SARATANI YA JICHO BADO NI HATARI KWA WATOTO, WAZAZI WATAKIWA KUWAFANYIA WATOTO UCHUNGUZI MAPEMA
Na Tonny
Alphonce, Mwanza.
Imeelezwa kuwa Saratani ya JICHO ni moja ya Saratani
inayoongoza kuwashambulia Watoto nchini ambapo kidunia kumekuwa na wagonjwa
wapya takribani 9000 kila mwaka ikiwa ni sawa
na mgonjwa mmoja kwa kila watoto elfu 15 wanaozaliwa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi na Utumishi Lilian
Shao wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando katika hotuba yake wakati maadhimisho ya
wiki ya Saratani ya Jicho ambapo amesema kuchelewa kufanyiwa uchunguzi mapema
kwa Watoto wanaopata matatizo ya macho kunasababisha asilimia 50 ya watoto kushambuliwa
na Saratani ya Jicho na hata kupoteza Maisha.
Amesema kwa hospital ya Bugando Takwimu za mwaka 2021
zinaonyesha Watoto 46 walitibiwa,Watoto 8 sawa na asilimia 18 hawakuendelea na matibabu kutokana na sababu mbalimbali,Watoto 13 sawa na asilimia
28 walipoteza Maisha na Watoto 25 ambao ni sawa na asilimia 54 walipatiwa
matibabu na kupona.
"Hivi karibuni tutafungua kliniki yetu mpya ya
kisasa yenye vifaa vya kisasa ambapo wagonjwa wetu watahudumiwa katika
mazingira mazuri zaidi,na niwakumbushe wazazi ukiona mboni nyeupe au kengeza
kwenye jicho la mtoto hiyo ni dalili ya saratani ya jicho mlete mtoto afanyiwe
uchunguzi mapema ili atibiwe na tuweze kupunguza vifo vya Watoto vinavyotokana
na saratani".alisema Shao
Kwa upande wake Daktari Mbobezi wa Magonjwa ya
Saratani Heroniam Joas amesema ugonjwa wa Saratani ya jicho kwa Watoto ni
tatizo kubwa ambapo takwimu kwa mwaka jana zinaonyesha kwa ujumla Watoto
waliopata kansa ni 250.
Dkt Joas amesema Saratani za Watoto mara nyingi hazina
sababu kama ilivyo kwa Saratani za watu wakubwa ambao hupata saratani kutokana
na sababu mbalimbali ikiwemo unywaji wa pombe,uvutaji wa Sigara au ulaji wa
vyakula vinavyoweza kusasababisha saratani.
"Japo hakuna Ushahidi wa kutosha lakini inaonyesha
kuwa sababu zinazoweza kusababisha Saratani ya Jicho mtoto anaweza kuzipata
kutoka kwa wazazi wake,vinasaba vya mzazi vinapobadilika na kupita na kwenda
kwa mtoto kunaweza kusababisha mtoto kupata saratani,mtoto akipigwa na mionzi
na umri wa wazazi ukienda sana kwa wazazi inaweza ikawa sababu ya mtoto kupata
hiyo saratani ya Jicho."Alisema Dkt Heroniam.
"Matibabu ya Saratani ya Jicho ni magumu yanahitaji
ushirikiano mkubwa kati ya madaktari na wazazi maana kuna wakati baada ya
uchunguzi wakati mwingine hutulazimu kutoa jicho la mtoto nah apo ndio mvutano
hutokea,mzazi anaweza akagoma jicho la mtoto wake lisitolewe wakati tunatakiwa
kuokoa uhai wa mtoto lakini angalau jicho moja litoke na mtoto aendelee na
Maisha".Alisema Dr Mgaya.
Daktari Christopher Mwananjao ambae ni Mkurugenzi wa idara ya macho
katika hospitali ya Bugando amewapongeza wazazi ambao wanaendelea kuwa
wavumilivu na kufatilia matibabu ya Watoto wao ambapo wengine wamepona na
wamerudi shule na kuwataka wazazi hao kuwa mabalozi kwa kutoa elimu kwa wazazi
wengine kuwapeleka Watoto Bugando kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi.
Diana John ambae ana mtoto mwenye Saratani amesema
changamoto kubwa ya matibabu ya Saratani ya Jicho anayopata ni muda wa matibabu
ambao unachukua muda wa miezi sita hadi saba na wakati mwingine mzazi huitajika
kununua miwani ambayo ni gharama kubwa hali ambayo husababisha wazazi wengi
kuingia kwenye madeni makubwa.
"Tulianza wengi hapa wazazi ambao walifika
kwaajili ya matibabu,wengi walikimbia tulipoanza tu matibabu na wengine
wamepoteza Watoto wao baada ya kukatiza matibabu yaani wamekuja kurudi kwenye
matibabu hali yam toto tayari mbaya".Alisema Diana.
Naye Nariba Luwecha mkazi wa Geita amewaomba wasamalia
wema wamsaidie ili aweze kuendelea na matibabu ya kansa ya jicho kwa mtoto wake
ambapo kwa sasa hawezi kupata nauli ya kuhudhuria Kliniki kila anapopangiwa
kutokana na ugumu wa Maisha alionao.
Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambayo inashirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma inatekeleza sera ya Afya 2007 ambayo imelenga kuboresha uhai wa mtoto kupitia utoaji huduma bure za afya kwa kina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano kama Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali Awali ya Mtoto inavyoelekeza.
Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuboresha Afya ya Uzazi,Mzazi,Mtoto
na Vijana nchini Tanzania (2016 – 2020)
umewekeza mazingira wezeshi ya kupunguza magonjwa,vifo vya kina
mama ,Watoto wachanga,Watoto na vijana kwa kutoa huduma bora endelevu na
jumuishi zinazowafikia watu wote katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma
katika vituo vya afya na kwenye jamii.
No comments