Breaking News

KAMATI YA SIASA CCM HALMASHAURI YA SHINYANGA YARIDHISHWA NA KASI YA MIUNDOMBINU YA MAJI SHUWASA

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka katika Halmashauri ya Shinyanga imefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya kusambaza majisafi kwa wananchi wa kata ya Didia pamoja na Tinde.


Katika ziara hiyo walitembelea na kujionea mradi wa ujenzi wa tangi kubwa la ujazo wa lita laki moja za maji lililopo katika kijiji cha Didia lenye uwezo wa kuhudumia wakazi zaidi ya 7000.


Mradi mwingine ambao kamati ya Siasa ilipata kutembelea ni pamoja na mradi wa usambazaji maji kwa wananchi katika kata ya Tinde kutoka katika tangi kubwa la maji lilipo katika kijiji cha Buchama.

Akizungumza mara baada ya kujionea na kukagua maendeleo ya miradi hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ndugu Edward Ngelela, amesema kuwa wao kama viongozi wa chama wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundombinu ya upatikanaji wa maji ikiwa ni moja ya jambo kubwa ambalo lipo katika Ilani ya chama chao la kuhakikisha inafikisha huduma ya majisafi kwa wananchi wote.


Aidha ametoa wito kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) kuhakikisha inakamilisha kwa wakati taratibu zote za uboreshwaji wa miundombinu hiyo ambayo ipo katika hatua za mwisho ili kuweza kufikisha majisafi kwa wananchi


“Niwaombe SHUWASA mhakikishe mnakamilisha mradi huu kwa haraka ili wananchi wetu waweze kupata huduma hii ya majisafi kwani ndio ishara itakayoonyesha kuwa tunafanya kazi na nyie pia mnafanya kazi katika kuwahudumia wananchi maana mnajukumu kubwa katika kuhakikisha mnaitekeleza Ilani kwa vitendo,” amesema Ngelela.


Pia ameongeza kuwa hapo awali Halmashauri ya Shinyanga ilikuwa ikipatiwa huduma ya usambazaji majisafi toka katika Mamlaka ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) lakini kutokana na baadhi ya maeneo ya Halmashauri kuwa na hadhi ya miji ndipo ikakabidhiwa SHUWASA hivyo wao kama viongozi wa chama hawatoacha kushirikiana na Mamlaka katika kuwahudumia wananchi.


Vilevile ameitaka SHUWASA kupitia upya bei za maji kwani inaonekana kuna maeneo kama Didia huduma ya maji kwa unit moja ni bei kubwa tofauti na maeneo mengine.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), CPA Sarah Emmanuel, katika kutoa taarifa ya miradi hiyo ambayo imetembelewa na kamati hiyo amesema SHUWASA inatarajia kuunganisha wananchi na huduma ya maji kupitia miradi hiyo ya Didia na Tinde ili waanze kupata majisafi na kufurahia matunda ya nchi yao.


Hata hivyo amewatoa hofu wananchi wa Didia katika ombi lao la kuomba kupunguzwa kwa bei za maji kwa unit moja kwani tayari SHUWASA imeishachukua hatua kwa kupeleka mapendekezo mapya ya bei za maji EWURA ambao ndio wenye mamlaka ya kuidhinisha na kubadilisha bei za maji.


Pia amewahakikishia wananchi wa kijiji cha Buchama kuwa Mamlaka inajitahidi kuhakikisha inapata fedha za kuwafikishia maji ili waweze kunufaika na huduma hiyo na wasiishie tu kuwa walinzi wa mradi wa tangi hilo bila kunufaika.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ndugu Edward Ngelela akizungumza
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), CPA Sarah Emmanuel akizungumza 

No comments