VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO BADO TATIZO MWANZA, WANAUME WARIPOTIWA KUTELEKEZA FAMILIA ZAO
Na Tonny
Alphonce, Mwanza.
Imeelezwa kuwa matukio ya Ukatili dhidi ya Watoto yameendelelea
kuongezeka Mkoani Mwanza na kufikia 31 huku matukio ya wanaume kutelekeza
familia yakiripotiwa 28 katika kipindi cha mwezi januari na march mwaka huu.
Faraja Mkinga ambae ni Mkuu wa dawati la Jinsia na watoto
mkoani Mwanza ameyasema hayo katika kikao maalumu cha wajumbe wa Mpango Kazi wa
Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Faraja amesema ukatili ambao watoto wamekuwa
wakifanyiwa ni pamoja na vipigo vilivyopitiliza pamoja na matukio ya kuingiliwa
kimwili ambapo matukio 19 ya ulawiti yaliripotiwa.
Kwa upande wa matukio yaliyowagusa wanawake na watoto wachanga,Faraja
ameyataja kuwa ni matukio 92 ya ubakaji, shambulio kwa
mwenzi 13, kutoa mimba matukio 3 na tukio moja la kutupa mtoto.
Amesema katika orodha matukio ya ukatili wa kijinsia
yaliyoripotiwa kwenye Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Mwanza
katika kipindi cha miezi mitatu ni matukio 347 ya ukatili wa kijinsia huku 96
kati yake yakiwa ni matukio kuwapatia wanafunzi mimba.
Akielezea sababu za matukio mengi kuripotiwa tofauti
na miaka ya nyuma amesema kwa sasa jamii imepata elimu ya kutosha kuhusia na
vitendo vya ukatili hivyo kupelekea kutoa taarifa katika vituo vya Polisi pindi
matukio yanapotokea.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki
za Wanawake na Watoto la Kivulini, Yassin Ally ameitaka jamii kubadilika katika
suala zima la malezi ili kuwa na jamii yenye hofu ya Mungu na hivyo kuchangia
kupunguza matukio hayo.
Yasini amesema wimbi la vitendo vya
Ulawiti,Ulevi,Utoro na Madawa ya kulevya limeanza kuingia katika shule za
msingi zilizopo katika kata ya Mirongo jijini Mwanza hivyo kuitaka jamii
wakiwemo viongozi wa dini na serikali kuchukua hatua za haraka ili kuwanusuru Watoto
walioko mashuleni.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Makanisa
mkoani Mwanza, Dkt Robert Bundala amesema mmonyoko wa maadili ,wazazi kutokuwa
na muda wa kutosha kuwa karibu na watoto kunachangia kutokea matukio ya
kikatili hivyo ameitaka jamii kuwa na hofu ya Mungu na kumrudia Mwenyezi Mungu
ili kuepukana na vitendo hivyo.
“Ukiangalia suala hili katika ulimwengu wa kiroho
unaona kabisa matendo haya yote yaliyoripotiwa hapa yana shetani ndani yake na
pia kukosekana kwa upendo wa kweli katika familia zetu kama mama atampenda baba na watoto kuwapenda
wazazi wao litakuwa ni suluhisho la kudumu katika kukabiliana na ukatili”.alisema
Dkt Bundala.
Isack Ndasa afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Mwanza kwa
upande wake amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na Watoto wao na kuwadadisi
changamoto wanazokutananazo shuleni na mtaani ili waweze kuwasaidia mapema kabla
hawajaathirika.
Katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake
na Watoto,Serikali iliandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto wa mwaka 2016/17 – 2021/22 (MTAKUWWA).
Mpango huu jumuishi unalenga kutokomeza ukatili kwa
kina ukiwa na afua ambazo zimelenga Elimu ya malezi,usalama shuleni,utekelezaji
wa sheria,mazingira salama katika maeneo ya umma na maeneo mengine.
No comments