MKUU WA WILAYA MAKILAGI - WAZAZI WASOMESHENI WATOTO KWA FAIDA YA BAADAE
Na Tonny Alphonce,Mwanza
Wazazi na walezi wa wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wametakiwa kuhakikisha wanawekeza katika elimu kwa watoto wao wakike na wakiume kwa manufaa yao na kwa taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi
wakati akizungumza na wazazi na walezi katika kikao cha kuwapongeza wazazi hao
kwa kuwasomesha watoto wao katika shule hiyo ya Mkuyuni.
Mheshimiwa Makilagi amesema elimu pekee ndio inaweza
kuwasaidia watoto kuwa na waisha mazuri ya baadae lakini pia ustawi wa taifa
unategemea jamii iliyo elimika.
“Mzazi yoyote aliyewekaza katika elimu hawezi kulala njaa na
atakula sasa hadi kufa kwake,elimu ni tofauti na biashara ambazo huanza na kufa
tofauti na waliowekeza kwa Watoto ambao wanaendelea kuishi vizuri hadi sasa”.alisema
Makilagi.
Makilagi amewataka wazazi kuhakikisha watoto wa kike
wanafikia ndoto zao na kuacha tabia ya kuwaozesha wangali wadogo kwa kuwa
katika umri huo hawawezi kuhimili mikimiki ya ndoa.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akiongea na Wazazi na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mkuyuni ya jijini Mwanza.
Amesema baadhi ya sababu zinazochangia watoto wengi
kuharibikiwa maishani ni pamoja na wazazi wote wawili kushindwa kutenga muda wa
kulea watoto tangu wanapokuwa wadogo ili kuwajengea msingi imara utakaowasaidia
maishani mwao.
“Kama kweli tunataka kuwa na kizazi kisichokuwa na kasoro
niwaombe wazazi wenzangu tuwekeze muda mwingi kwa Watoto wetu hii itatusaidia
kujua matamanio yao,matatizo yao na sisi kama wazazi sasa tutakuwa na wajibu wa
kuwasaidia kufikia ndoto zao na hata kutatua changamoto zao”.alisema Makilagi.
Makilagi amesema wazazi wanatakiwa kuwa makini pia kwa watoto
wao wa madarasa ya awali ambao mara nyingi huzua sababu za kutokwenda shule
hali ambayo ikiachwa itasababisha watoto hao kuwa watoro wakubwa kwa siku za
usoni.
“Mtoto anaamka asubuhi anasikia baridi anakuambia mama kichwa
kinauma na mzazi bila kufikiria unamwambia lala lala mwanangu hapo humsaidii
mtoto bali unatengeneza bomu”.alisema Mkilagi.
Amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya elimu kwa
kujenga shule bora na za kisasa kwaa ajili ya kuwapa nafasi ya kusoma watoto
wote wenye sifa ya kupata elimu.
Ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia watoto UNICEF mjini New York Marekani imeonya kuwa zaidi ya watoto
milioni 175, yaani nusu ya watoto wote wanaotakiwa kuwa katika shule za awali
kote duniani, hawasajiliwa katika elimu ya awali au chekechea na hivyo wanakosa
fursa ya uwekezaji muhimu na kukosa usawa kuanzia mwanzo.
No comments