Breaking News

BARRICK NORTH MARA NA SWALA SOLUTIONS YAFANIKISHA UJENZI WA NYUMBA YA WALIMU YA KISASA SHULE YA SEKONDARI YA MATONGO


Viongozi wa kata ya Matongo katika Halmashauri ya wilaya na Tarime wakifurahi pamoja na walimu wa sekondari ya Matongo katika hafla ya kukabidhiwa nyumba ya walimu wa shule hiyo iliyojengwa na kampuni ya ukandarasi katika mgodi wa Barrick North Mara ya Swala Solutions kwa kushirikiana na mgodi huo.wengine pichani ni Kaimu Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Swala Sulutions , Roy Kiprono Kimutai (mwenye miwani) na Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, (wa nne kulia).Hafla hiyo ilifanyika katika Shule ya Sekondari Matongo
Kaimu Meneja Uendeshaji wa kampuni ya Swala Solutions , Roy Kiprono Kimutai (Kushoto) akikabidhi funguo za nyumba ya walimu kwa Diwani wa kata ya Matongo,Godfrey Kegoye na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo,Daud Itembe (mwenye kofia) katika hafla ya kukabidhi nyumba ya walimu katika shule ya sekondari ya Matongo iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Tarime ambayo imejengwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na mgodi wa Barrick wa North mara.
Walimu na viongozi wa kata ya matongo wakifurahi pamoja na wawakilishi wa makampuni Barrick na Swala Solutions katika hafla hiyo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zabron Orege akikabidhi cheti cha shukrani kwa wawakilishi wa Barrick North Mara , Hermence Christopher na Alex Maengo katika hafla hiyo.
Wageni waalikwa wakifuatilia matukio wakati wa hafla hiyo

Tarime: Katika jitihada za kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini,kampuni ya Swala Solutions ambayo ni mzabuni wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, kushirikiana na mgodi huo imekabidhi msaada wa nyumba pacha ya kisasa (two in one) ya walimu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 120 katika Shule ya Sekondari Matongo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa mgodi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.


Hafla ya kukabidhi nyumba hiyo sambamba na uzinduzi wake ilifanyika shuleni hapo jana na kuhudhuriwa na wananchi,Diwani wa kata ya Matongo ,walimu na viongozi wa vitongoji jirani na eneo hilo na Mkurugenzi wa kampuni ya kikandarasi ya Nyamongo Contractors and Mine Company Ltd, Samwel Paul Bageni, ambaye ameipatia shule hiyo msaada wa kompyuta mbili.


Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye, amezishukuru kampuni za Swala Solutions na Barrick, akisema msaada wa nyumba hiyo umeipunguzia shule hiyo changamoto zinazoikabili.


"Tunamshukuru sana wadau wetu wetuwa maendeleo Barrick na Swala. Nyumba hii ni nzuri sana na hata mkandarasi ameitendea haki. Nitoe shukrani nyingi pia kwa mgodi wa Barrick kwa kutusaidia kutatua changamoto na kwenye sekta ya elimu tunaenda vizuri sana," amesema Kegoye ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Ameishukuru pia Serikali ya Kijiji cha Matongo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo wa elimu.


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe, amesema msaada huo ni ishara ya matunda ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Kampuni ya Barrick na jamii inayozunguka mgodi huo.


“Barrick ni mdau mkubwa sana wa maendeleo katika kata ya Matongo, na sioni tabu kusimama na kusema mgodi unafanya vizuri," amesema Itembe huku akitaja miradi mingi ambayo inatekelezwa katika kijiji hicho kwa ufadhili wa mgodi wa Barrick North Mara.


Kwa upande wake Kaimu Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Swala Solutions, Roy Kiprono Kimutai, ameshukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka Barrick North Mara, Serikali ya Kijiji, Kata ya Matongo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika utekelezaji wa mradi huo.


Naye Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher, ameipongeza Kampuni ya Swala Solutions, akisema kitendo walichofanya ni mfano wa kuigwa.“Huu ni ushirikiano mzuri na kwenye vikao vyetu tunahamasisha wakandarasi/ wazabuni kutoa kidogo kwenye sehemu ya faida yao kurudisha kwenye maendeleo ya jamii,” amesema Christopher.


Ameongeza kuwa manufaa ya mgodi wa Barrack North Mara kwa jamii inayouzunguka ni makubwa, ikiwemo kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR).


Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zabron Orege amesema nyumba waliyokabidhiwa imefanya idadi ya nyumba za walimu zilizokamilika shuleni hapo kufikia nne, kila moja ikiwa pacha (two in one).


Mwalimu Orege amesema ujenzi wa nyumba za walimu nyingine mbili unaendelea, na kwamba shule hiyo ina walimu 12 (wanaume tisa na wanawake watatu) na wanafunzi 228.

No comments