuwa rahisi  wao kwa wao kuchangiana kwenye  matibabu.

No comments