Breaking News

OUT CHIMBUKO LA WAHITIMU BORA


Asilimia kubwa ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), wana uwezo mkubwa wa kuchanganua na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili jamii yetu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala, Mhe. George Simbachawene, alipokuwa akizungumza na wahitimu (Alumni) wa chuo hiki wakati wa mkusanyiko wa pili wa jumuiya ya wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, uliofanyika Septemba 21, 2023, katika kituo cha mkoa wa Dodoma, jijini Dodoma.

“Uzuri wa aliyesoma chuo Kikuu Huria cha Tanzania huwezi kumfananisha na mtu mwingine yeyote sababu huku anafundishwa kujitegemea kwa kutafuta mahitaji yote yampasayo kusoma, mazingira hayo ndio anayokutana nayo kazini. Hivyo wanatengenezwa wahitimu ambao ni viongozi imara.” Amesisitiza Mhe.Simbachawene.

Aidha, ameongeza kuwa, chuo hiki ndiyo chuo pekee ambacho unaweza kujiendeleza huku unaendelea na kazi na shughuli zako. Mhe. Simbachawene alisoma shahada ya sheria ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kuhitimu kwa miaka Mitatu. Shahada hiyo ilimwezesha kufunzu mtihani wa uwakili na kuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Mhe. Simbachawene ametoa rai na ushauri kwa Watanzania wote kukitumia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kujiendeleza kielimu na huku wanaendelea na kazi zao bila kuziacha.

"Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni mkombozi kwa watu ambao wamekosa fursa ya kupata elimu ya juu kwa sababu ya changamoto mbalimbali ikiwemo kubanwa na majukumu ya kazi. Mimi nilikuwa nafanya shughuli zangu huku najiendeleza kielimu kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na nikahitimu vizuri." Ameongeza Mhe. Simbachawene.

Naye Mbunge wa Singida mjini na Rais mpya wa jumuiya ya Wahitimu wa chuo hiki Mhe. Mussa Sima, ametoa rai kwa wahitimu wenzie kushikamana vyema na chuo chao katika kuchangia maboresho mbalimbali kwani kimekuwa ni msaada mkubwa kwa Watanzania hasa wale waliopo kwenye ajira tayari hususani watumishi wa umma.

“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimetusaidia sana. Mtumishi aliyepo kazini badala ya kuacha kazi na kwenda kusoma, sasa ana nafasi ya kupata elimu ya chuo kikuu na bado anaendelea na majukumu ya kazi yake. Hii inamsaidia kuongeza ujuzi na kukua katika ajira kiutumishi.” Amesema Mhe. Sima.

Rais wa Jumiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Almas Maige ambaye pia ni mbunge wa Tabora Kaskazini, amesema ni wajibu kwa kila muhitimu kushiriki katika chama cha wahitimu ili kushiriki katika kutoa mchango wao wa kimawazo, kiuchumi, kijamii, utafiti na huduma za kitaalam.

“Wahitimu tukishirikiana vyema na chuo tutaweza kuwa sehemu ya majawabu ya baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo chetu na wanafunzi wanaohitimu katika vyuo ndiyo chachu na mbegu bora ya maendeleo ya chuo chochote duniani.” Amesema Mhe. Maige.

Kwa upande wake Makamu Mkuu kuu wa Chuo, Prof. Elifas Bisanda, amesema tangu chuo hiki kimeanza kuhitimisha mwaka 1999 hatujawahi kuwatumia wahitimu wetu, lakini ukweli ni kwamba Jumuiya ya wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni wadau muhimu sana kwa maendeleo ya chuo chetu katika Nyanja mbalimbali.

“Tunawahitaji wafanye kazi ya kutangaza huduma zetu kwa jamii, tunawahitaji kwa kupata taarifa za maendeleo ya elimu yao baada ya kuhitimu ili tuweze kuimarisha mitaala yetu lakini pia tunawahitaji wahitimu wetu katika maswala ya harambee ili kufanikisha maendeleo ya miradi mbalimbali ya chuo katika kutoa huduma zake.” Alimaliza kusema Prof. Bisanda.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Prof. Alex Makulilo, amevutiwa sana na shuhuda mbalimbali kutoka kwa Wahitimu kitu kinachoonesha kwamba chuo kinapiga hatua kubwa sana katika kuzalisha wataalamu wabobezi na wenye ujuzi wa kutosha wa kuwahudumia Watanzania. Akitoa neno la shukurani, amemshukuru mgeni rasmi na wahitimu wote kwa kupokea mwaliko na kuhudhuria kwenye shughuli hii bila kukosa licha ya kuwa na majukumu mengi ya ujenzi wa taifa na kimataifa.

"Tumeona katika kusanyiko hili kuna wahitimu wa chuo chetu kutoka mataifa mbalimbali wamehudhuria jambo linalothibitisha kwamba hiki ni chuo cha kimataifa. Wahitimu ni nguzo muhimu katika kuongeza udahili wa chuo na tunawaomba muendelee kufanya kazi kwa bidii huko mlipo na kutoa huduma bora kwa wananchi ili watu wavutiwe kujiunga na chuo chetu ndani na nje ya nchi." Amesema Prof. Makulilo.

Akifunga kusanyiko hilo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Fedha, Mipango na utawala, Prof. George Oreku, amemhakikishia mgeni rasmi kuwa Menejimenti na wafanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wataendelea kushirikiana na Alumni katika kuongeza ubunifu na kujituma katika kazi ili kuleta matokeo chanya.

Prof. Oreku, amevutiwa na wazo la kufunguwa akaunti maalumu kwa ajili ya wahitimu kuchangia maendeleo ya chuo na uhai wa jumuiya hiyo ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Amesema jambo hili ni zuri sana na Viongozi wetu akiwemo mgeni rasmi, rais mpya wa jumuiya na rais aliyemaliza muda wake waliahidi kila mmoja kuchanga shilingi milioni moja kwa mwaka.

"Wazo la kuanzisha akaunti maalumu ya jumuiya ya Wahitimu wa chuo hiki limekuja wakati muafaka na ni ishara kwamba jumuiya hii ina dhamira ya dhati ya kutaka kushirikiana na Menejimenti ya chuo katika kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake ikiwa ni kutoa elimu bora na nafuu kwa watu wote wakiwa mahali popote wakiendelea na kazi zao za ujenzi wa taifa. Tunasema asante sana kwenu wahitimu wote kwa moyo wenu na nia yenu ya dhati ya kushirikiana na chuo chetu." Alihitimisha Prof. Oreku.

No comments