Umoja wa Kitaifa wa Wanawake Wavuvi (TAWFA) Ilemela na Nyamagana ,Watakiwa kuwatumia Wataalamu kutoka Halmashauri.
Na Tonny Alphonce,Mwanza.
Umoja wa Kitaifa wa Wanawake Wavuvi (TAWFA) wa wilaya
za Ilemela na Nyamgana jijini Mwanza waliochaguliwa kuongoza umoja huo
wametakiwa kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake
Wavuvi na wachakataji wa Dagaa kwa kuwatumia wataalamu waliopo katika
halmashauri zao.
Kauli hiyo imetolewa na afisa maendeleo ya jamii mkoa
wa Mwanza Isack Ndasa wakati akifungua kikao cha kuwapata Wawakilishi wa TAWFA wa
wilaya za Ilemela na Nyamagana.
Bwana Ndasa amesema wanawake wavuvi na wachakataji wa
Dagaa wanatakiwa wajiamini katika utendaji wao wa kazi kwa kuwa bila wao jamii
inaweza isipate mazao ya Samaki yaliyo bora na hata halmashauri inaweza
ikapoteza mapato kama wanawake wakiamua kuacha kufanya shughuli za kiuchumi.
Amesema hata takwimu za kundi linaloongoza katika
ufanyajikazi za kiuchumi kwa Tanzania bado ni kundi la wanawake linaloongoza kwa asilimia
75 hivyo amewataka wanawake wasiwe wanyonge mbele ya mteja na badala yake watafute faida katika kazi hizo wanazofanya.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Usimamizi wa
Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Eltrudith
Lukanga amewataka viongozi hao wakahakikishe wanajenga taasisi imara ya
wanawake katika ngazi hiyo ya wilaya kwa kuanza kushungulikia kero walizonazo
wanawake wachakataji.
Bi Lukanga amesema EMEDO kwa ushirikiano na Wizara ya
Mifugo na Uvuvi wataendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa TAWFA ili
kuhakikisha mazingira wezeshi
yanapatikana kwaajili ya uvuvi endelevu utakaowasaidia wavuvi wadogo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo Lucy Kilanga amesema
viongozi hao wanne ambao wamechaguliwa watakuwa na jukumu la kutatua kero za
wanawake wachakataji walioko katika ngazi hiyo ya wilaya.
Wawakilishi wa TAWFA waliochaguliwa kutoka Nyamagana
ni Angelina Deogratius na Catherine Fransis na kwa upande wa Ilemela ni Maimuna
Rajabu na Ela Livingstone.
No comments