ILEMELA YAOMBA WADAU KUSAIDIA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO
Na Tonny Alphonce,Mwanza
Mkuu wa
wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza Hassan Masala amewataka wadau wanaofanyakazi na
kundi la wanawake na Watoto mkoani Mwanza kushirikiana na Serikali katika
kuhakikisha vitendo vya ukatili vikiwemo vya unyanyasaji watoto kijinsia
vinakomeshwa.
Akizungumza
katika kikao cha kujadili hali ya vitendo vya ukatili kwa wilaya ya Ilemela
kilichoandaliwa na shirika la Wadada Solution Mh Masala amesema ofisi yake
imekuwa ikipokea taarifa mbalimbali kutoka mitaani ambapo kuna Watoto
wameripotiwa kubakwa pamoja na matukio ya mimba za utotoni.
‘Twendeni
tushirikiane kuibua matendo yanayofanyika mtaani kwetu,twendeni tuendelee
kupaza sauti kwa waathirika kwa sababu kuna hata wazazi wanaficha matendo
wanaofanyiwa Watoto sasa haya yote yanatakiwa kuwekwa wazi ili serikali ijue
namna ya kupambana na vitendo hivi’.alisema Masala.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa shirika la Wadada Solution Lucy John amesema wameendelea
kutoa elimu mbalimbali za namna ya kukomesha vitendo vya kikatili kama ambavyo
wameweza kutoa elimu hiyo kwa wadau mbalimbali wanaogusa makundi ya wanawake na
Watoto.
‘Pengo
ambalo tumeliona ni ukosefu wa elimu katika familia nyingi kuhusu suala zima la
malezi na ndio maana vitendo vingine vingi vinatokea katika familia zetu na kwa
sasa kazi kubwa tunayoifanya ni kutoa elimu hii’.alisema Lucy.
Elihaika
Josphat ambae ni afisa mradi wa mradi wa kijana paza sauti chukua hatua amesema
katika kuhakikisha taifa linakuwa na wazazi wanaojitambua wamekuwa wakitoa
elimu ya uzazi katika kata za wilaya ya Ilemela ambazo ni
Sangabuye,Shibula,Bugogwa na Kitangili.
Elihaika
ameitaka jamii kuripoti matendo yote ya kikatili katika ngazi mbalimbali
zikiwemo za nyumbani na hata mashuleni ambako vitendo hivi vimeripotiwa
kufanyika kwa wingi.
Wakati wilaya
ya Ilemela ikiwaomba wadau kusaidia kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto
inaelezwa kuwa kuna upungufu wa utoaji taarifa za kesi za unyanyasaji na
utelekezaji wa Watoto kuanzia umri 0 – 8.
Kuna utafiti
mdogo ulifanywa kwenye jamii kuhusiana
na kesi za ukatili ,unyanyasaji,utelekezaji na unyanyasaji wa Watoto wadogo uliofanywa na wazazi na walezi.
Utafiti uliofanywa
na Benki ya Dunia katika mkoa wa Katavi ulionyesha asilimia 18 ya wazazi wenye Watoto
chini ya miaka mitatu huwapiga vibao Watoto wao hali kadhalika asilimia 5 ya
wazazi walionekana wakiwapiga vibao wakati wa utafiti wenyewe.
Ripoti ya
shirika la kimataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) inayohusiana na ukatili dhidi
ya watoto Tanzania inaonyesha kuwa msichana 1 kti ya 3 na Mvulana 1 kati ya 3
wanapitia aina mbalimbalin za ukatili kingono kabla hawajafikisha miaka 18.
No comments