WAZAZI WAWATELEKEZA WATOTO ZAIDI YA 40 WENYE UALBINO KITUONI.
Na Tonny Alphonce,Shinyanga
Watoto zaidi ya 40 wameshindwa kuchukuliwa na wazazi wao kutoka kituo cha shule ya msingi BUHANGIJA kilichopo mkoani SHINYANGA kutokana na wazazi wao kushindwa kuwachukua kwa sababu ya hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo pamoja imani potofu.
Wafanyakazi wa Radio Free Afrika wakiwa na baadhi ya watoto wenye Ualbino ambao wamebaki kituoni hapo kutoka na sababu mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Mwl Mkuu Msaidizi wa shule na kituo cha watoto Buhangija Loyce Daud wakati alipokuwa akipokea msaada wa vitu mbalimbali kutoka kituo cha Radio Free Afrika cha jijini Mwanza.
Mwl Loyce amesema kuna watoto hawajaonana na wazazi wao kwa zaidi ya miaka sita kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi,kifo na imani potofu.
'Hawa watoto mnaowaona hapa ni wachache kwa kipindi cha nyuma walikuwa kibaki watoto miatatu au mia mbili na kitu lakini kutokana na elimu waliyopewa wazazi hivi sasa wamepata mwamko wa kuja kuwachukua watoto wakati wa likizo'.alisema Mwl Loyce.
Mwl Loyce Daud akizungumzia maendeleo ya kituo hicho na changamoto walizonazo katika kituo hicho.
Mwl Loyce amesema kituo hicho ambacho kina walea watoto wenye ulemavu na wale wenye Ualbino,kimekuwa kikipata mzigo mkubwa wa kutelekezewa watoto wenye Ualbino kutokana na watoto hao kuendelea kubaguliwa na wanafamilia ambao huwa hawataki tena mtoto huyo kuonekana kwenye familia.
'Watoto wasiosikia na watoto wasioona wote wameenda likizo waliobaki wote hapa ni wenye ualbino peke yao,wazazi wengine wanakuwa wamekitupia kituo kama mzigo hawataki kuwaona tena na kwa mila za kisukuma ni ngumu mtu kwenda kuoa kwenye familia ambayo ina mtu mwenye Ualbino ndio maana baadhi ya familia ikishamfikisha mtoto kituoni haitaki tena kujua habari zake'.alisema Mwl Loyce.
Mwl Loyce ameitaka jamii kuwapenda watoto wenye Ualbino kwa sababu hawana tofauti na watoto wengine ambao hawana ulemavu na wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao.
Kwa upande wake meneja msaidizi wa vipindi kutoka Radio Free Afrika Yusuph Magasha amesema zawadi ambazo zimetolewa kwa watoto hao ni pamoja na Mchele,Maharage,Sukari,Unga,Mafuta ya kula na kupaka,Sabuni,Taulo za kike pamoja na vitu vingine.
Magasha amesema vitu vyote hivyo ni michango iliyotolewa na wafanyakazi na wadau wa Radio Free Afrika kama sehemu ya kuonyesha upendo wao kwa watoto wanaoishi katika kituo hicho Buhangija.
KITUO CHA BUHANGIJA JUMUISHI kina wanafunzi 920 wakiwemo wenye ulemavu mbalimbali huku watoto wenye Ualbino wakiwa watoto 107.
Credit; Picha kutoka Malunde Blog.
No comments