WATOTO 92,698 KUPATIWA CHANJO YA POLIO NYAMAGANA MKOANI MWANZA
Na Tonny Alphonce, Mwanza.
Watoto zaidi ya 92,698 wenye umri wa chini ya miaka
mitano wa wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone
ya ugonjwa wa Polio ikiwa ni jitihada za Serikali kuutokomeza ugonjwa huo ambao
husababisha ulemavu wa kudumu kwa mtoto.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo kwa
wilaya ya Nyamagana uliofanyika leo tarehe 18/05/2022 katika kata ya Mkolani,Mkuu
wa Wilaya ya Nyamagana Bibi Amina Makilagi amesema ili kufanikisha zoezi hilo wataalamu
watapita katika makazi ya watu,sehemu zenye mikusanyiko na katika maeneo ya
ibada ili kila mtoto aweze kupatiwa chanjo hiyo.
Bi. Makilagi amesema maamuzi ya kuwafata wazazi na walezi
kule walipo itawapunguzia Wazazi umbali wa kupata huduma hiyo lakini pia itawasaidia
wataalamu kujua idadi kamili ya watoto watakaopatiwa chanjo kwa wilaya ya Nyamagana.
“Kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika
mkoa wetu wa Mwanza ambao wanatoka nchi za jirani kuna uwezekano mkubwa wa
kupata maambukizi hivyo wazazi lazima mkubali watoto waweze kupata chanjo
vinginevyo watoto wetu watapata ulemavu na mimi nimewahi kuwaona wazazi
waliokaidi kuwachanja Watoto wao baada ya miaka michache kupita wakapata
ulemavu.”alisema Bi Makilagi.
Amesema ugonjwa wa Polio unaambukizwa na kirusi kiitwacho
Polio,ugonjwa huu unaweza kumpata mtu yoyote katika umri wowote ila kundi la watoto
huathirika zaidi kutokana na kinga zao kuwa chini.
Bi. Makilagi mesema kirusi hiki kinaweza kuingia mwilini kupitia
kwenye chakula,Maji au vitu mbalimbali ambavyo vimechafuliwa na virusi hivyo
ambavyo vikiingia mwilini hukaa kwenye utumbo na kuanza kuzaliana na mwisho
husababisha ulemavu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa jiji la Mwanza Daktari Sebastian Pima amesema hamasa ya wazazi ni kubwa tofauti na chanjo zingine kwa
kuwa wazazi wengi wamejitokeza kwaajili ya kuhakikisha watoto wao wanapata
chanjo.
Daktari Pima amesema chanjo hii ya Polio itatolewa kwa
siku 4 kuanzia leo tarehe 18/05/2022 hadi tarehe 21/05/2025 ambapo wazazi
wanaweza kuwapeleka watoto wao katika vituo vilivyoainishwa pamoja na kwenye
vituo vya afya vilivyo karibu nao.
Mzazi Zena Zuberi mkazi wa kata ya Mkolani Jijini
Mwanza,amesema chanjo ya Polio haina shida kwa kuwa anaijua na watoto wake wote
wamewahi kuchanjwa na hawakupata matatizo yoyote hadi wamekua watu wazima hivi
sasa.
“Bado wengine wanatuambia hawataki watoto wao
wachanjwe lakini hii chanjo ni ya kawaida hadi sasa mimi sijui kwa nini
hawataki kuchanja wakati karibia watanzania wote tumechanjwa chanjo ya Polio”alisema
Zena.
Nae Tunda Sabi au mama Hamisi amesema ameamua
kumpeleka mtoto wake akapate chanjo kwa kuwa ni haki yake ya msingi lakini pia
ni maelekezo ya Serikali hivyo hana budi kutekeleza zoezi hilo ambalo limeanza
wilayani Nyamagana.
Mama Hamisi amewaka wazazi kuwapeleka watoto wakapatiwe
chanjo kwa kuwa mtoto asipopata chanjo hii ni wazi familia ndio itakayoathirika
endapo mtoto atapata ulemavu wa kudumu utakao sababishwa na kirusi Polio.
Hatua hii ya kampeni ya chanjo kwa mkoa wa Mwanza inafanyika
wakati nchi ya Malawi ikiwa imeshambuliwa na mlipuko wa ugonjwa huo kuanzia
February 17 mwaka huu baada ya mtoto mmoja
kutoka mji mkuu wa Lilongwe kudhibitika kuwa na ugonjwa huo.
Kuanza kwa kampeni hii mkoani Mwanza itasaidia kuzuia
ugonjwa huo wa Polio usiingie nchini na hasa mkoani Mwanza kwa kuwa kuna
mwingiliano wa kibiashara na huduma kutoka nchini Malawi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya mara ya
mwisho Tanzania ilipata ugonjwa wa Polio mwaka 1996.
Kampeni hii
ya chanjo ni utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 1990 ambayo inatoa kipaumbele
katika utoaji huduma za kinga, tiba,uhamasishaji na utengano ambapo huduma hizi
hutolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Katika utoaji
huduma hizo,msisitizo umeelekezwa katika utoaji wa chanjo, elimu ya afya na
kuruhusu upatikanaji wa huduma hizo bila malipo.
Taarifa ya hali ya Malezi Jumuishi nchini Tanzania inaonyesha uwekezaji wa Serikali katika uhai wa mtoto unaonekana dhahiri kupungua kwa vifo vya watoto kati ya mwaka 2010 na 2015.
Credit:Nicolas Kajoba (picha ya matone)
No comments