Breaking News

‘NAHISI BAADHI YA VIONGOZI WANATATIZO LA LISHE'.MKUU WA MKOA MWANZA

Na Tonny Alphonce,Mwanza.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amewataka wataalamu wa afya kuangalia namna ya kuwasaidia watumishi wanaoshindwa kutekeleza maagizo wanayopewa na viongozi wao kwa sababu huenda wana tatizo la lishe.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akiongea na wajumbe walioshiriki kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe mkoa. 

Kauli ameitoa wakati akifungua kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe mkoa wa Mwanza ambapo baadhi ya halmashauri hazijatenga fedha za lishe licha ya mkataba  kuwataka kufanya hivyo.

Mhandisi Gabriel amesema inavyoonekana baadhi ya viongozi bado hawajalielewa  suala la lishe na huenda na wao wanachangamoto za lishe kwa kuwa kama mnakubaliana kufanya jambo halafu halifanyiki hilo nalo ni tatizo la lishe na kuwataka wataalamu wa afya kuangalia namna ya kuwasaidia.

Amesema ili kuwa na taifa imara,mathubuti lenye kupiga hatua katika nyanja zote za kimaendeleo huwezi kupinga ukweli kwamba suala la lishe ni mapambano na lazima kulitekeleza kwa kuwa tayari ni makubaliano.

‘Kama mkoa tumeanza kuchukua hatua wewe haujatoa fedha za lishe haujaunga mkono mapinduzi ya mageuzi haya unakuja kufanya nini hapa? unachoma gari mafuta ya nini ?mngetoa mafuta ya gari wote hiyo pesa mngeweka kwenye lishe mmetoa shilingi sifuri halafu mnakuja kwenye kikao bila kutimiza haya hayakubaliki.alisema Mhandisi Gabriel’

Amesema Serikali kwa kutambua lishe sasa ni suala la kimaendeleo hapa Tanzania mapambano dhidi ya Lishe duni yamekuwa moja wapo ya maeneo ya kipaumbele katika mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano 2021/2022 mpaka 2025/2026 mpango unaolenga kutekeleza dira ya maendeleo ya mwaka 2025.

Mhandisi Gabriel amesema serikali ya awamu ya sita inatambua umuhimu wa kuwekeza katika lishe kama msingi imara ya kuwa na jamii yenye afya bora katika utendaji wa kazi lengo likiwa kuhakikisha hadi kufikia mwaka2015/ 2025 iwe ni muongozo wa kuchukua hatua katika kutekeleza masuala ya Lishe.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel.

Amesema katika kufikia adhima mkoa wa Mwanza tayari umechukua hatua kwa kuwa na mpango mkakati wa lishe wa mkoa,kutiliana Saini mkataba wa kiutendaji wa lishe baina ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya,kutiliana Saini mkataba wa kiutendaji wa lishe baina ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri na mkuu wa mkoa.

‘Rai yangu kwenu kuhakikisha kila halmashauri itoe fedha za lishe pasipo kutegemea wadau kulingana na idadi iliyopo ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ili kufanikisha utelekelezaji wa afua za lishe,wengine wanasema wanategemea sana wadau ili kukamilisha baadhi ya mipango tuliyojiwekea ,hapana pamoja na kutenga tutoe'.alisema Mhandisi Gabriel.

Amesema mpango mkakati wa lishe wa mkoa utaenda sambamba na program jumuishi ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ambayo itaanza kutekelezwa hivi karibuni katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Mwanza.

"Najua hatujainza program hii ya MMMAM kwa mkoa wetu lakini tayari kuna mipango inaendelea ya utekelezaji wa mpango huu na nimejaribu kuupitia mpango huo nimeona hata tatizo letu la udumavu limeonekana humo japo hatupo kati ya mikoa 11 ambayo inaongoza kwa udumavu kwa maana hiyo lazima tupambane kumalimaliza tatizo la udumavu"alisema Mhandisi Gabriel

Aidha Mhandisi Gabriel amesema fedha zinazotengwa kwenye lishe zilete mabadiliko chanya katika jamii kwa kuboresha mikataba na kutoa viashiria vya mabadiliko katika jamii na kutokuwa na watoto wenye Utapiamlo.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dr Thomas Rutachunzibwa amewataka washiriki wakikao hicho kuacha kujificha kwenye kivuli cha fedha kwakuwa viashiria vingine havihitaji pesa likiwemo lile la kutoa elimu kwa kina mama juu ya umuhimu wa unyonyeshaji.

Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dr Thomas Rutachunzibwa akitoa maelekezo upande wa watumishi wa afya.

Dr Rutachunzibwa amewataka watendaji wote kuanzia watoa huduma ngazi ya jamii,watendaji wa Zahanati na Vituo vya afya kuhakikisha wanasimamia suala hilo la lishe katika ngazi hizo hasa katika mambo yasiyohitaji fedha yaweze kufanyika.

Kuhusu mpango jumuishi ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Dr Rutachunzibwa amesema kwa upande wa wataalamu wa afya tayari wapo vizuri wakiwa na uelewa wa kutosha na mara baada ya mpango huo kuanza utekelezwaji watashiriki vema.

Nae Benedicta Peter afisa lishe wa halmashauri ya wilaya ya Buchosa amesema kwa upande wa Buchosa kuna Watoto ambao wamegundulika kuwa na Utapiamlo mkali kwa asilimia 62.5 kutokana na sababu mbalimbali.

Afisa Lishe wa Hlmashauri ya Wilaya ya Buchosa Benedicta Peter akizungumzia hali ya Lishe katika eneo lake.

Amesema tatizo hilo ni kubwa na kitu ambacho watakifanya ni kuhakikisha wanawasaidia watoto waliochini ya miaka miwili ili wanapata matibabu na kupona kabla hawajafikia hatua ya udumavu usiotibika ambao huwapata watoto wenye umri wa zaidi ya miaka miwili.

‘kuna viashiria ambavyo bado hatufanyi vizuri kwenye uanzishwaji wa klabu za lishe mashuleni kwa sisi Buchosa kule kuna klabu ambazo zipo mashuleni tutazitumia hizo hizo ili walimu kwenye vikao vyao waingize masuala ya lishe kwa sababu hatuwezi kuanzisha klabu tofauti tofauti ili Watoto waanze kujua umuhimu wa kunyonyesha,mlo kamili ni nini,umuhimu wa kuwa na bustani za mboga mboga’alisema Benedicta.

Kulingana na Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya ya mwaka 2015-2016, takriban theluthi ya watoto wote chini ya miaka mitano wana udumavu na asilimia 14 wana upungufu wa uzito. Sababu kuu zinazoongoza kuleta utapiamlo ni ukosefu wa lishe mchanganyiko na bora kwa kila kaya, upatikanaji mbovu wa huduma za afya (pamoja na maji safi na salama, usafi wa mazingira), na mienendo duni ya lishe. Hali ya upungufu wa damu kwa mama ni shida nyingine kubwa nchini Tanzania, ikiwa na asilimia 57 ya wanawake wajawazito na asilimia 46 ya mama wanaonyonyesha wanaathiriwa.

No comments