Breaking News

LUGHA ZA UNYANYAPAA CHANZO CHA MAAMBUKIZI YA VVU

 

Na Tonny Alphonce,Mwanza

Chama cha lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (CHALUFAKITA) kimeombwa kushirikiana na vyombo vingine vya kukuza lugha ya Kiswahili hapa nchini kutafuta maneno mbadala yasiyowabagua watu wanaoishi na VVU.

Afisa Tathimini na Ufatiliaji wa Baraza la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA-MWANZA) Bwana Last Mlaki akiwasilisha mada kuhusu Athari ya lugha ya unyanyapaa katika kongamano la sita la CHALUFAKITA liliofanyika mkoani Mwanza.

Kauli hiyo imetolewa na afisa tathimini na ufatiliaji wa Baraza la watu wanaoishi na VVU Bwana Last Mlaki wakati akiwasilisha mada ya athari za matumizi ya lugha ya unyanyapaa katika kongamano la sita la CHALUFAKITA liliofanyika mkoani Mwanza tarehe 9-10/08/2023.

Mlaki amesema ipo sababu ya kushirikishwa watu wanaoishi na VVU katika mijadala,makongamano,michakato na tafiti yanayohusu lugha ya Kiswahili na Fasihi ili kuboresha sera,miongozo na sheria zinazohusu VVU na UKIMWI.

Amesema ipo sababu pia ya kuwa na chombo cha hiyari cha uratibu wa matumizi fasaha ya lugha vikiwemo vyombo vya habari ili kuondoa matumizi ya unyanyapaa katika jamii.

Changamoto ya unyanyapaa katika jamii imekuwa ikichochea maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwasababu hufika wakati mtu aliyenyanyapaliwa huamua kusambaza virusi kwa makusudi.alisema Mlaki

Amesema lugha kama amekanyaga miwaya,ana ngoma,ameathirika ni lugha za unyanyapaa ambazo hazipaswi kutumiwa pale unapomzungumzia mtu anayeishi na VVU na badala yake lugha ya kawaida ya mtu anaishi na VVU inaweza kutumika.

Kwa upande wake Dkt Mussa Hans kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam ambae pia ni kiongozi wa CHALUFAKITA amewata wanahabari kutumia lugha sahihi pale wanapoandika habari zao na pia amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kufanya utafiti na kuangalia maneno gani yanaweza kutumiwa bila kuleta unyanyapaa katika jamii.

Dkt Mussa Hans kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambae pia ni kiongozi wa CHALUFAKITA akichangia mada ya athari za matumizi ya lugha ya unyanyapaa katika kongamano la sita la CHALUFAKITA

Nae Jasmine Kinga kutoka kitengo cha Elimu Singida Manispaa amesema maneno mengine kama muathirika ni vema likaendelea kutumika kwasababu lugha hizi za unyanyapaa zinaweza kusaidia kuwafanya watu waogope kufanya ngono zembe.


Jasmine Kinga kutoka kitengo cha Elimu Singida Manispaa akichangia mada juu ya athari za matumizi ya lugha ya unyanyapaa katika kongamano la sita la CHALUFAKITA.
Akijibu hoja za wachangiaji Mlaki amesema neno ameathirika bado hawashauri neno hili kutumika katika watu wanaoishi na VVU ukimwita kwa jina hilo anajisikia mnyonge wakati watu wanaoishi na VVU siku hizi wanaishi vizuri kama watu wengine ambao hawana VVU.

Kongamano la sita la CHALUFAKITA limefanyika kwa siku mbili hapa mkoani Mwanza ambapo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo mada hii ya athari za matumizi ya lugha ya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU.

No comments