Breaking News

BARRICK YAPONGEZWA KWA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA SERIKALI ZA KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA



Wananchi wakitembelea banda la Barrick katika maonesho ya maadhimisho ya siku ya Mara.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, (wa pili kushoto) na ujumbe wake wakipata maelezo jinsi kampuni ya Barrick inavyoweka mkazo katika utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji kutoka kwa Afisa Mazingira wa Barrick North Mara,Samwel Ingram walipotembelea banda ya kampuni hiyo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika viwanja vya Sokoine wilayani Serengeti
Viongozi mbalimbali na Wananchi walipata fursa ya kutembelea banda ya Barrick katika maonesho ya kuadhimisha siku ya Mara.
Viongozi mbalimbali na Wananchi walipata fursa ya kutembelea banda ya Barrick katika maonesho ya kuadhimisha siku ya Mara.
Burudani mbalimbali zilikuwepo wakati wa maonesho hayo

***
NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuiunga mkono Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla katika uboreshaji huduma ya maji kwa wananchi, kutunza mazingira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mhandisi Mahudi ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la Barrick wakati wa kilele cha Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mara yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine uliopo mjini Mugumu katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.


“Hongereni sana Barrick kwa shughuli mnazofanya kusaidiana na Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla katika uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi, lakini pia utunzaji wa mazingira na kuinua uchumi wa nchi yetu,” alisema.


Kampuni ya Barrick imeshiriki maadhimisho hayo kupitia Mgodi wake wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Mhandisi Mahundi ameihimiza pia Barrick North Mara, kuendelea kuhakikisha shughuli zake za uchimbaji madini hazisababishi uchafuzi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla katika jamii inayozunguka mgodi huo.

Awali, Afisa Mazingira wa Mgodi wa Barrick North Mara, Samwel Ingram alimweleza Naibu Waziri Mahundi kuwa shughuli za mgodi huo zinafanyika katika eneo lililo ndani ya Bonde la Mto Mara, hivyo wanawajibika kulinda usalama wa vyanzo vya maji na mazingira yanayouzunguka.


Kuhusu huduma ya maji, Ingram alisema wanazingatia viwango vinavyokubalika kisheria katika kuchukua maji ya Mto Mara na kuyatibu kwa ajili ya matumizi ya ndani ya mgodi na kuyasambaza kwa wananchi wa vijiji vinavyopakana nao.


“Kwa upande mwingine, Barrick North Mara tunashirikiana na Serikali kupitia mamlaka husika zikiwemo Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijiji (RUWASA) na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) kuboresha huduma ya maji na utunzaji wa mazingira.

“Pia tunashiriki kwa vitendo kuiunga mkono Serikali katika juhudi za upandaji wa miti ili kutunza mazingira, sambamba na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na mazingira,” amesema Afisa Mazingira huyo wa Barrick North Mara.


Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara hufanyika Septemba 15 kila mwaka, ambapo nchi za Tanzania na Kenya zinazoshirikiana kuyaadhimisha hupokezana kuyaandaa kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na utunzaji endelevu wa Mto Mara ambao unatiririsha maji katika Ziwa Victoria.


Kauli mbiu ya Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mara mwaka huu wa 2023 inasema “Hifadhi Mto Mara kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi endelevu”.

No comments