RC MAKALLA AWAONGOZA MASHABIKI WA SOKA MWANZA, PAMBA JIJI FC IKIKATA UTEPE KWA USHINDI MNONO
Na Mwandishi wetu, Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla leo amewaongoza mashabiki wa soka uwanjani Nyamagana wakiishuhudia timu ya soka Pamba Jiji FC ikikata utepe wa michuano ya Championship kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Cosmo politan
Mhe.Makalla ambaye ni mlezi wa Pamba Jiji FC alionekana jukwaani muda wote akiwa mwenye furaha kutokana na kandanda la kitabuni lililosakatwa na vijana wake muda wote wa mchezo na kuchagiza ushindi huo.
Katika mpambano huo wana TP LINDANDA wakiwa na wachezaji waliotamba Ligi kuu msimu uliopita akiwemo Haruna Chanongo, Peter Mwalyanzi na Shaaban Kado hadi ngwe ya kwanza inamalizika walikuwa wanaongoza mabao 3-0 kabla ya ngwe ya pili kuongeza bao la nne.
Mara baada ya mchezo huo kocha wa timu ya Pamba Jiji Mbwana Makatta amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo na kuahidi kuzifanyia kazi baadhi ya kasoro za kiufundi ikiwemo umaliziaji na wachezaji kuongeza kasi dimbani.
Kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya msimu huu mlezi wa Pamba Jiji FC CPA. Amos Makalla amewataka wananchi wa Mwanza kuiunga mkono timu hiyo hasa kujitokeza uwanjani na kuichangia kwa hali na mali kwa lengo la kuwaongezea ari wachezaji, huku timu hiyo ikiwa tayari chini ya umiliki wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Kwa ushindi huo wana TP Lindanda wanaongoza kwenye msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na mtaji wa pointi 3 na mabao ya kufunga manne kabla ya kushuka tena dimbani Ijumaa hii kumenyana na Pan African kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana.
No comments