EMEDO YAIOMBA SERIKALI KUONDOA USHURU WA VIFAA VYA UOKOAJI MAJINI ILI KUNUSURU MAISHA YA WAVUVI
Na Tonny
Alphonce,Mwanza
Serikali imeombwa kuondoa ushuru kwa bidhaa za uokoaji
majini ili kutoa nafasi kwa wavuvi na wasafiri wa majini kununua bidhaa hizo
kwa bei ya kawaida.
Ushauri huo umetolewa na mratibu wa mradi wa kupunguza
ajali za kuzama majini wa shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo
Tanzania (EMEDO) Arthur Mugema wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini
kwake.
Arthur amesema kutokana na vifaa vya kuzuia kuzama
watu majini zikiwemo Jaketi maalumu kuwa bei ghali wavuvi wengi hukimbilia
kununua Jaketi za bei nafuu ambapo ajali ikitokea Mvuvi anaweza kuzama na kufa
maji kutokana na Jaketi aliyonayo kutokuwa na ubora unaotakiwa.
Amesema kutokana na kipato cha wavuvi kutokuwa kikubwa
ni vema Serikali ikaangalia uwezekano wa kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vyote
vya usalama vinavyotumika majini ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaofanya shughuli
zao za kiuchumi majini.
Arthur amesema Jaketi lenye ubora na usalama linauzwa kuanzia shilingi 40,000 hadi 50,000 kiasi ambacho ni kikubwa kiasi kwamba Wavuvi wadogo hawawezi kumudu gharama hiyo.
“Ukiachilia mbali Imani za kishirikina za kukataa
kuvaa majaketi ya kuwazuia kuzama lakini na bei nayo ni kikwazo kikubwa hivyo wavuvi wengi huamua kutovaa na matokeo
yake ajali inapotokea wengi wao hufariki dunia.”alisema Arthur.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa EMEDO Editrudith Lukanga amesema
katika kuhakikisha jitihada zinachukuliwa za kupunguza vifo vya majini tayari
shirika la EMEDO kwa kushirikiana na Taasisi kutoka Wingereza inayohusika na
masuala ya usalama kwenye maji na uokoaji RNLI wameingia mkataba wa miaka
mitatu wa kusaidia jamii za wavuvi.
“Eneo hili la ajali za majini limesahaulika
kiukweli mara nyingi tumekuwa tukisikia au kuona elimu ya usalama barabarani
inatolewa au takwimu za ajali za barabarani zikitolewa lakini ajali za majini
huoni jitihada kubwa zikichukuliwa kuhakikisha ajali hizo hazitokei”.alisema Bi
Lukanga
Amesema Mradi huu ni wa kwanza kutekelezwa Ziwa
Victoria na Unagharimu shilingi Bilioni 2.7 na
unatekelekelezwa kwa miaka mitatu ukilenga kupunguza hatari za kuzama
majini kwa jamii ya Wavuvi waliko mikoa ya Mwanza,Kagera na Mara.
“Tayari tumeanza kutekeleza mradi huu na vijana
wetu tayari wapo kazini ambapo wengine wapo mkoani Kagera kwa sasa na
tunaendelea kutekeleza mradi huu tukishirikiana na serikali.”alisema Bi Lukanga.
Wavuvi laki moja wanaofanya shughuli zao na kuishi pembezoni mwa Ziwa Victoria ,Mia mbili Thelathini na Moja, kati yao wanapoteza maisha kwa mwaka kwa kuzama majini.
Shirika la EMEDO ni miongoni mwa wadhamini wa Usiku wa
Waandishi wa habari na Wadau wa habari unaoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa
habari Mkoa wa Mwanza utakaofanyika Mwanza tarehe 03/06/2022 katika ukumbi wa
Rock City Mall.
No comments