Breaking News

Tathimini ya vyombo vya habari ndani ya miaka 60 ya uhuru na jinamizi la kushindwa kutengeneza ajenda.

 


Martin Sturmer katika kitabu chake cha *Media Hostory of Tannzania* , kilichochapishwa Ndanda 1998, kwenye ukurasa wa i ambao ni utangulizi, anaeleza vipindi vinne muhimu vya mapito ya vyombo vya habari.


 *1.Wakati wa ukoloni wa wajeruman* 

 *2.wakati wa ukoloni wa waingereza* 

 *3.Wakati wa vuguvugu la kupigania uhuru/ Nationalist Era* 

 *4.Baada ya uhuru/Post independence.* 

Nimeamua kuandika makala hii fupi ikiwa ni sehemu ya kutunza kumbukumbu ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika na kufanya tafakaru ya wapi tulipotoka, tulipo na nini matamanio yetu ya miaka 60 mingine.

Wakati wa majadiliano ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika tulikuwa na kongamano fupi lililoandaliwa na klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza (MPC) kwa kushirikiana na Mtandao wa watetezi wa Binadamu Tanzania (THRDC).

Kwa upande wangu nilikuwa mchokoza mjadala discussant, hivyo nilichokoza mjadala kwa watoa mada Dr. Rioba, Dr. Rose Reuben na Bibi Hilda Kileo.

Uchokozi wangu uliweka msisitozo kwenye nafasi ya vyombo vya habari kutengeneza ajenda/ agenda setting .

Hapa tuelewane kama ifuatavyo.

 *Utawala wa wajerumani 1890- 1916* 

Vyombo vya habari wakati wa utawala wa wajerumani vilikuwa na ajenda ya kurahisisha mawasiliano baina ya watawala na wataliwa na pia kutukuza tamaduni za wakoloni.

Wakati huo kulikuwa na Magazeti ya serikali, Walowezi na Wamisionari kama gazeti la *Msimulizi* lililoanzishwa mwaka 1888 na lillimilikiwa na Chuo Kikuu cha Agrikana pamoja na *Habari za Mwezi* lililoanzishwa mwaka 1894 yalijikita kwenye maudhui ya kurahisisha mawasiliano na kueneza mila na desturi za kijerumani.

 *Utawala wa waingereza 1916 - 1961* 

Utawala wa waingereza, ajenda kubwa ya vyombo vya habari ilikuwa ni, *kusaidia kurahisisha utawala wa waingereza na kueneza mila na desturi za kigeni pamoja na kukashifu utamaduni wa kiafrika* .

Magazeti kama *The Tanga Post, The voice of Tanganyika, Dar es salaam Times, African Comrade* lililomilikiwa na jamii ya Wahindi na *Mambo Leo* yote yalizalisha maudhui ya kusaidia serikali ya kiingereza kutawala na kufifisha mawazo chanya ya kiafrika.

Baada ya vita vikuu vya Dunia 1945, kuliibuka vyombo vya habari vilivyoanzishwa na waafrika kama gazeti la *Mambo Leo, Kwetu, Mwanafunzi* ambalo lilianzishwa kwa ajili ya kuchochea uenezaji wa kishwahili.

Lakini pia mwaka 1958 baada ya Umoja wa Mataifa kutoa *ripoti maalumu* ya kuwa, Tanganyika ingehitaji miaka 20 hadi 25 ili iweze kujitawala . Hapo ndipo makundi mbalimbali ya wapigania uhuru yaliiibuka na kuanzisha kampeni za kupinga hoja hizo pamoja na kudai uhuru kwa kupitia vyombo vya habari vya vyama vya siasa vilivyokuwa na itikadi za ukombozi.

Baadhi ya magazeti yaliyoanzishwa yalikuwa kama, *Baragumu, Ngurumo, Kiongozi na Sauti ya Tanu.* 

Ajenda kuu ya vyombo hivyo ilikuwa *kupigania kujitawala na kuheshimiwa kwa haki na utu wa mtu mweusi.* 

Ajenda hiyo ilifanikiwa na mwaka 1961 Tanganyika ikapata uhuru wake.

 *Baada ya uhuru 1961 - 1990* 

Baada ya uhuru na pia muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ndipo, Mwalimu Nyerere alitaifisha vyombo vya habari vya watu binafsi na makundi na kuwa chini ya Serikali.

Ajenda ya vyombo vya habari ikawa ni kupigana vita dhidi ya maadui *watatu, ujinga, umaskani na malazi.* 

Ajenda hiyo ilibebwa chini ya falsafa ya *ujamaa* na *kujitegemea* .

Hapo ikaibuka uandishi wa kijamaa/ Socialism Journalism, Chuo cha Kikatoliki cha Nyegezi Mwanza kukaingiza kwenye mtaala wake wa uandishi wa habari masuala la ujamaa na kujitemea na Nchi ikachanja mbuga na kupata maendeleo lukuki kama kuwa na viwanda, kilimo cha biashara na pia vyombo vya habari vikasaidia ukombozi wa Nchi mbalimbali na zikapata uhuru.

Wakati huo vyombo vya habari kama Redio Tanzania Dar es salaam ikawa na vipindi vingi vya kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha., nyimbo za kuhimiza kufanya kazi na kuwajibika zilisikika.

Kiukweli vilifanikiwa sana kwenye ajenda hiyo ya kupigana dhidi ya maadui hao watatu yani ujinga, umaskini na malazi.

 *Vyombo vya habari baada ya mageuzi ya kimfumo na uchumi miaka 1995* 

Alipoingia Rais Ally Hassan Mwinyi na sera za ruksa sera za kibepari zikatawala mambo yakabadilika , vyombo vya habari vya watu binafsi zikaibuka, Redio Free Afrika, ITV na vingine, vyombo vya habari vikaishi kwenye sintafamu kuwa vinataka kuemdelea ujamaa au kusifu ubepari?

Mwinyi akaondoka akafuata Jakaya Kikwete, Benjamin Mkapa na Magufuli hatimaye Samia Suluhu.

Kiukweli tangia awamu zote hizi ukiuliza *ajenda ya vyombo vya habari ni nini?* Itakuwa ngumu kujua.

Vyombo vya habari vya kale na vya kisasa vimeongezeka sana, kuna redio nyingi za kijamii, Runinga za mtandaoni na hata redio za kijamii pia uandishi wa habari wa citizen journalism umeibuka lakini wote hatujui ajenda ya vyombo hivyo ni nini?

Bila shaka mtakubaliana nami kuwa hakuna ajenda iliyopo kwa sasa kwa vyombo vya habari, hii naifananisha na Nchi kukosa mfumo watanzania hatujui tunaishi kwenye mfumo wa kijamaa au kibepari?

Ukiisoma katiba yetu tunajipambanua sisi ni wajamaa lakini maisha yetu ndani ya sera na mifumo ni ya kibepari.

Ni ukweli ulio wazi kuwa, ndani ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika kuna mambo tumefanikiwa kama, kuwa na sera ya habari na utangazaji pamoja na sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017 na zile za Jaji mkuu. Hivi sasa sekta ya habari ni taaluma rasmi, pia kama nilivyoainisha hapo juu kuongezeka kwa vyombo vya habari ni jambo jema, lakini je vyombo vya habari na wanahabari tuna ajenda gani kwa sasa?

Nifanye hitimisho kuwa,

Vyombo vya habari wakati wa mkoloni vilikuwa na ajenda ya kusaidia watawala wa kikoloni kutawala na kutukuza utamaduni na desturi zao, vyombo vya habari wakati wa kupigania uhuru vilikuwa na ajenda ya kuhakikisha uhuru unapatikana na vyombo vya habari baada ya uhuru vilikuwa na ajenda ya kupigana na maadui watatu, ujinga, umaskini na malazi.

Je nyakati tunazoishi vyombo vya habari vina ajenda gani?

Kwa kifupi hadi sasa hatuna ajenda kama vyombo vya habari, je ni ipi Tanzania tuitakayo bila ajenda ya vyombo vya habari?

 *Wasalaamu* 
 *Edwin Soko* 
 *Mwandishi wa habari* 
 *Mchambuzi*

No comments