DIASPORA WAOMBWA KUCHANGAMKIA FURSA MBALIMBALI ZA UWEKEZAJI ZA NSSF, ZIKIWEMO ZA NYUMBA NA VIWANJA
Na MWANDISHI WETU
Mkurugenzi
wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Balozi James Bwana, amewaomba Watanzania wanaoishi nje
ya nchi (Diaspora) kuona fursa ya kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa
Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika miradi ya uwekezaji inayotekelezwa na
Mfuko kwenye maeneo mbalimbali nchini.
"Naomba Diaspora wote
kuchangamkia miradi mbalimbali ya NSSF ikiwemo ya nyumba zilizopo
Toangoma, Kijichi na Dungu jijini Dar es Salaam, pamoja na viwanja
vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali ambavyo vinauzwa kwa gharama nafuu,"
amesema Balozi Bwana.
Amesema hayo tarehe 2 Julai, 2023 wakati
alipotembelea banda la NSSF, ambapo ameweza kujionea namna wafanyakazi
wa NSSF wanavyowahudumia kwa weledi wanachama na wananchi wanaotembelea
banda hilo.
Balozi Bwana ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa
Diaspora wote kuitikia wito huo kwa kunufaika na fursa za uwekezaji kwa
kununua nyumba na viwanja vya NSSF ambavyo ni vya uhakika.
Balozi
Bwana amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
ni mdau muhimu wa NSSF, na kwamba wanashirikiana katika masuala
mbalimbali ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na NSSF zinawafikia
Watanzania wote wakiwemo wanaoishi nje ya nchi 'Diaspora'.
"Natumia
fursa hii kuwapongeza NSSF wamekuwa na jukumu hili kwa muda mrefu
wamekuwa na mifumo mbalimbali ya kutoa huduma za Hifadhi ya Jamii kwa
Diaspora, lakini hivi sasa wanakamilisha mifumo mipya ambayo itaongeza
ushiriki zaidi kwa Watanzania waliopo nje ya nchi," amesema Balozi
Bwana.
Amesema pia Mfuko umekuwa ukiendesha miradi mbalimbali ya
uwekezaji, na kwamba tayari wana ushirikiano wa karibu na NSSF ambapo
hivi karibuni wana miradi mikubwa ya uwekezaji na uendelezaji
inayofanyika nchini Kenya ili kuendeleza vitega uchumi vya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lakini nje ya nchi.
Balozi Bwana amesema
uwekezaji wa NSSF hauishii tu katika uwekezaji wa ndani ya nchi, lakini
sasa wanavuka mipaka na kwenda katika maeneo mengine nje ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ili kwenda kukusanya na kuleta faida zaidi kwa
ajili kuwanufaisha wanachama wa NSSF.
"Nitumie fursa hii
kumpongeza kwa dhati Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bwana Masha Mshomba, kwa
kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya ya kuhakikisha Mfuko unaendelea
kusimama," amesema Balozi Bwana.
Aidha, ameipongeza Menejimenti
na Bodi ya NSSF kwa kazi nzuri na miongozo ambayo wamekuwa wakiitoa
katika kuhakikisha malengo makuu ya kuanzishwa kwa Mfuko yanaendelea
kusimamiwa na kutekelezwa. Malengo hayo ni kuandikisha wanachama kutoka
sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na
kulipa mafao.
Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na NSSF, wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Kulia kwa balozi ni Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele.
Mkurugenzi wa Masuala ya Diaspora wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi James Bwana akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NSSF, wakati alipotembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
No comments