Breaking News

SERIKALI YASHAURIWA KUKUSANYA TAKWIMU ZA AJALI ZA MAJINI,EMEDO YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA OFISI ZA TAKWIMU

 

Na Tonny Alphonce,Musoma

Imeelezwa kuwa ukosekanaji wa elimu na takwimu sahihi za watu wanaofanya shughuli zao ziwani ni sababu moja wapo zinazochangia ongezeko la ajali za majini kutokana na wananchi wengi kutokuwa na taarifa sahihi zinazoweza kuwasaidia kuchukua tahadhari za kujikinga na ajali hizo.

kauli hiyo imetolewa na wadau mbalimbali wa uvuvi wa kata za Kome na Busekela Mkoani Mara wakati wakichangia mada katika kikao cha utambulisho wa mradi wa kupunguza vifo vya kuzama majini katika Ziwa Victoria unaosimamiwa na shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo EMEDO.

Akizungumzia sababu zinazochangia kuongezeka kwa ajali za majini Mwenyekiti wa  kikundi shirikishi cha usimamizi wa rasilimali za uvuvi (BMU) Kome,Piudi Kigomasige ameitaka serikali ianze kuchukua takwimu za madhara yanayowapata wavuvi ili matukio ya kuzama na hata wanaokufa maji yaweze kujulikana na kutafutiwa ufumbuzi wa kuyamaliza mapema.

"Mimi naishauri kwa ofisi za takwimu wilaya waanze sasa kukusanya takwimu kila robo ya mwaka na kuwe na ushindani kati ya kata hizi mbili za Bukumi na Bwasi ili tuweze kujua ni sehemu ipi ambayo ina matukio mengi zaidi ya kufa maji au kuzama majini".alisema Kigomasige.

Nae Hamisi Hamisi Afisa Msaidizi wa Jeshi la Polisi wilaya ya Musoma amesema tangua aanze kufanyakazi ndani ya jeshi la Polisi hajawahi kusikia takwimu zikitolewa kuhusiana na wavuvi wanaokufa maji zaidi ya takwimu za doria zinazoonyesha idadi ya Mitumbwi iliyoshikwa,Nyavu haramu zilizoshikwa pamoja na Viripuzi haramu vinavyotumiwa na baadhi ya wavuvi.

Akizungumzia sababu za kukosekana kwa takwimu hizo afisa takwimu wilaya ya Musoma Victor Nyamhanga amezitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kutokusanywa kwa taarifa hizo,Vifo vya majini kuripotiwa kama maafa na sio ajali pamoja na halmashauri kutokuwa na mfumo wa kurekodi ajali hizo.

"Mfumo uliopo kiukweli umejikita zaidi katika kukusanya takwimu za mazao ya ziwani na ndio maana unaona nguvu kubwa huwa katika maeneo hayo tu na sio katika eneo hili la ajali za majini,kwa maeneo hiyo kuna haja ya kuanzisha sera itakayoangalia usalama wa wavuvi wawapo majini".alisema Nyamhanga.

Nyamhanga amesema kutokana na mapungufu hayo wao kupitia ofisi ya takwimu watashirikiana na EMEDO kupeleka mapendekezo serikalini ili kuanzisha mfumo wa kukusanya takwimu za ajali za majini ambazo zitaisadia serikali kujua sababu ya ajali hizo na namna gani ya kupambana nazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo EMEDO Editrudith Lukanga amesema kupitia mradi huo wa miaka mitatu wa kupuguza ajali za kuzama majini wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kuangalia namna ya kuanza kukusanya takwimu za ajali za majini ili iwe rahisi kujua ukubwa wa tatizo na namna ya kukabiliana nalo.

"Huu mradi ufanisi wake unategemea sana ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali ikiwemo Wizara,Halmashauri na hata watendaji wa kata wote na wote tumekuwa tukiwashirikisha katika kila hatua ya mradi huu, tunatakiwa kuamini kabisa kuwa  Kuzama kunazuilika cha msingi ni kuchukua tahadhari tu".alisema Bi Lukanga.

Akifunga kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Mtendaji wa wilaya ya Musoma Mwita Hamisi Mwita amelipongeza shirika la EMEDO kwa kuupeleka mradi huo katika wilaya Musoma hasa katika vijiji vya Busekela na Kome ambako kuna wavuvi wengi ambao watanufaika na mradi huo.

No comments