UNFPA NA WADAU WA AFYA KUENDELEA KUSAIDIA MAPAMBANO YA UGONJWA WA FISTULA NCHINI
Na Tonny Alphonce, Mwanza.
Umbali wa
huduma za afya,Kukosekana kwa huduma ya dharura kwa mama anapojifungua mbali na
kituo cha afya,kukosekana kwa elimu dhidi ya ugonjwa wa Fistula na upasuaji
usio salama ni sababu moja wapo zilizotajwa kusababisha ugonjwa wa Fistula.
Meneja miradi ya afya ya uzazi Mama na Mtoto kutoka Shirika la umoja wa mataifa afya ya uzazi (UNFPA) Felister Bwana akitoa salamu za Shirika la UNFPA katika maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani.
Hayo
yamesemwa na Meneja miradi ya afya ya uzazi Mama na Mtoto kutoka Shirika la
umoja wa mataifa afya ya uzazi (UNFPA) Felister Bwana wakati wa maadhimisho ya
siku ya Fistula Dunia yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza tarehe 23/05/2022
katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Felister
amesema katika kukabiliana na ugonjwa huo wa Fistula ambao chanzo kikubwa ni
uzazi pingamizi UNFPA imekuwa ikiwapatia mafunzo madaktari ili waweze kupata
utalaam wa kumzalisha mama salama,kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa lengo
kuzuia mimba katika umri mdogo na kuhakikisha huduma za dharura kwa mama
mjamzito anayepata uzazi pingamizi aweze kusaidiwa kwa haraka na hatimaye
ajifungue salama.
“Kwa
hiyo sisi UNPA tunawekeza rasilimali, pesa,ujuzi na utaalamu kupitia wizara ya
afya kuhakikisha hayo mambo matatu yanatekelezeka,kwa sababu tukiweza kuyafanya
hayo mambo matatu ni wazi tutapunguza vifo vinavyotokana na uzazi lakini
tunakuwa tumezuia Fistula”.alisema Felister.
Kwa upande
wake Dkt Issa Rashid kutoka CCBRT amesema wao wameitekeleza kwa vitendo kauli
mbiu ya mwaka huu inayosema Tokomeza Fistula,Wekeza Imarisha huduma ya afya na
Wezesha Jamii kwa kuzindua hospital mpya ya kina mama na wajawazito yenye uwezo
wa kubeba wagonjwa kuanzia 200 wakiwemo wale wenye Fistula.
Dkt Issa
amesema hospital hiyo itakapoanza kufanyakazi itawahudumia wanawake wenye
historia ya fistula,wanawake walemavu na mabinti wanaopata mimba chini ya miaka
20 bila malipo kwa lengo la kuzuia fistula mpya,Ulemavu na vifo vya mama na
mtoto.
Amesema
CCBRT tangu ianze mapambano ya kutoa matibabu ya Fistula mwaka 2003 wagonjwa
zaidi ya 8000 walitibiwa kwa mafanikio makubwa na zaidi ya asilimia 90 kati yao
walirudi nyumbani wakiwa wamepona na kubadilisha maisha yao.
Akizungumza
na wananchi mgeni rasimi katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Tiba Asili na Mbadala kutoka wizara ya afya Dkt Paul Mhame amesema jitihada za wadau
zinaonekana kuzaa matunda kwa kuwa ugonjwa wa Fistula umepungua kwa asilimia 30
ukilinganisha na mwaka 2015 na 2019.
Akizungumzia kushuka kwa idadi ya wagonjwa
Fistula Dkt Mhane amesema idadi hiyo imeshuka kutokana na kuimarika kwa huduma
za afya kwa mama wajawazito na upatikanaji wa huduma za upasuaji za dharura
ambao unatolewa katika hospitali zaidi ya tano hapa nchini.
Naye
Mkurugenzi wa Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dkt Fabian Massaga amesema
uzazi pingamizi unaweza kuzuilika kwa kuwa viashiria vyake vinajulikana ikiwemo
mama mjamzito anapokaribia kujifungua asindikizwe hospital ili akipata tatizo
msindikizaji anaweza kumsaidia mama na hatimaye kuzuia Fistula.
Dkt Massaga
amesema takwimu za mwaka2020/2021 zinaonyesha
hospitali ya Rufaa ya Bugando inapokea wagonjwa wa Fistula 300 hadi 400
kwa mwaka ambao hupatiwa huduma za upasuaji kwaajili ya kuhakikisha wanarudi
katika hali yao ya kawaida.
Muhanga wa
ugonjwa wa Fistula Neema Constantine ameitaka serikali na wadau wa afya
kuendelea kutoa elimu ya uelewa kwa jamii kwa kuwa bado wanawake wengi hawaujui
ugonjwa huu wakiuhusisha na Imani za kishirikina na hivyo baadhi yao hupoteza maisha
na kuacha Watoto wachanga wakikosa malezi muhimu ya mama.
Neema
amesema alipitia mateso makubwa alipopatwa na ugonjwa huo mara baada ya
kujifungua ambapo alichanika vibaya na alivyofanyiwa upasuaji na kushonwa hali
ilikuwa mbaya kwa kuwa upasuaji hakwenda vizuri na hivyo kuanza kutokwa na haja
kubwa katika sehemu zake zote za siri bila kujitambua.
Zaidi ya
wanawake 3000 nchini wanapatwa na ugonjwa wa Fistula kila mwaka mara baada ya
kujifungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya mama kuugua uchungu kwa
muda mrefu kabla kujifungu.
Shinikizo
la muda mrefu linalotokana na kichwa cha mtoto kulazimisha kutoka na kusababisha
kovu kubwa ambalo hugeuka shimo katika njia ya uzazi na kusababisha mama kuanza
kutokwa na haja ndogo na kubwa bila kujitambua.
Fistula
inachangia asilimia 8 ya vifo vya uzazi,asilimia 90 ya visa vya kujifungua
Watoto wafu ,hii ni Kwa mujibu wa shirika la UNFPA.
No comments