BARRICK NORTH MARA YAPONGEZWA KWA KUFANIKISHA MRADI MKUBWA WA MAJI NYAMONGO UNAOHUDUMIA WANAVIJIJI 35,000
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim (kulia) akizindua mradi wa maji Nyangoto. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Dkt Vincent Mashinji.
Akinamama wakipata huduma ya maji kwenye kituo cha kuchotea baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim kuzindua mradi wa maji Nyangoto wilayani Tarime.
****
*Umegharimu shilingi milioni 999 kutoka fedha za CSR
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim, amekagua na kuzindua rasmi mradi mkubwa wa majisafi na salama katika kijiji cha Nyangoto, kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, ambao ujenzi wake umegharimu shilingi takriban milioni 999 za fungu la Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR), zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara .
Utekelezaji wa mradi huo ulisimamiwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, na tayari umeshaanza kusambaza huduma ya majisafi na salama ya bomba kwa maelfu ya wanavijiji.
Akizungumza baada ya kukagua miundombinu na nyaraka zenye taarifa za mradi huo, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alieleza kuridhishwa na utekelezaji wake, akisema umekidhi viwango vya ubora na kuaksi thamani ya fedha (value for money) zilizotumika.
“Baada ya ukaguzi wa kina tuliofanya kwa upande wa nyaraka na miundombinu tumejiridhisha na utekelezaji wa mradi huu. Tuwapongeze ndugu zetu wa Barrick kwa namna ambavyo wametusaidia katika upatikanaji wa mradi huu mkubwa wa maji,” alisema Kaim.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Malando Masheku, mradi huo unasambaza majisafi na salama ya bomba kwenye kaya 3,737 zenye idadi ya watu 34,678 kupitia vituo 21 vya kuchotea maji katika vijiji vya Nyangoto, Mjini Kati, Matongo na Nyabichune - vinavyopakana na mgodi wa North Mara katika kata ya Matongo.
“Chanzo cha fedha za utekelezaji wa mradi huu ni fedha za CSR kutoka Barrick North Mara,” alisema Mhandisi Masheku wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2023.
“Upatikanaji wa uhakika wa huduma ya majisafi na salama huchangia katika kuzuia magonjwa na hivyo kuimarisha afya na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Mhandisi Masheku.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kuzindua mradi wa maji Nyangoto, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Tulinumpoki Mwakalukwa, alisema chanzo cha mradi wa maji Nyangoto kipo ndani ya eneo la mgodi wa Barrick North Mara. ambako maji hutibiwa baada ya kutolewa mto Mara, kabla ya kusukumwa kwa pampu kwenda kwenye tenki lenye uwezo wa kuchukua lita 300,000 kwa wakati mmoja kwa ajili ya kuyasambaza kwa wanavijiji kupitia vituo maalumu vya kuchotea maji.
Mhandisi Mwakalukwa alisema bado RUWASA ina majukumu ya kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu usimamizi, utunzaji na ulinzi wa mradi huo wa maji na miundombinu yake ili uendelee kunufaisha wengi kwa muda mrefu.
Alifafanua kuwa ulinzi wa miundombinu ya maji ni pamoja na wananchi kuepuka kukata mabomba, lakini pia kuwa wazalendo kwa kuchangia bili ya maji ili kuwezesha mradi kuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Alitumia nafasi hiyo pia kuwashukuru viongozi wa Serikali na Barrick North Mara, kwa ushirikiano mzuri wanaoipatia RUWASA katika juhudi za kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi vijijini.
Wakazi wa vijiji vinne vinavyonufaika na mradi wa maji Nyangoto wanasema umewapunguzia kero iliyokuwepo kwa asilimia 85 sasa kila mtu ana uhuru wa kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba, tofauti na zamani ambapo ilikuwa lazima waende kutafuta, au kununua maji kwa wanaoyatembeza kwenye baiskeli kwa gharama kubwa.
No comments