MTANDAO WA MAJI WA KILOMETA 24 KULAZWA BUSWELU, NYAMADOKE NA KAHAMA
Na Mwandishi wetu Mwanza.
Katika kuhakikisha huduma ya maji Jijini Mwanza inaimarika, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imepokea shehena ya mabomba ya gharama ya bilioni 2.4 kwa ajili ya maeneo ya Buswelu, Nyamadoke na Kahama.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya shehena hiyo ya mabomba Septemba 12, 2023, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Ndugu Neli Msuya amesema MWAUWASA inatekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo inayohudumia ili kuwapunguzia adha wananchi sambamba na kufikia azma ya Serikali ya kumtua Mama ndoo ya maji kichwani.
"Hii ni shehena ya kwanza na tunatarajia siku mbili zijazo tutapokea shehena nyingine kwa ajili ya maeneo ya Luchelele, Ilalila na Kisesa," amesema Ndugu Neli.
Ndugu Neli ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maji kwa jitihada zake za makusudi za kuimarisha huduma ya maji Mwanza.
"Tunaishukuru Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri wetu wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso kwa kujitoa kwa ajili ya wananchi wa Mwanza, kuhakikisha wana Mwanza wanapata huduma ya majisafi na salama," amesema Ndugu Neli.
Amefafanua kuwa tarehe 15 Septemba, 2023 MWAUWASA itafanya majaribio ya awali ya mradi wa Butimba. "Tunaanza majaribio ya awali ya mradi wa Butimba na hivyo tutakuwa na ongezeko la maji kutoka Butimba kadri mradi unavyoendelea kukamilika," amesema Ndugu Neli.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Buswelu, Mhe. Sarah Ng'wani ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma ya maji Jijini Mwanza.
Vilevile amewasihi wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji.
"Tunawasihi wananchi watambue kwamba miradi hii imeletwa na Serikali kwa gharama kubwa kwa ajili yao hivyo wanakila sababu ya kuhakikisha inatunzwa," amesisitiza.
No comments