MTOTO ANATAKIWA KULINDWA NA KUONYESHWA UPENDO TANGU AKIWA TUMBONI
Na Tonny Alphonce,Mwanza
Kina mama
wajawazito na jamii kwa jumla wametakiwa kuwekeza zaidi kipindi cha ujauzito
kwa kuwa katika kipindi hicho mama amebeba mtoto ambaye anatakiwa kuanza
kujengewa misingi ya maisha kuanzia akiwa na mwaka sifuri.
Kauli hiyo
imetolewa na Sister Denise Mattle katika
warsha ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto iliyoandaliwa na
Montessori Hubb ikiwa na lengo la kujadili mambo mtambuka yanayohusu
malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto pamoja na chngamoto za malezi
katika zama hizi za utandawazi.
Akiwasilisha
mada ya malezi sister Denise amesema bado kuna makosa mengi yanayofanywa na
walezi kuanzia mama anapokuwa mjamzito ambapo familia nyingine huanza
kumshambulia mama kwa maneno makali ambayo humuumiza mama na mtoto kwa ujumla.
“Mtoto akiwa
tumboni huwasiliana na mama kupitia neva kwa maana hiyo mama akiwa na huzuni na
mtoto pia hupata huzuni na hata baada ya kuzaliwa kama baba au mama akiwa mkali
kwa mtoto basi mtoto huathirika moja kwa moja na ndio maana tunawataka wazazi wajitahidi
kuongea na watoto kwa lugha rafiki kwa kuwa mtoto katika umri wa 0-6 au 0 – 7
hujifunza kwa kusikia au kushika na akihitaji kitu huanza kulia kama ishara ya
kuomba”.alisema Sister Denise.
Kwa upande
wake Matesha Sembuche akizungumzia Elimu ya Awali ya Montessori amesema wao
katika hatua za ujifunzaji za awali za mtoto wanafundisha watoto kwa vitendo
kwa kutumia vifaa ambavyo huviona nyumbani ambapo humjenga katika kuanza
kuandika na kusoma.
"Watoto tunawapa maumbo ya vitu mbalimbali,tunawapa chupa za maji wafungue,tunawapa chupa ya chai wafungue pamoja na mambo mengine na kila kitendo huwa na maana kubwa kwa kwa mtoto kwa mfano kufungua chupa mtoto anatumia vidole vitatu ambavyo atakuja kuvitumia katika kuandika kwa maana hiyo wale ambao husema ooh Montessori watoto hawasomi wanacheza tu wanakosea sana".alisema Matesha.
Amesema
kupitia vifaa walivyonavyo vyenyewe vimelenga kuimarisha milango mitano ya
fahamu ya mtoto ili kuanzia mapema mtoto aweze kutofautisha mambo ikiwemo
harufu,ladha na mambo mengine ambayo huamuliwa na milango ya fahamu.
Naye afisa
ustawi wa jamii kutoka wilaya ya Ilemela Pamela Javi amewataka walimu na wazazi
kushirikiana katika malezi ya mtoto ili kumlinda mtoto na vitendo vya kikatili
ambavyo vinaweza kufanywa nyumbani au shuleni.
"Wazazi na
walimu naomba niwaambie utafiti uliofanywa na UNICEF unaonyesha asilimia 60 ya
vitendo vya kikatili kwa mtoto hufanyika nyumbani na asilimia 40 ya vitendo vya
kikatili pia hufanyika shuleni kwa maana hiyo sisi wote hapa lazima tutafakari
tujue namna gani tutamlinda mtoto popote anapokuwa"s.alisema Pamela
Pamela
amesema mtoto anapofanyiwa ukatili humsababishia maumivu ya muda mfupi na muda
mrefu na ndio maana kuna watoto walifanyiwa ukatili utotoni na wao baada ya
kukua wanatafuta namna ya kulipiza walichofanyiwa na hivyo kusababisha vitendo
vya kikatili kuendelea kutokea katika jamii.
Michael
Sungusia meneja miradi kutoka Montessori amesema kwa miaka 26 sasa Montessori
Community of Tanzania imekuwa ikiendesha mbinu za ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kusaidia
ukuaji wa mtoto kwa manufaa ya taifa na
kwa hivi sasa wanaungana na serikali katika kutekeleza Program Jumuishi ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya wali ya
mtoto kwa kuweka katika uhimizaji na ukuzaji
wa malezi jumuishi yenye tija kwa taifa kwa kuzingatia vipengele vya Afya bora ,Lishe
tosherevu,Ulizi na Usalama ,Malezi yenye mwitikio chanya pamoja na Fursa za
ujifunzaji wa awali.
No comments