Breaking News

Tume ya nguvu za atomiki Tanzania yaombwa kutoa elimu kwa Wananchi

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia  Mh Omary Kipanga

Na Hellen Mtereko, Mwanza

Tume ya nguvu za atomiki Tanzania imeombwa kujikita kwenye utoaji wa elimu ya matumizi ya mionzi kwa Wananchi ili waweze kupata uelewa juu ya matumizi bora na salama.

Ombi hilo limetolewa leo hii na  Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia  Mh. Omary Kipanga Jijini  Mwanza kwenye hafla fupi ya  uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa maabara ya ofisi ya kanda ya ziwa ya tume ya nguvu za atomiki Tanzania iliyopo katika kata ya Mkolani.

Amesema wananchi wengi hawana uelewa wa matumizi ya mionzi ni vema wakajikita kutoa elimu ili Wananchi wapate uelewa kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuepukana na athali mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

Pia amewaasa wananchi kuitunza maabara hiyo pindi itakapokuwa imekamilika ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu ambayo itakwenda kupunguza changamoto ya ucheleweshwaji wa vipimo vya mionzi.

Naye Mwenyekiti wa tume za nguvu za atomiki Tanzania Prof.Joseph Msambichaka amesema kuwa mradi wa ujenzi wa maabara ya ofisi ya kanda ya ziwa utagharimu kiasi cha sh bilioni 2.8 hadi kukamilika.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo itasaidia sana kurahisha huduma kwa wananchi ukilinganisha na zamani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya nguvu za atomiki Tanzania Lazaro Busagara amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa katika mtaa wa Majengo uliopo Kata  ya Mkolani umetoa ajira 100 kwa wakazi wa maeneo hayo.


Busagala amesema kuwa, tume itakamilisha ofisi za kanda Mwanza, kama mkakati ulivyopangwa ili kuweza kuendelea kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Ameongeza kuwa wataendelea kuwasimamia wakandarasi wawe na umakini zaidi ili jengo liwe bora na tume itaendelea kusimamia mradi huo ili  ukamilike kwa wakati.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi ambae amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Muhandisi Robert Gabriel, amemshukru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kuchagua Mkoa wa Mwanza kujengwa Maabara hiyo ambayo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kupata huduma za vipimo mbalimbali za mionzi na itakuwa chanzo cha kuchochea maendeleo  katika Wilaya na Mkoa kwa ujumla.

Mwishooo

No comments